Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango (Mb) akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango
wa Maendeleo wa Taifa , Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka
2019/20, bungeni jijini Dodoma.
..................................
MAELEZO
YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB)
AKIWASILISHA MAPENDEKEZO YA
SERIKALI
YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA
NA
YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA
SERIKALI
KWA MWAKA 2019/20
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha
wabunge wote kukutana tena hapa Jijini Dodoma, kupokea mapendekezo ya Serikali
ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2019/20, kwa mujibu wa Kanuni ya 97 fasili ya (1) na (2) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016.
Aidha, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kuendelea kuijalia nchi yetu umoja na amani.
2. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii
kuwapongeza Mheshimiwa Angellah
Jasmine Kairuki (Mb), Mheshimiwa Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb), Mheshimiwa
Prof. Palamagamba Aidan Kabudi (Mb), Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb),
Mheshimiwa Joseph George Kakunda (Mb) na Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga
(Mb) kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa
Mawaziri ili kuongoza wizara mbalimbali. Ni matumaini yangu kuwa
Waheshimiwa Mawaziri mlioteuliwa na Waheshimiwa Wabunge wote mtaendelea
kunipatia ushirikiano katika kuijenga nchi yetu kwa manufaa ya Watanzania wote.
3. Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii inawasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango
wa Maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka
ujao wa fedha 2019/20 ambayo imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya
kwanza ni tathmini ya mwenendo wa hali ya uchumi. Sehemu ya pili ni Mapitio ya
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/19 na Mapendekezo ya Serikali
ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2019/20. Sehemu ya tatu ni tathmini
ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2018/19 na mapendekezo ya kiwango na ukomo
wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20.
SEHEMU
YA KWANZA
TATHMINI
YA MWENENDO WA HALI UCHUMI
4. Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuiandaa nchi
kuelekea uchumi wa kipato cha kati, uchumi umeendelea kuimarika. Pato la
Taifa kwa kutumia mwaka wa kizio 2015 linaonesha kuwa katika robo ya tatu
(Julai hadi Septemba) ya mwaka 2018, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa
asilimia 6.8 ikilinganishwa na asilimia 5.0 kipindi kama hicho mwaka 2017.
Shughuli za kiuchumi zilizokuwa kwa kasi kubwa ya ukuaji ni afya (asilimia
13.2), usafirishaji na uhifadhi mizigo (asilimia 12.4); Maji (asilimia 10.7);
Ujenzi (asilimia 7.4); Habari na Mawasiliano (asilimia 7.3); viwanda (asilimia 7.3);
na Biashara na Matengenezo (asilimia 7.3).
5. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018, mwenendo wa mfumuko wa bei nchini
uliendelea kuwa tulivu katika wigo wa tarakimu moja kutokana na kuimarika kwa
hali ya upatikanaji wa chakula nchini na nchi jirani pamoja na usimamizi
madhubuti wa sera za fedha na bajeti za Serikali. Mfumuko wa bei ulipungua
kutoka wastani wa asilimia 4.0 Januari 2018, hadi kufikia asilimia 3.4 Juni
2018 na kuendelea kupungua zaidi hadi asilimia 3.0 Januari 2019.
6. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka unaoishia Januari 2019 thamani ya
mauzo ya bidhaa na huduma nchi za nje ilikuwa dola za Marekani milioni 8,300.0
na thamani ya bidhaa na huduma zilizonunuliwa kutoka nje ilikuwa dola za
Marekani milioni 10,462.6. Kwa upande wa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa,
huduma na uhamisho wa mali nchi za nje ilikuwa dola za Marekani milioni 2,982.2
kutokana na kuongezeka kwa thamani ya bidhaa za mitaji zilizoagizwa kutoka nje
ya nchi kwa ajili ya miradi mikubwa ya maendeleo. Kwa matokeo hayo akiba ya
fedha za kigeni ni Dola za Marekani milioni 4,884.4 Januari 2019, kiasi
kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha
takribani miezi 4.8. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi 4.5.
7. Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa
wastani wa asilimia 6.6 katika mwaka 2018 ikilinganishwa na ongezeko la wastani
wa asilimia 5.5 katika kipindi cha mwaka 2017. Mwenendo huo ulichangiwa na
kuimarika kwa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kulikotokana na jitihada za
Serikali kupitia Benki Kuu katika kuchochea ongezeko la mikopo kwa sekta
binafsi. Riba za dhamana za muda mfupi za Serikali zilipungua hadi wastani wa
asilimia 6.4 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 11.1 mwaka 2017. Vile vile,
riba za mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi zimeendelea kupungua
kutoka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2017 hadi wastani wa asilimia 17.4 mwaka
2018.
8. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kuimarika kufuatia
utekelezaji wa sera ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi pamoja na jitihada
zilizochukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu katika kuchochea ongezeko la
mikopo kwa sekta binafsi. Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi imeendelea
kuongezeka ambapo Januari 2019 ilikuwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia
2.1 Januari 2018. Sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea
kuelekezwa katika shughuli binafsi (asilimia 27.9 ya mikopo yote) ikifuatiwa na
shughuli za biashara zilizopata asilimia 18.4, uzalishaji viwandani (asilimia
11.6) na kilimo (asilimia 7.8).
9. Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo wa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani
umeendelea kuwa tulivu ambapo katika mwaka 2018, Dola moja ya Marekani
ilinunuliwa kwa wastani wa Shilingi 2,263.8. Hii ni kutokana na utekelezaji
madhubuti wa sera za fedha, usimamizi thabiti wa mapato na matumizi ya
Serikali, matumizi ya gesi asilia na umeme wa maji badala ya mafuta katika
kuzalisha umeme na baadhi ya viwanda nchini kuzalisha bidhaa ambazo awali
zilikua zikiagizwa kwa wingi kutoka nje.
10.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano, itaendelea
kutekeleza sera madhubuti za fedha na bajeti ili kuhakikisha uchumi wa nchi
yetu unaendelea kuimarika.
SEHEMU
YA PILI
TATHMINI
YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2018/19 NA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO
WA MWAKA 2019/20
1. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2018/19
11.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika mwaka 2018/19, Serikali
ilitenga Shilingi bilioni 12,007.3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo,
zikijumuisha Shilingi bilioni 9,876.4 fedha za ndani na Shilingi bilioni
2,130.9 fedha za nje. Hadi Januari 2019, jumla ya Shilingi bilioni 2,788.5
zilitolewa kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, Shilingi bilioni
144 zilipokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na kupelekwa moja kwa moja
kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Wizara, Taasisi na Wakala za
Serikali, Sekretaieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Vile vile,
Shilingi bilioni 3,803.4 zimetumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo. Serikali imeshatenga na inatarajia kutoa kiasi cha
Shilingi bilioni 1,433.8 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya
maendeleo, ukiwemo mradi wa kufua umeme kwa kutumia nguvu ya maji Mto Rufiji
(MW 2,115).
12.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, hatua zilizofikiwa katika utekelezaji
wa baadhi ya miradi ya maendeleo katika mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:
(i)
Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge: Ujenzi wa kipande
cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) unaendelea vizuri kama ilivyopangwa,
ambapo shughuli zinazoendelea ni ujenzi wa madaraja, makalavati, daraja lenye
urefu wa km 2.54 katikati ya jiji la Dar es Salaam, ukataji wa miinuko, ujazaji
wa mabonde na utandikaji wa reli. Katika kipande cha Morogoro – Makutupora (km
422), kazi zinazoendelea ni pamoja na ukataji wa miinuko na ujazaji wa mabonde,
usanifu wa njia na ujenzi wa kambi za Kilosa na Ihumwa. Kwa upande wa kipande
cha Isaka – Rusumo (km 371), hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa mapitio ya
upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa njia ya reli. Aidha, taratibu za
ununuzi wa mabehewa, injini na mitambo itakayotumika kutoa huduma ya usafiri
kwenye reli ya Standard Gauge zipo katika hatua za mwisho.
Katika
miradi inayogharamiwa na mfuko wa reli, shughuli zilizofanyika ni: kununua
vichwa 11 vya treni kwa ajili reli ya kati; kuendelea na ukarabati wa reli ya
Tanga – Arusha (km 439) ambapo kipande cha Tanga – Mombo (km 129) kimeanza
kufanya kazi ya kusafirisha mizigo na ukarabati wa vipande vya Mombo – Same
(km124) na Same – Arusha (km 186) unaendelea. Aidha, kazi ya ukarabati wa
mabehewa inaendelea ambapo hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa ukarabati wa
mabehewa 15.
(ii)
Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Rufiji – MW 2,115: Hatua iliyofikiwa ni:
kupatikana kwa mkandarasi wa mradi wa kufua umeme utokanao na nguvu ya maji
katika Mto Rufiji ambaye ni Kampuni ya Ubia kati ya Arab Contractors na Elsewedy
Electric S.A.E kutoka Misri ambapo mkataba wa ujenzi umesainiwa na
mkandarasi alikabidhiwa eneo la mradi mwezi Februari 2019. Mafanikio
yaliyopatikana ni pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu wezeshi
ikijumuisha njia ya umeme wa msongo wa kV 33 kutoka Msamvu hadi eneo la mradi;
mifumo ya huduma ya maji na ya mawasiliano ya simu; kukamilika kwa ujenzi wa
nyumba 10 na kuendelea na ukarabati wa nyumba 28 za iliyokuwa kambi ya RUBADA;
ujenzi wa barabara za Kibiti – Mloka – Mtemere – Matambwe Junction – Mto
Rufiji (km 210) na Ubena Zomozi – Mvuha – Kisaki – Mtemere Junction (km
178.39) zimekamilika.
