Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano
na Mazingira Mhe. January Makamba (katikati) akiongea na Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge wa Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Suleiman Murad Sadick
katika moja ya ziara za kikazi za Kamati hiyo hivi karibuni.
....................................
Na Lulu Mussa,Dodoma
Serikali imesema itaendelea na juhudi
za kushawishi wadau wa maendeleo na Jumuiya za Kimataifa ili kupata fedha za
kusimamia uratibu wa shughuli za mazingira na kukabiliana na Athari za
Mabadiliko ya Tabianchi nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba ameyasema hayo hii leo Jijini
Dodoma wakati wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti
kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka
2019/2020 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Amesema Tanzania ni Mwanachama kwenye Mifuko na Mikataba mbalimbali duniani
hivyo kuna fursa za kunufaika na fedha zitolewazo na mifuko hiyo akitoa mfano
wa Green Climate Fund.
Aidha Waziri Makamba ameainisha
mafanikio yaliyopatikana katika Ofisi yake kwa kipindi cha mwaka 2018/2019,
kuwa ni pamoja na kufanya Mapitio ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997
na Mkakati wa Utekelezaji wake, kuandaa rasimu ya Mpango wa Taifa wa
Mazingira wa mwaka 2019 – 2023, na Maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti
Viumbe Vamizi (Invasive Alien Species).
Pia, katika kipindi cha mwaka
2018/19, Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha rasimu ya mwisho ya Ripoti ya
Tatu ya Hali ya Mazingira Nchini baada ya kupata maoni ya wadau kabla ya
kuwasilishwa Bungeni kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira
ya Mwaka 2004.
Waziri Makamba amesema katika
kuhakikisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira unazingatiwa jumla
ya miradi 1,254 ya maendeleo imefanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM)
na Ukaguzi wa Mazingira na katika kuharakisha uwekezaji katika sekta ya viwanda
nchini, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira linatoa Kibali cha
Awali cha Mazingira (Provisional Environmental Clearance) ili kuwawezesha
wawekezaji kuendelea na maandalizi ya awali ya mradi wakati mchakato wa
Tathmini ya Athari kwa Mazingira unaendelea.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Suleiman Sadick
amepongeza uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa jitihada za kuhifadhi
mazingira nchini. ” Kamati inatambua jitihada za Ofisi yenu katika kuhifadhi
mazingira, sisi tunawaunga mkono” alisisitiza Mhe. Sadick.
No comments:
Post a Comment