Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP)
Simon Sirro amefanya mabadiliko ya kiuongozi kwa maofisa wa jeshi hilo
baada ya Rais John Magufuli kufanya uteuzi wa makamishna wapya.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Machi Mosi, IGP Sirro amewataja
makamishna walioteuliwa na Rais Magufuli kuwa ni Charles Mkumbo ambaye
anakwenda kuongoza kamisheni ya intelijensia na Liberatus Sabas ambaye
anakuwa mkuu wa operesheni na mafunzo.
Wengine ni Leonard Lwabuzala ambaye ataongoza kamisheni ya fedha na
logistics na Benedicto Wakulyamba ambaye anakuwa mkuu wa kamisheni ya
utawala na menejimenti ya utumishi na Shaaban Mlai ambaye ataongoza
kamisheni ya maabara ya uchunguzi wa kisayansi.
Mbali na makamishna hao, Sirro amefanya mabadiliko ya kiutawala kwa
maofisa wa jeshi hilo; James Mushi ambaye alikuwa kamanda wa polisi mkoa
wa Ruvuma anakuwa Mkuu wa Chuo cha Polisi (CCP) Moshi wakati RPC wa
Njombe, Renata Mzinga akirudishwa Makao Makuu.
Sirro amewataja makamanda wapya wa mikoa kuwa ni Amon Kakwale (RPC wa
Temeke), Jonathan Shana (RPC Arusha), Marwa Mahiga (RPC Ruvuma), Salum
Hamduni (RPC Njombe) na Zuberi Chembela (RPC Ilala).
Viongozi wengine waliohamishwa vituo vya kazi ni Mihayo Nsekela (ofisi
ya operesheni na mafunzo), Simon Haule ambaye alikuwa RPC wa Shinyanga
anarudishwa Makao Makuu na Yusuph Sarungi ambaye alikuwa RPC Songwe
anakuwa mkuu wa kitengo cha kushughulikia wizi wa mifugo (SPU).
Benedict Mapugila ameteuliwa kuongoza kikosi cha bandari wakati Michael
Marwa anapelekwa makao makuu Zanzibar. Sirro amesema Albert Nyamhanga na
Nsato Marijani wanakwenda Idara ya Wakimbizi ambayo iko chini ya Idara
ya Uhamiaji.
No comments:
Post a Comment