(iii)
Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Hatua iliyofikiwa ni: kuwasili kwa ndege
nyingine tatu, moja ikiwa ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na mbili zikiwa ni
Airbus A220-300, na hivyo kufanya idadi ya ndege zilizonunuliwa kuwa sita;
kulipa sehemu ya gharama za ununuzi wa ndege moja aina ya Boeing 787-8
Dreamliner na Bombadier Q400 zinazotarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwaka
2019. Kufuatia hatua hiyo, ATCL itaanzisha safari za ndege kwenda nchini China
na India ambazo kimkakati ndizo masoko mapya ya utalii.
(iv)
Miradi ya Umeme: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme
yenye urefu wa km 250 ya msongo wa kV 220 Makambako – Songea pamoja na vituo
vitatu vya kupoza umeme vya Makambako, Madaba na Songea, hivyo kuwezesha mikoa
ya Njombe na Ruvuma kuunganishwa katika Gridi ya Taifa; kuendelea na mradi wa
kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 wa Singida – Arusha – Namanga wenye urefu
wa km 414; kuendelea na miradi ya kusafirisha umeme ya Geita – Nyakanazi (kV
220), Rusumo – Nyakanazi (kV 220) na Bulyankulu – Geita (kV 220); kuendelea na
utekelezaji wa mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini na Makao Makuu ya Wilaya
ambapo vijiji 1,782 na wateja 96,832 wameunganishiwa umeme hivyo kufikia jumla
ya vijiji 1,039 vilivyounganishwa na umeme; kukamilisha utengenezaji wa mitambo
minne ya kufua umeme na kupelekwa mitambo miwili ya kufua umeme katika eneo la
mradi wa Kinyerezi I Extension – MW 185; Mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo MW 80:
Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi wa barabara za kuingia eneo la
mradi; kukamilika kwa ujenzi wa kikinga maji; kuanza kazi ya kuchimba handaki
la kupitisha maji; kuendelea na uchimbaji wa eneo itakapofungwa mitambo; na
kukamilika kwa ujenzi wa nyumba mbili kati ya tano za wafanyakazi.
(v)
Huduma za Maji Mijini na Vijijini: miradi 65 imekamilika na kufanya jumla ya
miradi yote iliyokamilika kufikia 1,659 na vituo vya kuchotea maji kuongezeka
hadi 131,370 na kuhudumia wananchi 25,359,290. Upatikanaji wa huduma za maji
Jijini Dar es Salaam umefikia asilimia 85, katika mikoa mingine asilimia 80,
miji midogo asilimia 64 na vijijini asilimia 64.8. Aidha, utekelezaji wa miradi
ya maji katika maeneo mengine unaendelea katika hatua mbalimbali ikiwa ni
pamoja na mradi wa maji wa Ziwa Victoria – Igunga – Nzega na Tabora, mradi wa
maji katika jiji la Arusha na Same – Mwanga – Korogwe. Vile vile, utekelezaji
wa mradi wa maji katika miji 28 wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 465
upo katika hatua za kumpata Mtaalamu Mwelekezi na Mkandarasi wa mradi.
(vi)
Miradi ya Afya: Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza
upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa asilimia
96. Hatua nyingine zilizofikiwa ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa jengo la
vifaa vya uchunguzi (X–Ray Building) na kununua vifaa vya tiba ya mionzi
katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya; na kuongeza utoaji wa chanjo kufikia
asilimia 97. Aidha, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya afya katika
ngazi zote ikijumuisha ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa,
kanda na kitaifa; ujenzi wa hospitali za halmashauri 67; ujenzi wa vituo vya
kutolea huduma za afya 352; kuajiriwa kwa watumishi wa sekta ya afya 7,680; ujenzi
wa nyumba 310 za watumishi wa afya; ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa
Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za halmashauri, Vituo vya Afya na
Zahanati. Serikali imeendelea kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa kwa
kuboresha miundombinu ya kutolea huduma, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na
hivyo kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi katika hospitali za Muhimbili,
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road
(ORCI), Taasisi ya Mifupa (MOI), hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali
ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi – Mloganzila.
(vii)
Miradi ya Elimu: Serikali imeendelea kugharamia elimumsingi bila ada ambapo
kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 24.4 kinatumika. Hatua nyingine zilizofikiwa
ni: ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikijumuisha
madarasa 870, matundu ya vyoo 1,958, mabweni 210, mabwalo 79; ukarabati wa
shule kongwe; ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vya ualimu Ndala,
Shinyanga, Patandi, Mpuguso na Murutunguru; kukamilisha maboma ya madarasa,
mabweni na nyumba za walimu 39; ukarabati wa vyuo vya kati 20 kati ya 54 vya
Maendeleo ya Wananchi (FDCs), nyumba za walimu 39; kukamilika na kuzinduliwa
kwa Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,600 kwa wakati
mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; ujenzi wa mabweni katika Chuo Kikuu
cha Mzumbe yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000; ujenzi na ukarabati wa
miundombinu katika vyuo vikuu vya Sokoine na Dar es Saaalm; na mikopo kwa
wanafunzi wa Elimu ya Juu 119,214; uimarishaji wa vyuo 10 vipya vya VETA na
kukuza ujuzi kwa vijana; na ujenzi wa shule kwa ajili ya wanafunzi wenye
mahitaji maalum katika chuo cha Ualimu Patandi.
