Saturday, December 15, 2018

NAIBU WAZIRI WA NISHATI SUBIRA MGALU AHAHIDI KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA NISHATI YA UMEME KTK VITUO VYA AFYA NCHINI

Naibu Waziri wa nishati Subira Mgalu kulia akiangalia mwenendo wa upanuzi wa ujenzi wa kituo cha afya mkoani kushoto kwake ni Mganga mkuu wa halmasshauri ya mji Kibaha. (PICHA NA VICTOR MASANGU).
........................................

VICTOR  MASANGU, KIBAHA   

NAIBU waziri wa nishati Subira Mgalu katika kuumga mkono Juhudi za Rais Dk . John Pombe Magufuli ya kuboresha sekta ya afya hapa nchini  ameliagiza Shirika la umeme Tanzania (TANESCO)   kuhakikisha wanapeleka miundombinu ya nishati ya umeme haraka iwezekanavyo  katika maeneo ya  vituo vipya vya afya 300 pamoja na  hospitali 69 ambazo zinajengwa  na serikali kwa lengo la kuboresha huduma ya  matibabu kwa wananchi wake.

Mgalu  ambaye pia ni Mbunge wa viti maalumu kupitia  Mkoa wa Pwani alitoa  kauli hiyo  wakati wa ziara yake ya kikazi kwa ajili ya  kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo iliyopo katika halmashauri ya mji Kibaha pamoja na kukagua mwenendo wa ujenzi wa upanuzi  katika  kituo cha afya mkoani kilichopo Wilayani Kibaha.

“Kwa kweli nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inafikisha kwa haraka miundombinu ya umeme katika vituo vipya vya afya ambavyo vinajengwa pamoja na hospitali hivyo nachukua nafasi hii kuwaagiza Tanesco pamoja na REA kufikisha umeme haraka iwezekanavyo katika maeneo hayo ili wananchi waweze kupata huduma ya afya katika mazingira ambayo ni rafiki kwao na katika hili tunamshukuru sana Rais wetu Dk. John Pombe Magufuli,”alisema Mgalu.

 Aidha alibainisha  kwamba kwa sasa lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inaboresha miundombinu ya umeme katika maeneo mbali mbali ili zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali ziweze kupata nishati ya umeme wa uhakika ambao utasaidia kuboresha zaidi katika utoaji wa huduma ya afya kwa wananchi wa Tanzania ambao hapo awali walikuwa wanateseka.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa halmashauri ya mji Kibaha Tulitweni Mwinuka alisema  kwamba wamepokea kiasi cha shilingi milioni 500 kutoka serikali kuu kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho  cha afya mkoani katika maeneo ya  wodi ya wazazi,jengo la mionzi  jengo maalumu kwa ajili ya kufulia pamoja na jengo la upasuaji ambapo kukamilika kwake kutaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya  mlundikano kwa wagonjwa.

Nao baadhi ya wanawake Wilayani Kibaha  Elina Mngonja na Selina Wilsoni  wamemshukuru Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli kwa kuboresha sekta ya afya hapa nchni ambapo  wamesema kukamilika kwa upanuzi wa kituo hicho hasa katika wodi za kinamama wajawazito  utakuwa ni mkombozi mkubwa katika suala zima la utoaji wa huduma hasa  wakati wanapokwenda  kujifungua.
 
Naibu waziri wa Nishati Subira Mgalu kulia akipokea taarifa ya ujenzi wa upanuzi wa kituo cha afya mkoano kutoka kwa Mganga mkuu wa halmashauri ya mjini Kibaha Tulitweni Mwinuka. (PICHA NA VICTOR MASANGU)
Mganga mkuu wa halmashauri ya mji Kibaha Tulitweni Mwinuka kushoto akimwonyesha ujenzi unavyoendelea  wa mradi wa upanuzi wa kituo cha afya cha Mkoani kilichopo Wilayani Kibaha, Naibu waziri wa nishati Subira Mgalu kulia kwake ambaye alifanya ziara kwa ajili ya kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo. (PICHA NA VICTOR MASANGU)

No comments:

Post a Comment