Saturday, March 30, 2019

MRADI WA MAJI MLANDIZI -MBOGA KUANZA MWEZI WA NNE


Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo, Ridhiwani Kikwete, akielezea kwa umakini ramani ya mradi wa Mlandizi Mboga unaotarajiwa kuanza kujengwa mwezi April ,mwaka huu utakaohudumia wakazi wa jimbo hilo akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA Mhandisi Arone Joseph  na Mkurugenzi wa Miradi DAWASA Mhandisi Lydia Ndibalema. (picha na Mwamvua

Mbunge wa Chalinze ,Ridhiwani Kikwete akikagua eneo lilalotengenezwa mabomba ya kusambazia maji yatakayotumika kwenye mradi wa maji Mlandizi -Mboga Chalinze.
........................................


NA MWAMVUA MWINYI

MBUNGE wa Chalinze ,Ridhiwani Kikwete ameeleza, imechukua miaka 16 kwa wananchi wa Chalinze kupata majisafi na salama na imani yake kubwa ipo kwa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA wafanikishe mradi huo.


Aliyasema hayo, wakati alipotembelea,  kiwanda cha mabomba cha Tanzania Steel Pipes kinachotengeneza mabomba ya kusafirishia maji kwenye mradi wa maji wa Mlandizi- Chalinze- Mboga.


Ridhiwani amefurahishwa na maendeleo ya utengenezaji wa mabomba hayo ambapo takribani mabomba 321 yameanza kusafirishwa kwa ajili ujenzi wa meadi huo unaotarajiwa kuanza katikati ya mwezi April.


“Sikuwahi kuona namna wananchi wanatumia maji pamoja na wanyama kama ng’ombe ila kukamilika kwa mradi huu kutawezesha watu kupata majisafi na salama”


Alisema mradi huo utawanufaisha wakazi wa maeneo hayo ikiwa pamoja na wananchi wanaoishi kwenye eneo la mradi.


Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA Mhandisi ,Arone Joseph Nae Joseph alisema ,mradi wa maji wa Mlandizi -Mboga unatarajiwa kusafirisha maji lita milioni 9.3  (mita za ujazo 9300) kwa siku kiasi kianchokisiwa kuweza kutosheleza mahitaji ya walengwa kwa sasa na ongezeko la matumizi kwa siku za usoni.


“Hadi sasa, kiasi cha mabomba ya umbali wa km 3.7 yameshazalishwa katika kiwanda cha TSP na yameanza kupelekwa kwenye maeneo ya mradi ambapo ujenzi unatarajiwa kuanza katika Vijiji vya Mboga na Msoga,” alisema Joseph.


“Katika usanifu wa mradi huo, umetilia maanani ongezeko la watu na mahitaji ya miaka 20 ijayo na kutosheleza idadi ya watu hadi kufikia 120,912 ndani ya eneo la mradi na utakuwa kwa umbali wa Kilomita 58 ujenzi wa vituo viwili vya kusukumia maji na utagharimu bilion 14 hadi kukamilika kwake,”anasema Joseph.


Maeneo yatakayohudumiwa na mradi huo ni pamoja na Ruvu darajani, Vigwaza,Ranchi ya Taifa Ruvu (NARCO), Chahua -Lukenge, Visenzi, Buyuni na Mdaula -Unebazomozi.


Kwingine ni Chamakweza, Pingi, Pera, Chalinze, Chalinze Mzee, Msoga na Mboga aidha, viwanda vitakavyofaidika ni pamoja na Twyford, kiwanda cha ngozi, kiwanda cha Matunda cha Sayona pamoja na watumiaji wengine wakubwa ikiwemo kampuni Yapi Merkezi wajenzi reli ya kisasa (SGR)

No comments:

Post a Comment