Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati
Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga ameeleza kuridhishwa kwake na kazi kubwa
iliyofanywa na TANESCO ya kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyokosa umeme kutokana
na kuungua kwa transfoma ya Mlandizi yanapatiwa Umeme katika kipindi kifupi.
Hayo yalibainika wakati alipofanya
ziara ya kukagua Kituo cha kupoza umeme cha Mlandizi mkoani Pwani kilichopata hitilafu tarehe 30/3/2019, majira ya Saa 1:50
asubuhi baada ya Transfoma katika kituo hicho kuungua na moto.
Akitoa maelezo kwa Kamishna, Naibu
Mkurugenzi Mtendaji anayesimamia mifumo ya Usafirishaji umeme kutoka TANESCO,
Mhandisi Isaack Chanji, alieleza kuwa, maeneo yaliyoathirika na tukio hilo ni
pamoja na Mlandizi yote, baadhi ya maeneo ya Chalinze, Kibaha, Kibamba, Mbezi
kwa Msuguri na Kimara.
Hata hivyo, maeneo yote hayo
yalipatiwa Umeme kupitia vituo vya Ubungo, Chalinze na Mlandizi chenyewe baada
ya kukamilisha matengenezo ya dharura.
Kamishna Luoga aliwataka Wataalam
kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi ya ukarabati wa Transformer
ya akiba yenye uwezo wa MVA 10 iliyopo katika Kituo hicho ifikapo tarehe 2/4/2019
ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana katika viwanda vilivyopo Kibaha
pamoja na Mitambo ya maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu.
Aidha, aliitaka TANESCO kushirikiana
na Kikosi cha Zimamoto cha Mkoa wa Pwani ili kufanya uchunguzi wa chanzo cha moto
huo pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha tatizo hilo halitokei tena.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Luoga
alikagua Kituo pamoja na kuongea na Wataalam wanaofanya kazi ya matengenezo
katika kituo hicho akiwemo Mhandisi Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
No comments:
Post a Comment