Thursday, December 27, 2018

RC NDIKILO AWAGEUKIA MAFATAKI YALIYOBEBESHA MIMBA WANAFUNZI 16 PWANI

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 

MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo amewaagiza wakuu wa wilaya kuhakikisha wanawapa msukosuko na kuwakamata wanaohusika kuwapa mimba wanafunzi 16 na kusababisha kushindwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi  ,pasipo kuwaachia wakiendelea kutamba kitaani. 


Aidha amewataka wazazi na walezi kuacha kumalizana kesi za mimba za utotoni majumbani na kurubuniwa fedha ili kuwaachia huru wanaobainika kuwapa mimba watoto wao wakike. 


Akizungumzia changamoto zinazodaiwa kusababisha kushuka kwa ufaulu, Ndikilo alitoa maelekezo hakuna kufanya masihala kwa wanaohusika kufanya vitendo hivyo,na wanatakiwa wakamatwe na kufungwa miaka 30 jela.


Alisema wanafunzi 223 ambao ni sawa na asilimia 0.74 hawakufanya mtihani wa kumaliza darasa la saba, kutokana na utoro 149,mimba 16 ,ugonjwa 15,vifo tisa na sababu nyingine 34.
Alitaja tatizo jingine kuwa ni utoro,mdondoko suala ambalo linachangia kushusha taaluma. 


“Tunakazi ya ziada kukabiliana na mdondoko mashuleni, tunalea watoto kuacha shule, wilayani Mkuranga mdondoko ulikuwa 67,Kibiti 36,Chalinze 36,”


“Kisarawe wanne, Bagamoyo 12,Mafia wanne, Kibaha Mjini tisa na Kibaha Vijijini wanne “alifafanua Ndikilo. 


Awali katibu tawala mkoani hapo, Theresia Mbando alieleza, idadi ya wahitimu waliosajiliwa kufanya mtihani ,walikuwa 30,010 kati yao wavulana 14,304 na wasichana  15,706 ambapo waliofanya mtihani huo ni watahiniwa 29,787 wakiwemo wavulana 14,182 na wasichana 15,605 sawa na asilimia 99.26.


Nae ofisa elimu mkoa Abdul Maulid alisema, halmashauri ya Chalinze waliopata mimba ni Tisa, Mkuranga wanne ,Bagamoyo mmoja, Kisarawe mmoja na Rufiji mmoja. 


Hata hivyo,kunaonyesha kupanda kwa ufaulu kimkoa kutoka asilimia 66.9 mwaka jana hadi asilimia 77.79 mwaka huu. 

No comments:

Post a Comment