Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango (Mb), akieleza jitihada za Serikali katika kupambana na utapiamlo
ikiwa ni pamoja na kila mkoa kuandaa bajeti ya lishe wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa
masuala ya Lishe duniani, Sarah Zeid (hayupo pichani), Kushoto ni Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara Dkt. Khatibu Kazungu na kulia ni Kamishna Msaidizi wa Bajeti wa
Wizara hiyo Dkt. Charles Mwamwaja.
......................................
.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Binti wa Mfalme wa Jordan, Sarah
Zeid, ambaye ni Mwanaharakati wa masuala ya lishe, wanawake na watoto
Duniani, jijini Dodoma.
Katika mazungumzo yao, Dkt. Mpango,
alimweleza Princess Sarah Zeid kwamba Tanzania bado inakabiliwa na changamoto
ya masuala ya lishe, utapiamlo na udumavu wa watoto licha ya nchi kuwa na
chakula cha kutosha.
Dkt. Mpango alisema kuwa iwapo eneo
la lishe halitasimamiwa kikamilifu Taifa litazalisha watoto wenye udumavu wa
ubongo na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kufikiri na utendaji hafifu wakiwa
katika shughuli mbalimbali.
Alisema ipo mikoa ambayo inazalisha
mazao mengi kama Mbeya na Njombe lakini ina kiwango kikubwa cha watoto
wenye utapiamlo, na kutoa wito kwa kila mtanzania kuhakikisha anaangalia ni
chakula gani kinahitajika kwa ajili ya lishe ya watoto na wakinamama wajawazito
ili kupunguza udumavu na vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.
Aidha amempongeza Mwana wa Mfalme wa
Jordan, Sarah Zeid, kwa kampeni yake anayoifanya duniani kote kupambana na vifo
vya wakinamama wajawazito na watoto kwa kuwa mchango wa wanawake ni mkubwa
katika jamii ikiwemo uzalishaji mali.
Alisema idadi ya wanawake nchini
Tanzania ni asilimia 51 ya idadi ya watu wote wanaokadiriwa kufikia milioni 55 ambapo
mchango wako katika sekta mbalimbali za uchumi umekuwa mkubwa hivyo jitihada za
kuwalinda zinahitajika.
Alimweleza Binti Mfalme wa Jordan,
Sarah Zeid kwamba kwa kutambua umuhimu wa lishe serikali imelivalia njuga suala
la lishe kwa kutenga bajeti kila mwaka katika kila wizara na kwamba fedha hizo
zimewekewa wigo zisitumike kwa matumizi mengine.
“Nimeziagiza Wizara, Mikoa na
Halmashauri zote nchini kutumia fungu lililotengwa kwa ajili ya lishe kwa
matumizi yaliyopangwa ili kuhakikisha watanzania wanaimarika kiafya na
kushiriki kikamilifu katika Shughuli za Maendeleo” Alisema Dkt. Mpango.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa
Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa Mkutano kati yake na Mwana
wa Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Dunia, Sarah Zeid
Kwa upande wake Mwana wa Mfalme wa
Jordan, Sarah Zeid, ambaye aliambatana na Mwakilishi wa Shirika la
Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) nchini Tanzania, Bw. Michael Dunford,
ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake katika kupambana na
utapiamlo unaosababishwa na ukosefu wa lishe.
Amewataka watanzania kuhakikisha
suala la Lishe linapewa kipaumbele na kila mmoja kwa manufaa ya Taifa na
Dunia kwa ujumla na kwamba atahamasisha jumuiya ya kimataifa kuchangia jitihada
za Serikali za kupambana na tatizo la lishe, na vifo vya wanawake wajawazito na
watoto.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula
la Umoja wa Mataifa-WFP nchini Tanzania Bw. Michael Dunford, amesema kuwa
shirika lake linatambua mchango mkubwa wa Serikali katika kupambana na masuala
ya lishe duni na shirika lake litaendelea kushirikiana na nayo ili kufikia
malengo yanayotarajiwa.
Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya lishe duniani, Sarah Zeid, akieleza anavyofurahishwa na Serikali ya Tanzania inavyosimamia suala la lishe, wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani- WFP nchini Tanzania, Bw. Michael Dunford.
Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya lishe duniani, Sarah Zeid, akieleza anavyofurahishwa na Serikali ya Tanzania inavyosimamia suala la lishe, wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani- WFP nchini Tanzania, Bw. Michael Dunford.
Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja
wa Mataifa (WFP) Bw. Michael Dunford, akieleza utayari wa Shirika hilo
kuisaidia Tanzania katika masuala ya lishe, wakati wa Mkutano kati ya Binti
Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid (kushoto) na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Jijini Dodoma.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia), na Ujumbe
wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), ukiongozwa na Binti
Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya lishe duniani, Sarah Zeid (wa
pili kulia) katika mkutano kuhusu lishe, uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya
Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango (Mb) akipeana mkono na Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa
masuala ya Lishe Duniani, Sarah Zeid (kushoto), baada ya kumalizika mkutano
kuhusu Lishe uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini
Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb) na Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala
ya lishe Duniani, Sarah Zeid (kushoto), wakifurahia jambo katika picha ya
pamoja na wajumbe kutoka Tanzania na Shirika la Chakula Duniani- WFP, baada ya
kumalizika kwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili katika ukumbi wa Wizara ya
Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
(Picha na Peter Haule, Wizara ya
Fedha na Mipango)
No comments:
Post a Comment