Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa
Bw.Alex Nkenyenge (Kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo Machi 30, 2019
Jijini Dodoma kuhusu kutekeleza maagizo ya Serikali kwa Baraza hilo
kusimamia Uchaguzi ndani ya Klabu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) ndani
ya siku 30 kuanzia leo.Kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo wa
Wizara ya Habari utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Yusuph Singo.
.....................................
Na Shamimu nyaki –WHUSM
Serikali imeliagiza Baraza la Michezo
la Taifa (BMT) kushirikiana na Shirikisho la mpira wa Miguu (TFF) kuhakikisha
uchaguzi ndani ya Klabu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) unafanyika
ndani ya siku 30 kuanzia leo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Idara ya
Maendeleo ya Michezo Bw.Yusuph Singo katika mkutano na Waandishi wa Habari leo
Jijini Dodoma ambapo amesema kuwa migogoro iliyokuwepo huko nyuma imeshafika
tamati hivyo uchaguzi ndani ya Klabu hiyo ni lazima ufanyike.
“Nailekeza BMT iwaelekeze TFF
kuhakikisha taratibu zote za uchaguzi zinafuatwa na uchaguzi ndani ya Klabu ya
Dar es Salaam Young Africans unafayika ndani ya siku 30 kuanzia sasa”.amesema
Bw.Singo.
Aidha Bw.Singo amewahisi Viongozi,
wanachama na wapenzi wa Klabu ya Dar es Salaam Young Africans kutoanzisha
migogoro wala vikwazo vingine bali kutumia siku 30 hizo kufanya uchaguzi ili
kupata viongozi watakaoisimamia na kuiongoza Klabu hiyo kuendelea kufanya
vizuri katika mpira wa miguu ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw.Alex Nkenyenge amesema amepokea maagizo na
atayafanyia kazi mara moja ili kipindi kilichowekwa na Serikali cha siku 30
Klabu ya Yanga iwe tayari ina uongozi.
Bw.Nkenyenge ameongeza kuwa
atahakikisha Kamati ya Uchaguzi ya TFF inapanga utaratibu unaotakiwa kufuatwa
kulingana na Katiba ya Shirikisho hilo ili Uchaguzi huo ufanyike hatimaye
migogoro iliyodumu kwa muda mrefu ndani ya Klabu hiyo ifikie mwisho na Klabu
iendelee kufanya vizuri katika mpira wa miguu.
Klabu ya Dar es Salaam Young Africans
(Yanga) ni miongoni mwa Klabu kubwa za mpira wa miguu hapa nchini ambayo kwa
muda mrefu haijatekekeleza uchaguzi kwa mujibu wa Katiba yao.
No comments:
Post a Comment