Na.Immaculate Makilika – MAELEZO
Jeshi la Polisi nchini limetakiwa kuwa na
mwelekeo mpya wa kujenga uchumi wa kisasa, kwa kushiriki katika shughuli
za ujenzi wa viwanda sambamba na sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa
viwanda na kufikia nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam, wakati
alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwatunuku vyeo wahitimu 513
waliofaulu zaidi mafunzo ya Uofisa na Ukaguzi, katika Chuo cha
Taaluma ya Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es salaam, Rais Magufuli
alisema kuwa imefika wakati Jeshi la Polisi kuwa na mwelekeo mpya wa
uchumi wa kisasa ili kusaidia majeshi hayo kuwa na uwezo wa kujiendesha vizuri
bila kutegemea sana Serikali.
“Mtafute mwelekeo mpya wa majeshi yetu, unaolenga
kujenga uchumi wa kisasa, mjipange kushiriki shughuli za uchumi hasa ujenzi wa
viwanda, pamoja na kupanua wigo wa kutengeneza sare zenu, na bidhaa mbalimbali
za viatu au maji hali itakaosadia kuwa na bidhaa za ziada badala ya
kununua na kuweza kujiendesha” alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli alitolea mfano baadhi ya majeshi
kushiriki katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara
,ambapo alisema Jeshi la nchi ya China limejenga mji mkubwa
nchini humo.
Aidha, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Magereza
kushirikiana na majeshi mengine nchini likiwemo Jeshi la Polisi kwa kutengeneza
bidhaa mbalimbali pamoja na kusaidiana masuala kadhaa.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli ameahidi kukipatia
Chuo cha Taaluma ya Polisi nchini kiasi cha shilingi milioni 700 kabla ya
ijumaa wiki ijayo kwa ajili ya kukarabati chuo hicho kwa kujenga mabweni na
madarasa ya kisasa kwa lengo la kuboresha hali ya chuo na kuongeza ufanisi kwa
wahitimu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,
IGP Simon Sirro, alisema ujenzi wa makazi ya Polisi unaendelea kwa
kutumia fedha walizopewa na Serikali kiasi cha shilingi bilioni 3.7, na
wanatarajia kukarabati nyumba 400 za Polisi mara baada ya kupewa kiasi
cha fedha kilichobaki ikiwa ni ahadi ya Rais Magufuli, aliyoitoa mapema
mwaka huu ya kuwapa Jeshi hilo shilingi bilioni 10 ambazo ameahidi kuwapa
ndani ya kipindi cha wiki moja.
Vilevile, IGP Sirro, alisema kuwa nchi iko salama
kwani hali ya uhalifu imepungua kwa kuwa Jeshi la Polisi limeendelea
kufanyakazi kwa kuzingatia nidhamu na weledi
“Hali ya uhalifu imepungua nchi nzima,makosa ya
barabarani yamepungua kwa asilimia 32.6, ajali zimepungua kwa asilimia 30.8,
kwa ujumla kumekuwepo na upungufu wa matukio ya uhalifu kwa sababu Jeshi la
Polisi linashirikiana na wananchi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia
na mali zao”alisema IGP Sirro
Naye, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi, Naibu
Kamishna wa Polisi, Anthony Rutashugurugukwa, alisema kuwa mafunzo hayo
yanayotolewa kwa lengo la kupanda daraja na vyeo yalidumu kwa muda wa
miezi sita, ambapo wanafunzi 513 walihitimu masomo hayo yaliyogawanyika katika
sehemu mbili za mafunzo ya Ukaguzi na Uofisa.
Wahitimu wa mafunzo ya
Uofisa walikuwa 120 ikiwa wanaume 106 na wanawake 14. Aidha, katika mafunzo ya
Ukaguzi kulikuwa na wahitimu wanaume 393 na wahitimu wanawake 60.
Naibu Kamishna huyo wa Polisi alisema kuwa
wahitimu hao wamepata mafunzo mbalimbali yakiwemo stadi za upelelezi, medani za
kivita na masuala mengine mtambuka.
No comments:
Post a Comment