Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima (wa pili kutoka kushoto)
akimsikiliza Mratibu wa Kanda kutoka Baraza la Taifa Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira Bw. Godlove Mwamsojo mara baada ya kutembelea
dampo lililopo katika Kata ya Saja, Kijiji cha Itengelo Wilaya ya
Wanging’ombe. Naibu Waziri Sima ameagiza kufungwa kwa dampo hilo na
kuteketeza taka zote zilizopo.
…………………..
Na Lulu Mussa,Njombe
Halmashauri ya Mji wa Makambako
Wilayani Njombe imeagizwa kusitisha mara moja utupaji wa taka ngumu
katika dampo lililopo katika Kata ya Saja, Kijiji cha Itengelo Wilaya ya
Wanging’ombe kutokana na kutokidhi matakwa ya Sheria ya Mazingira na
malalamiko yaliyotolewa na wananchi katika vijiji vya jirani.
Agizo hilo limetolewa hii leo
Mkoani Njombe na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mhe. Mussa Sima mara baada ya kufanya ziara ya kikazi na
kumuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Makambako Bw. Rashid Hozi kutafuta
eneo maalumu litakalokidhi mahitaji husika ikiwa ni pamoja na kufanya
tathmini ya athari kwa mazingira
Akiwa katika eneo hilo la dampo la
Makambako ambalo kwa hivi sasa liko katika Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe
Sima ameshuhudia wananchi wakiingia kiholela katika dampo hilo kwa ajili
ya kuokota bidhaa mfano chupa za plastiki kwa ajili ya kuziuza.
“Serikali inatumia pesa nyingi
katika huduma za afya ni wakati sasa tupunguze mzigo huu kwa magonjwa
yanayoweza kuepukika kwa kuwa na mazingira safi na salama. Kuanzia sasa
ni marufuku wananchi kuingia dampo kuokota chupa za plastiki, hii
inahatarisha afya zao wenyewe, hivyo utaratibu wa kutenganisha taka
uanzie katika vyanzo vya uzalishaji” Sima alisisitiza.
Awali Mratibu wa Kanda wa Baraza
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Nyanda za
Juu Kusini Bw. Godlove Mwamsojo amesema kuwa Baraza limetoa notisi ya
siku sitini (60) kuanzia tarehe 01/02/2019 kwa Halmashauri hiyo ya
kusitisha utupaji wa taka katika eneo hilo na kuwaagiza kuteketeza taka
zote zilizopo katika kipindi kilichotajwa.
Bw. Mwamsojo amesema kuwa Sheria
ya Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 119 kinazitaka Mamlaka za
Serikali za Mitaa kutafuta namna bora ya kuteketeza taka ngumu katika
maeneo yao na kuainisha kuwa dampo hilo kwa sasa liko katika eneo la
mwinuko hivyo kipindi cha mvua hutiririsha maji ambayo si salama kwa
wakazi wa maeneo ya chini.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Sima
pia amemuagiza Mratibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) kuhakikisha anafuatilia utekelezaji wa agizo hilo na
endapo Halmashauri haitatekeleza agizo hilo hatua kali za kisheria
zichukuliwe dhidi yao .
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
wa Mji wa Makambako Bw. Rashid Hozi amekiri kupokea barua ya Baraza la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na kuahidi kutekeleza maagizo
yaliyotolewa kwa muda muafaka.
Naibu Waziri Mussa Sima, yuko
katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini kuainisha
changamoto za kimazingira katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na
kukagua mitambo ya kuteketeza taka hatarishi katika Hospitali, kujionea
hali ya madampo katika mikoa husika endapo utaratibu wa kutenganisha
taka unazingatiwa ili kuzuia wananchi kuzifuata baadhi ya bidhaa zinazo
rejerezeka katika maeneo ya dampo kwa lengo la kudhibiti milipuko ya
magonjwa.
Katika Mikoa ya Njombe, Mbeya na
Iringa Mheshimiwa Sima pia atapata fursa ya kuembelea kwenye ikolojia ya
vyanzo vya maji vinavyo changia maji katika bonde la Rufiji.
No comments:
Post a Comment