Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.
OFISI ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi) imebaini matumizi mabaya ya fedha za serikali Sh. bilioni 2.98 katika halmashauri ya Ulanga mkoani Morogoro na kuagiza wakuu wa idara wote waliohusika wavuliwe nyadhifa zao huku watumishi wengine waondolewe majukumu ili vyombo vya dola viendelee na hatua kwa mujibu wa sheria dhidi yao.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa nchi ofisi ya Rais
Twala za mikoa na Serikali za mitaa Mhe. Selemani Jafo wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari juu ya uchunguzi maalum uliofanywa kwa
halmashauri ya wilaya hiyo.
Jafo alisema kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi imefanya
uchunguzi maalum katika halmashari 12 nchini ambazo ni Ulanga, Same, Mbulu,
Meru, Itigi, Misungwi, Nyang’hwale, Serengeti, Bahi, mpwapwa, Morogoro Dc na
Kibaha Tc ambapo katika halamasahuri ya Ulanga uchuguzi ulianza Novemba 13 hadi
23 mwaka huu.
Alisema uchunguzi huo ulifanyika kufuatia
malalamiko ya wanachi mbalimbali pamoja na mbunge wa jimbo la Ulanga Mhe.
Goodluck Mlinga kutokana na ubadhirifu uliokuwepo.
Aidha alisema kiasi hicho kimebainika kupotea
kutokana na matumizi mabaya ya fedha za serikali ambapo watumishi wasio
waadilifu katika halmashauri hiyo walikiuka taratibu na kufanya manunuzi hewa
na kutumia vibaya fedha kinyume na malengo yaliyopangwa.
“Halmashauri hii imekuwa ikifanya udanganyifu
katika taarifa za miradi ya maendeleo taarifa za mfuko wa wanawake na vijana,
kwa ujumla inausimamizi mbovu wa mapato na kuwa na udhibiti hafifu wa makusanyo
na matumizi ya fedha za Umma”alisema Jafo.
Jafo alisema kuwa mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri ya Ulanga, Yusufu Daud Semguruka kwa nafasi yake ya afisa masuhuli
alishindwa kusiomamia sheria ya fedha za serikali za mitaa katika kudhibiti na
kuweka mifumo dhabiti ya kuhakikisha fedha ziko salama kuanzia makusanyo hadi
matumizi yake.
“Hii ni pamoja na kushindwa kumsimamia mweka
hazina wa halmashauri katika kutekeleza majukumu yake na kwa kushindwa
kutekeleza majuku hayo amesababisha hasara halmashauri ya shilingi
2,980,172,763.60″alisema Jafo.
Alifafanua kuwa Rajabu Siriwa,ambaye alikuwa ni
mweka hazina wa halmasahuri hiyo alichangia kuhujumu mapato ya serikali kwa
kuweka utaratibu ambao umeisababishia hasara serikali.
Alisema kuwa mweka hazina huyo aliidhinisha malipo
ya sh. 225,586,400 nje ya bajeti bila idhini ya ofisi ya Rais Tamisemi ambapo
malipo hayo yalihusisha posho ya safari ya mkurugenzi mtendaji Sh. 192,000,000.
“Pia kukusanya mapato na kutoyapeleka benki,
katika mfumo wa LGRCIS umeonyesha halmashauri ilikusanya fedha ambazo
hazikupelekwa benki kabisa shilingi 760,686,732.43 fedha hizi hazijulikani
matumizi yake halisi ni nini”alihoji Jafo.
Aidha alisema kuwa mweka hazina huyo aliandaa
taarifa zenye udanganyifu kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotumia
fedha za makusanyo ya ndani.
“Halmashauri imeripoti kupeleka shilingi
301,442,686 uhalisia wamepeleka 113,406,106.34 na udanganyifu katika mfuko wa
vijana na akina mama halmashauri inaripoti kupeleka shilingi 120,000,000 uhalisia
wamepeleka sh. 31,500,000 kwa mwaka 2017/18 na 2018/19 hadi novemba 2018 wakati
uchunguzi unakamilika”alisema.
Aidha Jafo alisema kuwa Mhandisi David Kaijage
akiwa anakaimu ofisi ya mkurugenzi februari mosi mwaka huu hadi Februari nane
alihusika kwenye kuihujumu halmashauri kwa mapato ya Sh. 470,000,000
yaliyopolelewa kutoka kiwanda cha kilombero Valley Teak Company kwa kuzirejesha
kwa mlipaji siku hiyohiyo waliyopokea.
“Pia alisaini hati ya malipo kumlipa bahari
Phamarcy kwa siku ambayo hakuwa kaimu mkurugenzi na mkurugenzi
alikuwepo”alisema.
Wakati huo huo Bw. Stanley Godwil Nyange na Bw. Isaack Mwasankope Salumu ambao wote ni wahasibu wameihujumu Halmashauri kwa kutumia akaunti zao binafsi kupokea fedha za makusanyo ya Halmashauri kiasi cha sh 203.398,700 aliongeza.
Waziri Jafo pia alisema kuwa uchunguzi huo pia umebainisha kuwa Isaack Mwasankope, Salehe Mbogoso pamoja na Johson Mwanyombole ambao wote ni wahasibu wa halmashauri hiyo walihusika kuchukua fedha taslim za makusanyo katika kituo cha kivukoni na kisha kuzitumia bila kuzipeleka Benki sh 168,000,000.
Yassin Galahenga na Mohamed Majaliwa Saidi wataalam wa mifumo (TEHAMA) walishirikiana na wahasibu kurekebisha Ankara na kufuta madeni bila idhini ya Mkurugenzi alibainisha Waziri Jafo.
Waziri Jafo aliongeza kuwa Bw. Willy Ndabila ambaye alikua afisa manunuzi alihusika na manunuzi hewa ya madawa yenye thamani y ash.
73,212,909.40 pamoja na kulipa fedha zaidi yaani sh
146,425,818 huku Goodluck Mbata ambaye ni muhasibu wa hospital aliandaa malipo
na kusainisha mara mbili kwa watu tofauti huku akijua kufanya hivyo ni kuandaa
malipo mara mbili kwa hitaji moja (double paymet).
Waziri Jafo aliagiza ofisi ya mkuu wa mkoa wa
Morogoro kuhakikisha kuwa wakuu wa idara na vitengo waliohusika akiwemo Willy
Ndabila ambaye amehamishiwa itilima,na Rajabu Siriwa ambaye amehamishiwa Gairo
wavuliwe nyadhifa zao na mamlaka za nidhamu na vyombo vya dola viendelee na
hatua kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kuwa watumishi wote waliohamishiwa
Halmashauri ya ulanga wakiwa na makosa yaani DPMU Willy Ndabila na DT Rajabu
Siriwa warejee halamashauri ya Ulanga ili kuiwezesha halmashauri na vyombo vya
Dola kufanya kazi yake.
“Maelezo juu ya mkurugenzi huyu wa Ulanga yenyewe yatatolewa baadaye na serikali”alifafanua Jafo.
Hatahivyo Jafo alisema kuwa mkuu wa mkoa wa
Morogoro ahakikishe kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi imepata maelezo kwanini
wataalamu hao hawakuchukuliwa hatua stahiki zenye tija dhidi ya taarifa za
mkaguzi wa ndani ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha2017/18 kabla ya januari 15
mwakani.
No comments:
Post a Comment