WAZIRI wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewasili mjini Morogoro leo, kwa ajili ya
kuanza ziara yake ya kikazi kwa kutembelea Wilaya zote za Mkoa huo, akisikiliza
kero za wananchi pamoja na kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya
ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake.
Waziri
Lugola anatarajia kuanza ziara hiyo rasmi kesho Machi 7, 2019 mjini Morogoro
kwa kukutana na Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na
kupokea taarifa ya Kamati hiyo, pia atakutana na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya
CCM Mkoa na Wilaya, na baadaye atazungumza na Wakuu wa vyombo vya ulinzi na
usalama vya Wizara yake, na baada ya hapo atafanya kikao na Baraza la Askari na
Watumishi raia wote wa Wizara hiyo waliopo mjini humo.
Akizungumza
na Mwandishi wa habari hii, leo, Lugola amesema atafanya mkutano mkubwa wa
hadhara wa wananchi utakaofanyika mjini humo ili aweze kusikiliza na kuzitatua
kero mbalimbali zitakazosemwa na wananchi katika mkutano huo.
“Nawaomba
wananchi wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Wilaya zake, wahakikishe wanakuja kwa
wingi katika mikutano yangu kuanzia mkoani hapa na Wilaya zote
nitakazozitembelea, ili tuweze kubadilishana mawazo, kusikiliza kero zao
na pia kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya,
wananchi nileteeni kero zenu ili tuzitatue na tuijenge nchi yetu,” alisema
Lugola.
Lugola
aliongeza kuwa, mkutano huo utafanyika saa 10:00 hadi 12:00 jioni utaanza mjini
humo na pia atatoa muda wa wananchi kujitokeza mbele kuja kuuliza maswali na
yeye aweze kuyajibu.
Waziri
Lugola ambaye alisema atafanya mikutano katika Wilaya zote atakazozitembelea
pamoja na kufuatilia maagizo yake mbalimbali ambayo aliyatoa mwaka jana 2018
katika mikutano yake, kama yalifanyiwa kazi na viongozi wa Taasisi
anazoziongoza au yalipuuzwa.
Maagizo
hayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, kupiga
marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na
agizo la pikipiki zote nchini zilizopo vituoni ziondolewe ambazo hazina kesi
mahakamani.
Lugola
alisema katika ziara yake aliyoifanya mwaka jana Mkoani Kigoma, na mwaka huu
Mkoa wa Kagera na Arusha, aligundua wananchi wanakabiliwa na changamoto
mbalimbali hivyo hawezi kukaa ofisini, lazima afanye ziara nchi nzima
kuwasaidia wananchi kutatua kero zao ambapo baadhi yao wakiwalalamikia Polisi
wakiwaonea.
“Wananchi
wanapojitokeza kwa wingi inasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndio
mana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima, hii inasaidia sana kujua
matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa Taasisi
zangu zilizopo ndani ya Wizara hii, na hakika Serikali ya Dokta Magufuli
inawajali wananchi wake ndio mana inawafuata mahali walipo, ili wazungumze na
Serikali yao uso kwa uso,” Alisema Lugola.
Lugola
alisema Taasisi zilizopo ndani ya Wizara yake ambazo ni Jeshi la Polisi, Jeshi
la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na Idara ya Probesheni na Huduma kwa
Jamii, wajipange ili waweze kumpa taarifa za utendaji kazi wao kuanzia ofisi za
Mkoa hadi Wilaya zilizopo mkoani humo.
No comments:
Post a Comment