Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo
alipokuwa akiongea na wananchi wa mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite Sumbawanga
mjini.
.................................
Mkuu wa
Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa
ACP Mathias Nyangi kuhakikisha anafanya msako wa waganga wa kienyeji katika
mkoa na kuwakamata wale wote wanaofanya uganga wa kienyeji bila ya kuwa na
leseni halali za kuwaruhusu kufanya shughuli hizo.
Ametoa
agizo hilo baada ya kusikiliza vilio vya wananchi wakati wa mkutano ulifanyika
mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite, mjini Sumbawanga, wananchi waliokuwa
wakiomboleza vifo vya watoto wawili na mmoja kubaki mahututi katika hospitali
ya rufaa ya mkoa baada ya mganga wa kienyeji kuwateka na kuwaficha katika gari
lake chakavu tangu watoto hao kupotea tarehe 21.3.2019 na wawili kupatikana
wakiwa wamefariki tarehe 23.3.2019 baada ya mmoja aliyepona kutoroka na
kuwajulisha wananchi kilichotokea.
Amesema
kuwa msako huo wa waganga wa kienyeji ufanyike katika wilaya zote tatu za mkoa
ili kuwahakikishia wananchi amani na utulivu ambayo imekuwepo kwa miaka yote na
kuwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha wanawafagia waganga hao
wanaonyesha dalili za kuvuruga utulivu uliopo katika mkoa.
“RPC fanya
Operesheni kali ya waganga wa Kienyeji ndani ya Mkoa huu, wale ambao wana
leseni tutajua hukohuko kwamba huyu ana leseni n ani halai au siyo halali na
kama sio halali basi huyo ni halali yako, na kama kuna mganga wa kienyeji asiye
na leseni, huyo ndio kabisa halali yako zaidi, kuanzia sasa hivi bonde la ziwa
Rukwa kule Nkasi, Kalambo, Sumbawanga yenyewe hapa kote, opresheni ipite ya
kamatakamata waganga wa kienyeji, tumechoka,” Alisisitiza.
Wakati
wakitoa malalamiko yao kwa mkuu huyo wa mkoa, wananchi hao walisema kuwa vifo
vya watoto hao vinahusishwa na Imani za kishirikina ambapo kumekuwa na wimbi la
vijana wanaoonekana wakila, wakinywa na kuvaa vizuri bila ya kujulikana
shughuli zao maalum wanazofanya jambo mbalo limekuwa likiwaumiza kichwa
wananchi hao na kukosa majibu.
Mmoja wa
wananchi hao Debora Maenge alisema
“Nasikitika kwa tukio hili lililotokea mtaa
wa Vuta, huyu mtu tunaishi nae jirani sana, tunajua ni mtu mwema, kumbe ni mtu
ambae sio mwema na hafai kabisa katika jamii, cha kushanga alikuwa na vibali
ambavyo alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ni mganga wa jadi, vibali hivi
vinatolewa serikalini, Je serikali yetu mtaendelea kutoa vibali hivi ili watu
waendelee kuuawa kiasi hiki? serikali angalieni mnapotoa vibali je ni waganga
Kweli?” Aliuliza.
Mh. Wangabo
alitembelea eneo la nyumba ya mganga huyo wa kienyeji ambayo gari alilowafichia
watoto ilikuwamo na kukuta nyumba hiyo ikiwa imevunjwa na gari la mganga huyo
kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali.
Watuhumiwa
James Kapyela (52) pamoja na mtoto wake Michael Martin (14) wa tukio hilo la
mauaji ya watoto Nicolous Mwambage (7) pamoja na Emanuel Juma (4) hivi sasa
wanashikiliwa na polisi huku uchunguzi wa awali ukionyesha watoto hao
walifariki kwa kukosa hewa baada ya kufungiwa ndani ya gari chakavu aina ya
Chaser Saloon iliyokuwa haitumiki na vioo vya gari hiyo kufungwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.
Joachim Wangabo akionyesha eneo katika nyumba iliyokuwa haijamalizika ambapo
maiti za watoto hao zilipatikana baada ya kutupwa na mtuhumiwa James Kapyela
ambae ni mganga wa kienyeji.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
akitoa pole kwa wazazi waliofiwa na watoto wao alipotembelea Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Rukwa mara tu baada ya kupata taarifa ya vifo vya watoto wawili na
mmoja kuwa mahututi baada ya kupatikana tangu kupotea kwao tarehe 21.3.2019.
Eneo la Nyumba ya mtuhumiwa ambaye ni Mganga wa
Kienyeji wa mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite mjini Sumbawanga baada ya nyumba hiyo
kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali baada ya kubaini kuwa mganga huyo
amesababisha vifo vya watoto wawili na mmoja kuwa mahututi.
No comments:
Post a Comment