Sunday, March 24, 2019

RAIS WA MSUMBIJI AISHUKURU TANZANIA KWA MISAADA YA DAWA NA CHAKULA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi na Wananchi wake  wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Wananchi wa Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kutoa misaada ya Madawa, Magodoro na vyakula kwa watu wa Msumbiji walioathirika na kimbunga.

Kimbunga kilichopita katikati ya Jamhuri ya Msumbiji  kilicho anza tarehe 14 Machi 2019,  kimesababisha madhara makubwa katika mji wa Beira ambao ni wa tatu kwa ukubwa na wa pili kibiashara baada ya Maputo.

Upepo uliambatana na mvua uling’oa miti, mapaa ya nyumba za mabati na vigae na kuvunja madirisha ya vioo bila huruma katika mji huo.

Kufuatia janga hilo ambalo limezikumba pia nchi za Malawi na Zimbabwe, Rais Magufuli alitangaza kutoa msaada wa haraka ambapo ndege kubwa za JWTZ zilipeleka misaada hiyo kama inavyoonekana katika picha. 

Mjini wa Beira na wilaya  za jirani ziko kwenye uwanda wa tambarale. Mji huo pia una mito miwili mikubwa inayoingia katika bahari ya Hindi na hiyo ndiyo sababu ya mara kwa mara unakabiliwa na mafuriko.

Tanzania inaomba Mungu mvua zipungue kwa majirani hao ili waweze kuidhibiti hali hii ya mafuriko inayoendelea sasa baada ya Kimbunga kupita.

Mji wa Beira umeharibika vibaya ambapo asilimia 97 ya majengo, miundombinu, na mali za wananchi zimeathiriwa na kimbunga hicho.

Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mhe. Rajab Luhwavi ambaye alipokea shukrani hizo kwa niaba ya Serikali ameihakikishia Msumbiji kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hiyo  kwa hali na mali. 

Aidha, Mhe. Balozi ametoa pongezi kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wadau wengine kwa kufanikisha msaada huo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, 
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 

Dodoma, Tarehe 24 Machi 2019

No comments:

Post a Comment