(viii)
Kilimo: Utoshelevu wa Chakula kwa mwaka 2018/19 umefikia asilimia 124. Aidha,
Serikali imeanza utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya
pili (ASDP II) na mkazo umewekwa katika kuendeleza mazao ya kimkakati yakiwemo
Kahawa, Pamba, Chai, Korosho, Tumbaku, Alizeti, Michikichi, Mpunga na Mahindi.
Ili kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo, Serikali inaendelea kuimarisha shughuli
za ushirika, ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa vyenye uwezo wa kuhifadhi
tani 250,000 katika kanda saba, kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta hususan
alizeti na michikichi, kuimarisha shughuli za utafiti wa mazao, kuongeza
thamani ya mazao ya kilimo kwa kufufua vinu vya kusindika mazao ya nafaka na
mafuta, kudhibiti visumbufu vya mazao, kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa
pembejeo za kilimo na kuimarisha mifumo ya masoko ya mazao. Vile vile, Serikali
imeanza kuboresha mifumo ya takwimu za kilimo kwa kuanza usajili wa Wakulima.
(ix)
Mifugo: Hatua iliyofikiwa ni kuendelea kuimarisha vituo 3 vya kuzalisha
vifaranga vya samaki vya Kingolwira (Morogoro), Mwampuli (Igunga) na Ruhila
(Songea) kwa kuzalisha na kusambaza vifaranga vya samaki kwa wafugaji wa
samaki wakiwemo vijana. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na sekta Binafsi
imeweza kuzalisha jumla ya vifaranga 17,301,076 kama ifuatavyo: kambamiti 11,080,000,
sato 5,072,800 na kambale 1,148,276. Vile vile, jumla ya wananchi 6,995
wamepatiwa elimu ya ugani katika ukuzaji wa viumbe maji.
(x)
Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga
(Tanzania): Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa tathmini ya athari za
mazingira na jamii kwa upande wa Tanzania; kukamilika kwa tafiti za kijiolojia
katika eneo la Chongoleani; kukamilika kwa tathmini za Kijiolojia na
Kijiofizikia katika eneo la mkuza wa bomba; na kutwaa ardhi eneo la Bandari –
Tanga (Chongoleani) kutakapojengwa miundombinu ya kuhifadhi mafuta.
(xi)
Miradi ya Viwanda: Kiwanda cha Kuunganisha Matrekta (TAMCO, Kibaha): Hatua
iliyofikiwa ni: kuingiza matrekta 822 aina ya URSUS (semi knocked down) ambapo
matrekta 571 yameunganishwa na matrekta 339 yameuzwa; Kituo cha Zana za Kilimo
na Ufundi Vijijini – CAMARTEC: kutengeneza zana zikijumuisha mashine 64 za
kupandia mbegu za pamba, kusaga karanga, kukausha mbogamboga na kukata majani
pamoja na ujenzi wa mitambo 55 ya biogas; SIDO: kuendelea na
ujenzi wa majengo ya viwanda 11 katika Mikoa ya Dodoma, Geita, Kagera, Katavi,
Manyara, Mtwara na Simiyu na ujenzi wa ofisi za SIDO katika mikoa mipya ya
Geita na Katavi.
(xii)
Miundombinu ya Biashara ya Madini: Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa
miundombinu ya kuboresha mazingira ya biashara kwenye sekta ya madini
ikihusisha: vituo vya umahiri katika mikoa saba, vituo vitatu vya mfano, jengo
la taaluma la madini katika chuo cha madini, One Stop centre Mirerani, Brokers
house Mirerani, uanzishwaji wa masoko ya madini mikoani, na uwekaji wa
mfumo wa ulinzi wa kidigitali Mirerani, ununuzi wa mtambo wa uchorongaji miamba
kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo kupitia STAMICO.
(xiii)
Ardhi na Makazi: Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na: kuandaliwa na kusajiliwa
kwa Hati Milki 110,000 na Hati za Kimila 133,000; kuandaliwa kwa mipango ya
matumizi ya ardhi ya vijiji 263 katika Wilaya 45; kuandaliwa kwa Mipango
Kabambe ya miji mikuu ya mikoa ya Arusha, Mwanza, Mtwara, Mara, Singida, Iringa
na Pwani, Ruvuma, Tabora na Simiyu; kuendelea na hatua za maandalizi ya Mipango
Kabambe ya miji mikuu ya mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Rukwa, Shinyanga,
Manyara, Dodoma, Tanga, Mbeya, Kagera, Kigoma, Katavi, Lindi, Kilimanjaro, Njombe
na Geita; kuanzishwa kwa Mfumo Unganishi wa Taarifa za Ardhi; na kuongezeka kwa
idadi ya benki na taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba kufikia 31 na
kuwanufaisha wananchi 4,174. Aidha, Mfuko wa Mikopo Midogo Midogo ya Nyumba
ulio chini ya Benki Kuu umeongezewa mtaji wa dola za Marekani milioni 18 ambapo
taasisi za fedha tano (5) zimepatiwa mtaji wa shilingi bilioni 13.87 kwa ajili
ya kukopesha wananchi wa kipato cha chini kwa masharti nafuu.
(xiv)
Ujenzi wa Barabara Dar es Salaam: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi
wa barabara ya juu katika makutano ya TAZARA (Mfugale flyover); kuendelea na
ujenzi wa barabara za muingiliano Ubungo; mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es
Salaam km 210 za barabara kwa kiwango cha lami; na kuendelea na ujenzi wa
barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (km 19) kwa njia nane.
(xv)
Ujenzi wa Meli: Hatua iliyofikiwa ni: kuendelea na Ujenzi wa meli mpya yenye
uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika ziwa Victoria;
kufikia asilimia 82 ya ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria
200 na mizigo tani 200 za mizigo katika ziwa Nyasa; na kukamilika kwa ujenzi wa
matishari mawili katika Ziwa Nyasa. Kwa upande wa Ziwa Tanganyika, Ujenzi wa
Meli Mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo, ambapo
uandaaji wa mikataba kwa ajili ya ujenzi wa meli hiyo pamoja na ukarabati wa
meli ya MV Liemba umekamilika. Miradi mingine ni kukamilika kwa ujenzi wa
kivuko kipya cha Kigongo – Busisi; kukamilika kwa ukarabati wa kivuko cha MV Pangani
II; kuendelea kukarabati vivuko vya MV Sengerema, MV Kigamboni na MV Misungwi.
(xvi)
Viwanja vya Ndege: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa asilimia 90.7 ya ujenzi
wa jengo jipya la abiria (Terminal III) katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere; kuendelea na upanuzi wa maegesho ya ndege, ujenzi wa jengo la
mizigo, uzio wa kiwanja, maegesho ya ndege za mizigo na jengo la kuongozea
ndege katika kiwanja cha ndege cha Mwanza. Aidha, ujenzi na ukarabati wa
viwanja vya ndege vya mikoa vikiwemo vya Sumbawanga, Kigoma, Shinyanga, Mtwara,
Songea, Mara, Songwe, Mbeya, Mwanza, Kigoma, Tabora na Iringa unaendelea.
(xvii)
Mawasiliano: Hatua iliyofikiwa ni: kuendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano ambapo vituo vitatu (3) vya Mkongo katika maeneo ya Tukuyu, Kibaha
na Kahama vimejengwa na kuvipa nguvu vituo vitatu (3) vya mkongo (Optical Line
Amplifier (OLA) katika maeneo ya Ifakara, Kidatu na Mafinga; na kuendelea
kutekeleza mradi wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi umetekelezwa kwa
kubandika vibao vya namba za nyumba katika Halmashauri 12. Vile vile, Mfumo wa
Usimamizi na Ufuatiliaji wa Mawasiliano ya Simu (TTMS) umekabidhiwa rasmi
kutoka kwa Mkandarasi SGS/GVG ambapo katika kipindi cha Julai, 2018 hadi
Februari, 2019 jumla ya miamala 2,004,196,139 imepita katika mitandao ya simu
na wastani wa fedha zilizopita ni Shilingi bilioni 12,202.7.
(xviii)
Uendelezaji wa Bandari: Bandari ya Dar es Salaam: Hatua iliyofikiwa ni:
kukamilika kwa ujenzi na kuanza kutumika kwa gati Na.1; na kuendelea na ujenzi
wa sakafu ngumu katika gati la kupakua na kupakia magari; Bandari ya Tanga:
ukarabati wa miundombinu ya barabara kuelekea lango Na. 2 umekamilika; Bandari
ya Mtwara: ujenzi wa gati la mita 300 la kuhudumia shehena mchanganyiko unaendelea.
Aidha, ujenzi wa Bandari katika Maziwa Makuu (Ziwa Victoria, Tanganyika na
Nyasa) unaendelea.
(xix)
Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: kazi zilizofanyika ni kujengwa kilomita
140.42 za barabara kuu na kilomita 12.43 za barabara za mikoa kwa kiwango cha
lami. Aidha, kwa upande wa madaraja hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa ujenzi
wa Daraja la Mlalakuwa (Dar es Salaam); kuendelea na ujenzi wa madaraja ya
Momba (Rukwa) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 94, Sibiti (Singida)
asilimia 88.35, Mara (Mara) asilimia 85; na Ruhuhu (Ruvuma) asilimia 76; na
kuanza ujenzi wa Daraja Jipya la Selander na barabara unganishi zenye urefu wa
kilomita 5.2.
(xx)
Ufungaji wa rada nne za kuongozea ndege za kiraia JNIA, KIA, Mwanza na Songwe:
Hatua iliyofikiwa ni: JNIA: Kukamilika kwa asilimia 95 ya miundombinu ya rada.
Mwanza: Ujenzi wa miundombinu ya rada unaendelea vizuri. KIA: Ujenzi wa
miundombinu ya rada unaendelea na umefikia asilimia 90. Songwe: taratibu
za ujenzi wa miundombinu zinaendelea. Aidha, mitambo itafungwa miundombinu
itakapokamilika.
(xxi)
Miradi ya Mahakama: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama za
Wilaya za Bukombe, Chato, Ruangwa, Geita na Kilwa; kukamilika kwa ujenzi wa
Mahakama za Mwanzo za Magoma (Korogwe) na Mlowo (Mbozi); kuendelea na ujenzi wa
Mahakama za mikoa ya Njombe, Katavi, Lindi na Simiyu; kuendelea na ujenzi wa
Mahakama za Wilaya za Kasulu, Sikonge, Kilindi, Bunda, Longido, Kondoa, Njombe,
Rungwe, Chunya, Wanging’ombe, na Makete; kuendelea na ujenzi wa Mahakama Kuu
Kigoma na Mara ambao umefikia asilimia 80; ujenzi wa Mahakama za Mwanzo za
Mkunya (Newala), Uyole (Mbeya), Ngerengere, Mlimba na Mang’ula (Morogoro);
ukarabati mkubwa wa nyumba tatu za kufikia Majaji Mtwara; na kukamilika kwa
uboreshaji wa mfumo wa ukusanyaji takwimu na kusajili mashauri, kuingiza
taarifa muhimu za wadaawa ikiwa ni pamoja na kutuma taarifa kwa ujumbe mfupi
(sms) kwa wadaawa kuhusu mwenendo wa mashauri. Aidha, imeanzishwa huduma ya
mahakama zinazotembea (mobile court, kwa kuanzia na mikoa ya Dar es salaam na
Mwanza, magari ambayo yamezinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mh. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwezi Februari 2019.
(xxii)
Miradi ya Kimkakati ya kuongeza mapato katika Halmashauri: Hatua iliyofikiwa ni
utekelezaji wa miradi ya kimkakati 37 ya kuongeza mapato ya halmashauri na
kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali ikijumuisha Soko
la kisasa – manispaa ya Morogoro, soko la kisasa – halmashauri ya mji Kibaha,
Pwani, ghala la kisasa – halmshauri ya wilaya ya Ruangwa, kituo cha mabasi
Mbezi Louis – Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, soko la Mburahati –
manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, ujenzi na upanuzi wa kiwanda cha kutengeneza
chaki na kiwanda cha vifungashio – halmashauri ya wilaya ya Maswa, Simiyu,
stendi ya mabasi Korogwe. Miradi hii inatekelezwa katika halmashauri 29 na ipo
katika hatua mbalimbali.
(xxiii)
Uwekezaji: Sekta ya Uwekezaji imeendelea kukua ikilinganishwa na nchi nyingine
za Afrika Mashariki ambapo ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonesha
Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji kati ya nchi za Afrika Mashariki. Kwa
mfano, Ripoti ya Uwekezaji ya Dunia ya mwaka 2018 inayotolewa na Shirika la
Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) inaonesha kuwa Tanzania
imevutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 1,180,
ikifuatiwa na Uganda Dola za Kimarekani milioni 700 na Kenya Dola za Kimarekani
milioni 672. Aidha, ripoti ya “Where to Invest in Africa” ya mwaka 2018
inayojulikana kama RMB’s Investment Attractiveness Index inayoonesha
nchi zinazovutia zaidi kwa uwekezaji barani Afrika, Tanzania imeendelea kuwa
katika kumi bora kwa kushika nafasi ya saba (7) kati ya nchi 52 ikipanda kutoka
nafasi ya 9 mwaka 2017.
Aidha,
jitihada za Serikali kuhamasisha ujenzi wa viwanda nchini zimewezesha
kuongezeka mitaji katika viwanda mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mtaji uliowekezwa
chini ya Mamlaka ya EPZ umeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.422 mwaka
2016 hadi Dola za Marekani bilioni 2.23 hapo Novemba, 2018, ikiwa ni ongezeko
la Dola za Marekani milioni 808 (sawa na ongezeko la asilimia 56.8). Mwenendo
wa mauzo ya bidhaa za viwanda hivyo nje ya nchi yamekuwa yakiongezeka mwaka
hadi mwaka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.194 hapo Novemba 2018, kutoka
Dola za Marekani bilioni 1.1 mwaka 2016, ikiwa ni ongezeko la asilimia 99.45.
Mtaji mkubwa umewekezwa katika viwanda vya kuongeza thamani mazao (agro
processing) ambapo ina asilimia 38 ya mtaji wote; zikifuatiwa na viwanda vya
kuunganisha mitambo (assembling & engineering) asilimia 31 ya mtaji, mavazi
na nguo asilimia 21 ya mtaji na uchakataji madini asilimia 10 ya mtaji. Aidha,
viwanda 71 ni vya makampuni ya kigeni, viwanda 58 ni vya makampuni ya ubia na
viwanda 45 ni vya makampuni ya ndani.
(xxiv)
Kuhamishia Utekelezaji wa Majukumu ya Serikali Makao Makuu Dodoma: Serikali
imetekeleza azma yake ya kuhamia Makao Makuu ya Nchi, Dodoma ambapo mpaka hivi
sasa Wizara zote zimeshahamia Dodoma na jumla ya Watumishi 8,883 wanatekeleza
majukumu yao wakiwa hapa Dodoma (Watumishi hao ni kutoka Ofisi/Wizara na Vyombo
vya Ulinzi na Usalama). Vile vile, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu,
Mawaziri na Naibu Mawaziri pia wameshamia Dodoma. Uendelezaji wa eneo la Mji wa
Serikali – Ihumwa umeanza na jumla ya majengo 22 ya Ofisi za Wizara na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali yako katika hatua za mwisho za ujenzi.
(xxv)
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana: Serikali imeendelea kuwawezesha Vijana kiuchumi
ili waweze kujiajiri katika nyanja za uzalishaji mali na kutoa huduma ambapo
hatua iliyofikiwa ni: kutolewa kwa mikopo nafuu yenye thamani ya Shilingi
bilioni 2.74 kwa vikundi vya vijana 523, vyenye wanachama 3,661 katika
Halmashauri 128 za Tanzania Bara; na kuanzishwa kwa SACCOS 127 za Vijana kati ya
184 zinazotarajiwa kuanzishwa hadi kufikia mwaka 2020.
(xxvi)
Mafanikio mengine ni kuendelea kuimarika kwa Amani, utulivu na usalama nchini
hivyo, kuwezesha kukua kwa shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika kutimiza
jukumu hilo, Jeshi la Polisi limeendelea kuweka juhudi katika kudhibiti uhalifu
sanjari na kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili jamii
ibadilike na kuachana na matukio ya uhalifu.
(xxvii)
Mazingira: Serikali imetekeleza hughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuimarisha mfumo wa ikolojia ili kuhimili mabadiliko ya tabia nchi, kujenga
uwezo w taasisi na jamii kuhimili changamoto za mazingira na athari za
mabadiliko ya tabia nchi na kuboresha kanuni za kutoa leseni za tathmini ya
mazingira kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa leseni za muda kabla ya kuanza
mradi.
(xxviii)
Miradi ya Sekta Binafsi: Sekta hii imeendelea kushiriki katika ujenzi wa
viwanda ambapo katika kipindi cha 2015 hadi 2018, jumla ya viwanda 3,530
vilijengwa na kuanza uzalishaji.
1. MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2019/20
13.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/20 ni wa nne katika mfululizo wa
mipango ya kila mwaka ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
Mitano 2016/17 – 2020/21, wenye dhima ya Kujenga Uchumi wa Viwanda ili
Kuchochea Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo ya Watu. Maandalizi ya Mpango huu
yamezingatia azma ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; na
Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
14.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 yanatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa
katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambavyo
ni:
(i)
Viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda: Miradi
itakayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye lengo la kujenga viwanda
vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hususan kilimo, madini na gesi
asilia. Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia,
Uanzishwaji na Uendelezaji wa Kanda Maalamu za Kiuchumi na Kongane za Viwanda,
viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuongeza thamani
ya madini na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu;
(ii)
Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi itakayotekelezwa
katika eneo hili ni ile yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya,
elimu na ujuzi, upatikanaji wa chakula na lishe bora na huduma za maji safi na
salama. Shughuli zitakazotiliwa mkazo ni pamoja na kugharamia utoaji wa elimu
msingi bila ada, kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi,
utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (Programu ya Lipa
Kulingana na Matokeo katika Elimu), ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi
stadi nchini, kuboresha huduma za maji vijijini;
(iii)
Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji: Miradi
itakayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye lengo la kuendeleza ujenzi na
ukarabati wa miundombinu (reli, bandari, nishati, viwanja vya ndege, barabara).
Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Rufiji MW 2,115;
Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard
Gauge; na kuendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti
wa Biashara na Uwekezaji. Aidha, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20
umeweka msukumo katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza
ikiwemo kupitia upya mfumo wa kitaasisi, kisera na kisheria pamoja na kanuni
zake ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika kuwekeza kwenye
miradi ya maendeleo; na
(iv)
Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango: Miradi inayotekelezwa katika
eneo hili inalenga kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji wa Mpango,
kuweka mfumo utakaowezesha upatikanaji wa uhakika wa rasilimali fedha na kuweka
vigezo vya upimaji wa mafanikio ya utekelezaji.
SEHEMU
YA TATU
TATHMINI
YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19 NA MAPENDEKEZO YA KIWANGO NA UKOMO WA
BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2019/20
1. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19
15.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, mwaka 2018/19, Serikali ilipanga
kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 32,476.0. Kiasi hicho
kinajumuisha: mapato ya ndani shilingi bilioni 20,894.6; misaada na mikopo
nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo shilingi bilioni 2,676.6; na mikopo
yenye masharti ya kibiashara kutoka vyanzo vya ndani na nje shilingi bilioni
8,904.7. Aidha, matumizi ya kawaida yalikadiriwa kuwa shilingi bilioni 20,468.7
na matumizi ya maendeleo shilingi bilioni 12,007.3.
16.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kipindi cha Julai 2018 hadi Januari
2019, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 9,111.9, mapato yasiyo ya kodi
shilingi bilioni 1,522.9 na mapato yaliyokusanywa na Halmashauri yalikuwa
shilingi bilioni 371.7.
17.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua
mbalimbali za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji kama
ilivyoainishwa ndani ya Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara na
Uwekezaji (Blueprint) kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na
kuongeza mapato ya Serikali. Hatua hizo ni pamoja na: Kupunguza kodi kwa
wachimbaji wadogo wa madini; Ugawaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo
wadogo; Kupunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa unaotozwa kwenye pombe kali
zinazotengenezwa nchini kwa kutumia zabibu zinazozalishwa nchini; Kuweka
utaratibu mpya wa ukusanyaji wa kodi ya majengo; Kuboresha mifumo ya TEHAMA ya
kukusanya kodi na maduhuli ikiwemo Electronic Fiscal Device Management System
(EFDMS) ambao hupokea na kutunza kumbukumbu za utoaji wa risiti za mauzo.
18.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, hadi Januari 2019, Washirika wa
Maendeleo walitoa jumla ya shilingi bilioni 1,034.8. Kati ya kiasi kilichotolewa,
misaada na mikopo nafuu ya Kibajeti ilikuwa shilingi bilioni 125.4 na miradi ya
maendeleo shilingi bilioni 782.0. Mifuko ya Kisekta ilipokea shilingi bilioni
127.4.
19.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2018 hadi
Januari 2019, Serikali ilikopa shilingi bilioni 2,025.0 kutoka soko la ndani.
Aidha, katika kipindi hicho, Serikali ilifanya majadiliano na taasisi
mbalimbali za kifedha za kimataifa na kupata shilingi bilioni 458.6 kutoka
Benki ya Credit Suisse mwezi Februari 2019 na shilingi bilioni 247.7
zinatarajiwa kupatikana kutoka benki ya HSBC hivi karibuni. Vile vile, Serikali
ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na baadhi ya wakopeshaji walioonesha
nia ya kuikopesha Serikali kwa mwaka 2018/19.
20.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2018 hadi
Januari 2019, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi ya jumla ya shilingi bilioni
13,750.6. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 10,962.1 zilitolewa kwa ajili
ya Matumizi ya Kawaida na shilingi bilioni 2,788.5 zilitolewa kwa ajili ya matumizi
ya maendeleo. Mahitaji yaliyopewa kipaumbele katika utoaji wa fedha ni pamoja
na: Ulipaji wa deni la Serikali ikijumuisha michango ya mwajiri katika Mifuko
ya Hifadhi ya Jamii shilingi bilioni 5,465.9 ambapo Shilingi bilioni 3,803.4
zimetumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo;
na mishahara ya watumishi wa Serikali shilingi bilioni 3,890.0. Serikali
imeshatenga na inatarajia kutoa kiasi cha Shilingi bilioni 1,433.8 kwa ajili ya
kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo mradi wa kufua umeme kwa
kutumia nguvu ya maji Mto Rufiji (MW 2,115).
21.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuchukua hatua
mbalimbali za kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ili kufikia
malengo ya bajeti ya mwaka 2018/19. Miongoni mwa mikakati hiyo ni: Kuhamasisha
ulipaji wa kodi kwa hiari kupitia vipindi mbalimbali vya elimu kwa umma;
Kutekeleza mwongozo wa ushirikiano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo;
Kuendelea kusisitiza nidhamu ya matumizi katika utekelezaji wa bajeti kwa
kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya Mwaka 2015; kulipa madai yote
yaliyohakikiwa ya makandarasi; Kuanza kutumika kwa Mfumo wa Kielektroniki wa
Stampu za kodi (ETS) ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi; na
Kutekeleza Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS) ili kuongeza
ufanisi katika usimamizi wa makusanyo ya kodi za ndani.
1. SERA ZA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/20
22.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Sera za mapato kwa mwaka 2019/20
zitalenga: Kuboresha mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji,
ukuaji wa biashara ndogondogo na za kati pamoja na ukuaji wa uchumi endelevu;
Kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari, upanuzi wa wigo wa kodi na
matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika usimamizi wa kodi; Kuimarisha usimamizi wa
sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa
mapato; Kuwianisha na kupunguza tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wakala za
Serikali na Mamlaka za Udhibiti; na Kuwajengea uwezo maafisa wa Wizara, Idara
Zinazojitegemea, Wakala na Halmashauri ili kuimarisha uwezo wa ukusanyaji wa
mapato yasiyo ya kodi.
23.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, uboreshaji wa mazingira haya
utawezesha kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uwekezaji, uzalishaji, ajira na
miamala ya biashara ambayo kwa ujumla itachangia kuongezeka kwa vyanzo vya
mapato. Aidha, kwa upande wa misaada na mikopo nafuu, Serikali itaendelea
kuimarisha mahusiano kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Ushirikiano na Washirika
wa Maendeleo.
No comments:
Post a Comment