Sunday, December 9, 2018

WAZIRI KALEMANI AZITAKA TAASISI ZINAZOJENGA DODOMA KULIPIA UMEME ILI KUHARAKISHA UJENZI.

Taasisi zinazojenga majengo katika mji wa Serikali Dodoma zatakiwa kulipia gharama ya umeme mapema.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameziagiza Wizara na Taasisi zilizoanza ujenzi na zilizo katika maandalizi ya ujenzi wa majengo katika Mji wa Serikali jijini Dodoma kuhakikisha kuwa, wanalipia gharama ya kupeleka umeme katika maeneo yao ili kuharakisha shughuli za ujenzi.

Dkt Kalemani ameyasema hayo wakati alipokuwa akikagua maandalizi ya ujenzi wa Jengo la Wizara ya Nishati katika Mji wa Serikali, Ihumwa jijini Dodoma ambapo aliambatana na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Raphael Nombo na Kamati ya Wizara inayosimamia ujenzi huo.

Dkt Kalemani amesema kuwa tayari miundombinu ya umeme imeshafika katika eneo hilo kwani Tanesco wameshafunga transfoma inayosambaza umeme katika eneo husika.

Ameeleza kuwa endapo Taasisi hizo zitalipia gharama hizo mapema zitaweza kufanya shughuli za ujenzi, usiku na mchana na hivyo kukamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa.

Aidha ametoa agizo kwa Meneja wa TANESCO mkoa wa Dodoma kuhakikisha kuwa, anafahamu mahitaji ya umeme ya eneo hilo la Serikali ili nishati ya umeme isiwe kikwazo cha utekelezaji wa kazi za ujenzi katika eneo hilo.

Kuhusu maandalizi ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati, ameridhishwa na hatua ya maandalizi na kumuelekeza mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
kuwa, kazi hiyo inakamilika kabla ya mwezi Januari, mwakani.

Aidha amemuagiza kuwa azingatie ubora na kuhakikisha kuwa anakuwa na vibarua wa kutosha kukamilisha hiyo ndani ya wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendelezaji Milki kutoka NHC, Haikamen Mlekio amesema kuwa watatekeleza maagizo ya Waziri kwa kumaliza ujenzi wa jengo hilo ndani ya wakati kwa kuwa wanauzoefu katika kazi hiyo.

Ameeleza kuwa tayari wana vibarua wa kutosha wa kuwawezesha kufanya kazi kwa haraka na ubora unaotakiwa.

No comments:

Post a Comment