Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki imepokea kwa masikitiko makubwa, taarifa kuhusu ajali ya
ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Ethiopia, iliyotokea tarehe 10 Machi
2019 nchini Ethiopia na kusababisha vifo vya watu wote 157 waliokuwemo kwenye
ndege hiyo.
Ndege hiyo
ya abiria, aina ya Boeing 737 yenye namba za usajili ET 302 iliyokuwa
inafanya safari zake za kawaida kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole,
mjini Addis Ababa, Ethiopia kuelekea mjini Nairobi, Kenya, ilikuwa imebeba
abiria 149 kutoka mataifa mbalimbali na wafanyakazi wa kwenye ndege wapatao 8.
Kwa mujibu
wa taarifa kuhusu ajali hiyo, iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Afisa
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Ethiopia, ikiwemo orodha ya abiria na
mataifa wanayotoka, hakuna Mtanzania aliyekuwemo kwenye ndege hiyo.
Orodha ya
nchi na idadi ya raia (kwenye mabano) waliokuwa kwenye ndege hiyo ni kama
ifuatavyo: Kenya (32), Canada (18), Ethiopia (9), China (8), Italia (8),
Marekani (8), Ufaransa (7), Uingereza (7), Misri (6), Ujerumani (5), India (4),
Slovakia (4), Austria (3), Urusi (3), Sweden (3), Hispania (2), Israel (2),
Morocco (2) na Poland (2).
Nchi
zingine ni Ubelgiji (1), Djibouti (1), Indonesia (1), Ireland (1), Msumbiji
(1), Norway (1), Rwanda (1), Saudi Arabia (1), Sudan (1), Somalia (1), Serbia
(1), Togo (1), Uganda (1), Yemen (1), Nepal (1), Nigeria (1) na raia aliyekuwa
na hati ya kusafiria ya Umoja wa Mataifa (1).
Mamlaka
husika zimeanza uchunguzi ili kujua chanzo cha ajali hiyo.
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaungana na wote walioguswa na msiba huu mzito
kutoa pole kwa mataifa yote yaliyopoteza raia wake kwenye ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment