Na Humphrey Shao, Globu ya Jamiii
Baada ya kurasimishwa kwa iliyokuwa bandari bubu ya
Bagamoyo Mamlaka ya Mapato Tanzania
imeongeza kiasi cha makusanyanyo yake hadi kufikia bilioni 1.2 kwa mwezi huku
mamlaka ya usimamizi bandari TPA ikiingiza hadi sh milioni 33 kwa siku kutoka
sh 600,000.
Hayo yameelezwa jana na Msimamizi wa bandari hiyo kwa
upande wa TPA, Withara Jared Withara, wakati akizungumza na waandishi wa habari
bandarini hapo kuhusiana na hatua walizopiga baada ya kurasimishwa na mpango
uliopo wa kufanya maboresho ya bandari hiyo.
Alisema mapato hayo yanatokana na usafirishaji wa bidhaa
kwenda na kutoka visiwa vya Zanzibar
ambao hufanywa kwa kutumia majahazi ambapo kwa siku moja huweza kuhudumia hadi
majahazi nane na shehena tani 1000.
Alitaja bidhaa zinazosafirishwa sana katika bandari hiyo
kuwa ni mafuta ya kula, mbao, kokoto, vilainishi vya mashine pamoja na mazao ya
chakula kama vile vitunguu, nyanya, hoho n.k. “na bidhaa nyingi zinatoka Zanzibar kuja bara kuliko
zile zinazoenda kule kutoka huku.”
Akielezea historia ya bandari hiyo alisema ilianzishwa
toka enzi za biashara ya utumwa mwaka 1892 baada ya utumwa kukomeshwa ilikuwa
ikitumika kama bandari bubu na baadae ikiwa
inasimamiwa na TRA kitengo cha forodha hadi mwaka 2009 ilipochukuliwa na TPA.
Kuhusu mpango wa maboresho ya bandari hiyo alisema kuna
mpango wa kujenga ukingo kuzuia mmomonyoko pamoja na kuboresha gati iliyopo
ambayo ni ya mda mrefu pamoja na kununua boti ya kufanya ulinzi ili kuzuia
bandari bubu zinazozunguka bandari hiyo.
“Uwepo wa bandari bubu unapunguza majahazi yanayokuja
kwenye bandari yetu na hivyo kupoteza mapato na kuhatarisha usalama wa nchi na
wananchi kwasababu vitu vinaingizwa kimagendo,” alisema Withara.
Mpango wa kufufua bandari bubu ambazo zipo zaidi ya 250
nchi nzima utaongeza mapato ya mamlaka kwa kiasi kikubwa sambamba na kudhibiti
bidhaa za magendo nchini.
Inakadiriwa kuwa jumla ya mapato ya bandari hizo yanaweza
kufikia theluthi moja au nusu ya mapato ya Bandari ya Dar es Salaam.
Bandari ya Dar es Salaam ambayo imefikia kuhudumia shehena
za tani milioni 16.2 kwa mwaka inaingiza Sh bilioni 70 kwa mwaka kwa
mujibu wa takwimu za TPA za mwaka 2017.
Zipo hatua kadhaa zinazochukuliwa katika mpango wa kufufua
bandari bubu ikiwemo kuzianisha, kuwashirikisha wadau, kuzifanyia tathmini,
kuandika ripoti ya kuanisha bandari zenye sifa za kuweza kufufuliwa na kisha
kuipeleka kwa wizara husika kwaajili ya mapitio na kupitishwa.
Kwa sasa zoezi la kuzitambua na kuzianisha zinaendelea na
kwa mujibu wa TPA zoezi hilo
linatarajia mwezi huu na kwamba likikamilika zinaweza kufikia bandari bubu
zaidi ya 300.”
Tayari vikao vimeshafanyikakati ya TPA na wakuu wote wa
mikoa na wilaya ambazo zina bandari bubu na nusu ya viongozi wote wa
vijiji na kata katika maeneo hayo tayari wameshashirikishwa kwenye suala hilo
na vikao vinaendelea.
Ushirikishwaji huo wa wadau umefanyika ili kupata
ushirikiano katika utekelezaji wa usimamizi wa bandari hizo pindi
zitakaporasimishwa na kutopata mapingamizi.
Hatua hii ni miongoni mwa mabadiliko makubwa yanayofanywa
na TPA katika kuhakikisha bandari zinachangia kwa kiasi kikubwq ukuaji wa
uchumi wa taifa.
No comments:
Post a Comment