Tuesday, March 26, 2019

POLISI PWANI YAPATA MILIONI 500 ZA KUJENGA NYUMBA.

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI

JESHI la polisi mkoani Pwani, limepatiwa sh. milioni 500 ikiwa ni ahadi ya Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt. John Magufuli, ili kuhakikisha wanajenga makazi ya kuishi askari polisi.


Ahadi hiyo aliwahi kuitoa Dkt. Magufuli April 7 mwaka jana akiwa Arusha akizindua nyumba za askari katika mkoa huo.


Akizungumzia kuhusu fedha hizo, kamanda wa polisi mkoani Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP -Wankyo Nyigesa, alisema mkoa huo ni miongoni mwa mikoa ambayo askari wake wana changamoto ya makazi hali inayosababisha kupanga uraiani ama kuishi Dar es salaam.


“Tatizo hilo hupelekea endapo kukitokea dharula askari huchukua masaa hata wakati mwingine matano kuitikia wito wa dharula “alisema Wankyo.


Wankyo alielezea, mpango huo utawezesha kuanza kwa kujenga nyumba 20 pamoja na kukabiliana na changamoto hiyo na askari kuweza kuitikia wito kwa haraka.


Alibainisha, kwasasa hatua iliyopo ni kusafisha kutoa visiki, vichuguu, vichaka na kusawazisha eneo la ujenzi ambapo wanamshukuru mdau Said Salum Bakhresa kwa kutoa katapila aina ya CAT -7R kwa ajili ya kusafisha.


Alieleza, katika kufanya hivyo ,mdau huyo ametumia milioni 75.

Kamanda huyo, aliwaomba wadau wengine kushirikiana na kuunga mkono juhudi za Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama, kwa kutoa vifaa vingine ili kuendeleza zoezi hilo na kufanikisha ujenzi huo haraka iwezekanvyo.

No comments:

Post a Comment