Tuesday, March 5, 2019

RC MTAKA ATOA WITO KWA WANAWAKE KUHIMIZA JAMII KUSOMESHA WATOTO ILI KUONDOKANA NA MILA POTOFU


 Mkuu wa  Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiimba pamoja na Kwaya ya Upendo kutoka Kanisa la Anglikana Musoma katika Siku ya maombi ya Dunia yaliyofanyika Machi Mosi, 2019 katika Viwanja vya Parokia ya Yohana Mbatizaji Nyamiongo Musoma kwa kujumuisha wanawake wa madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake WaKatoliki Tanzania(WAWATA)  . 
 Mkuu wa  Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) na Askofu Jimbo Katoliki la Musoma Mhashamu Michael Msongazila wakifurahia jambo katika Siku ya maombi ya Dunia yaliyofanyika katika Viwanja vya Parokia ya Yohana Mbatizaji Nyamiongo Musoma kwa kujumuisha wanawake wa madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake WaKatoliki Tanzania(WAWATA)  , Machi Mosi, 2019.
Mkuu wa  Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka( wa pili kushoto), viongozi wa Kanisa na baadhi ya viongozi wa wanawake wakiwa  ibada ya siku ya maombi ya Dunia yaliyofanyika Machi Mosi, 2019 katika Viwanja vya Parokia ya Yohana Mbatizaji Nyamiongo Musoma na  kujumuisha wanawake wa madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA) 
Na Stella Kalinga, Mara
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wanawake, kuwa mstari wa mbele kuhimiza jamii juu ya umuhimu wa kuwasomesha watoto, ili kuondokana mila potofu  zilizopitwa na wakati, ukiwemo ubaguzi wa kijinsia na mfumo dume.
Mtaka ametoa wito huo, wakati wa siku ya maombi ya Dunia yaliyofanyika Nyamiongo  Manispaa ya Musoma Mkoani Mara ambako alikuwa mgeni rasmi, ambayo yaliwahusisha wanawake kutoka katika madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA).
Amesema suluhisho la mila potofu zilizopitwa na wakati kama mfumo dume, ubaguzi wa kijinsia na kuona watoto wa kiume ni bora kuliko wa kike ni kuwasomesha watoto wote pasipo kujali kuwa ni wa kike au wa kiume.
“Ukisomesha watoto wako vizuri wakafanikiwa kwenye hiyo nyumba hakuna atakayesema yeye ni bora zaidi ya mwenziye, hakuna atakayesema mimi ndiye mwanaume kwenye hii nyumba na huyu ni  mwanamke, somesheni watoto hayo mambo yote yaliyopitwa na wakati yataisha” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amewaomba wanawake na waumini wote wa ujumla kuendelea kuliombea Taifa, Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wengine, ili nchi iendelee kuwa na amani na viongozi waweze kufanya mazuri yaliyokusudiwa kwa ajili ya Watanzania wote.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini pamoja na kusimamia kiroho wawe msaada kwa makundi mbalimbali yaliyomo makanisani hususani vijana na wanawake, ili yaweze kuendesha miradi ya maendeleo itakayowasaidia kubadilisha maisha yao kiuchumi.
Baadhi ya wanawake walioshiriki katika Maombi ya dunia baada ya kusikia hotuba ya Mkuu  wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ambaye alikuwa mgeni rasmi wamesema watahakikisha wanasimamia vema malezi ya watoto wao na kuhakikisha wanasoma huku wakiunga mkono wazo la vikundi kuwa na miradi ya maendeleo.
“ Kama mama nimejifunza mengi; moja ni kuwa tukiwasomesha watoto wetu hakutakuwa na unyanyasaji, mfano kama kuna watu wanafanya ukeketaji kwa watoto wa kike, jamii ikielimika haya hayatakuwepo na tutahakikisha wanasoma mpaka vyuo vikuu; ujasiriamali nao tutafanya ili tujikwamue kwenye umaskini” Devotha Charles mshiriki kutoka Mwisenge
“Baadhi ya wanawake katika makanisa yetu tulikuwa hatua miradi na wengine waliokuwa nayo  ilikuwa  inaenda kwa kusuasua, lakini baada ya ujumbe tulioupokea leo nina hakika utaleta mwamko kwa wanawake wengi kuanzisha miradi ya kuwasaidia kupata kipato” Jackline Cheche mshiriki kutoka Parokia ya Nyamiongo Musoma.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Mhashamu Michael Msongazila amesema maombezi kwa ulimwengu yaendelee kufanyika ili watu waweze kuheshimu uhai wa mwanadamu.
“Ombeeni ulimwengu uheshimu uhai wa mwanadamu tumeumbwa katika sura na mfano wa Mungu, tumekabidhiwa dhamana hiyo ya uumbaji, uhai huu tuulinde tuutetee na tuukuze kwa ajili ya kujenga ulimwengu, maisha yetu yana nafasi ya pekee yanapokuwa na Mungu” alisema Askofu Mlonganzila.
Maombi ya Dunia kwa wanawake wa madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA) hufanyika kila mwaka Machi Mosi yakiwa na lengo la kuombea familia, Taifa na Dunia kwa ujumla juu ya amani na mahitaji mengine.
MWISHO

No comments:

Post a Comment