Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili-kushoto),
akitoa maelekezo kwa Mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini wilayani
Muheza (shati ya bluu-katikati), alipotembelea genge lake lenye vifaa vya kazi
akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo Machi 29, 2019. Katikati-mwenye
ushungi ni Mkuu wa Wilaya, hiyo Mhandisi Mwanaasha Tumbo na wa kwanza kushoto ni
Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu.
.................................
Na Veronica Simba – Muheza
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema Serikali ya
Awamu ya Tano imedhamiria kuwafikishia huduma ya umeme watanzania wote bila
kubagua aina ya makazi yao na kwamba itaendelea kutekeleza jukumu hilo pasipo
kukatishwa tamaa na yeyote.
Aliyasema hayo Machi 29, 2019 akiwa katika ziara ya
kazi wilayani Muheza, ambapo aliwasha umeme katika vijiji vya Mamboleo-Lusanga,
Mamboleo-Nkumba na Misongeni. Vilevile, alikagua genge la Mkandarasi
anayetekeleza miradi ya umeme vijijini wilayani humo pamoja na kuzungumza na
wananchi.
Naibu Waziri alisema kumekuwepo na maneno ya baadhi ya watu
kubeza jitihada zinazofanywa na Serikali kuwaunganishia umeme watanzania wote
hususani waishio vijijini pasipo ubaguzi, wakitoa sababu kwamba wenye nyumba za
nyasi hawastahili kupatiwa huduma hiyo.
Akifafanua, alisema kuwa, wataalamu wa serikali wamekuwa
wakihakikisha taratibu za usalama zinafuatwa wakati wa kuunganisha umeme katika
nyumba za vijijini, hususani zilizoezekwa kwa makuti au nyasi.
Aliwataka wananchi kuondoa hofu kuwa madhara yanaweza
kutokea katika nyumba za aina hiyo ambazo zimeunganishiwa umeme na badala yake
wawapuuze watu wanaobeza jitihada hizo, na zaidi wautumie umeme kujiletea
manufaa katika maisha yao.
Pia, Naibu Waziri alieleza kuwa, kazi ya kuwapelekea
wananchi wa vijijini umeme inafanyika sambamba na zoezi la uhamasishaji wa
kujenga makazi bora.
Alisema, mwananchi mwenye makazi duni akiunganishiwa umeme,
anapata hamasa ya kuboresha zaidi makazi yake na hilo limekuwa likifanyika
sehemu mbalimbali nchini kote.
“Maelekezo yetu kwa wakandarasi ni kutobagua nyumba ya aina
yoyote. Watanzania wote wanahitaji umeme pasipo ubaguzi wa aina yoyote. Hakuna
sababu ya mtu aliye karibu na miundombinu, halafu asiunganishiwe umeme,”
alisisitiza.
Baadhi ya wananchi wenye nyumba zilizoezekwa kwa makuti
wilayani Muheza na ambao wameunganishiwa umeme, akiwemo Musa Rashidi, mkazi wa
kijiji cha Mamboleo, waliipongeza Serikali na kutoa shukrani nyingi kwa
kuwapatia huduma ya umeme pasipo kuwabagua. Waliahidi kuboresha zaidi makazi
yao.
“Naishukuru sana Serikali kwa kuniunganishia umeme katika
nyumba yangu, maana kabla ya huduma hii, hali haikuwa nzuri hapa nyumbani. Nimefarijika
sana,” alisema Musa.
Awali, akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya
hiyo, ofisini kwa Mkuu wa Wilaya, Naibu Waziri alisema suala la kukatika-katika
kwa umeme wilayani humo linatokana na njia inayotumika kusafirisha umeme, yenye
msongo wa kilovoti 132 kuzidiwa nguvu kutokana na matumizi kuongezeka.
“Ndiyo maana serikali ikaja na mpango wa kujenga njia
nyingine ya umeme yenye uwezo wa kilovoti 400 kutoka Kinyerezi – Kibaha –
Chalinze – Segera hadi Tanga ili kuboresha hali ya upatikanaji umeme mkoani
humu,” alisema Naibu Waziri.
Aidha, Naibu Waziri aliuagiza uongozi wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO), mkoani Tanga na nchi nzima kwa ujumla, kuboresha utoaji
taarifa kwa viongozi na wananchi.
Aliwataka kutoa taarifa kwa wakati kunapokuwa na ratiba ya
kukatika kwa umeme, ikiwa ni pamoja na kueleza umeme utakatika muda gani, kwa
sababu gani, maeneo yatakayoathirika pamoja na hatua zinazochukuliwa kutatua
tatizo husika.
Vilevile, aliwataka wananchi wa Mkoa wa Tanga, ambao wana
utamaduni wa kuchoma moto maeneo mbalimbali kwa ajili ya kilimo, kuchukua
tahadhari ili kutoathiri miundombinu ya umeme.
“Natoa rai kwa wananchi, unapohujumu miundombinu ya umeme ni
kosa kisheria maana ni uhujumu uchumi. Na mkumbuke, serikali inatumia gharama
kubwa kuwekeza katika miundombinu husika.”
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanaasha Tumbo,
alimweleza Naibu Waziri kuwa Wilaya hiyo imekuwa ikipata matatizo ya kukatika
umeme mara kwa mara.
Naye Mbunge wa Jimbo la Muheza, Adadi Rajabu (CCM), alisema
umeme wa REA umekuwa ni jambo la kufurahisha kiasi kwamba wale ambao
hawajafikiwa na huduma hiyo wanalalamika.
Hivyo, alimwomba Naibu Waziri
kusimamia suala hilo ili vijiji na vitongoji ambavyo havijafikiwa, vipelekewe
umeme mapema.
Taarifa ya TANESCO wilayani Muheza inabainisha kuwa; vijiji
87 kati ya 135 vya Wilaya hiyo tayari vina umeme ambapo ni sawa na asilimia 64.
Mradi wa REA III Mzunguko wa I ukikamilika mwishoni mwa Juni mwaka huu,
asilimia 75 ya vijiji vya wilaya husika vitakuwa na umeme.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisalimiana na
viongozi pamoja na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza,
alipowasili kwa ziara ya kazi, Machi 29, 2019. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya,
Mhandisi Mwanaasha Tumbo.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili-kulia) akimpa
mkono wa pongezi mkazi wa kijiji cha Mamboleo-Nkumba, wilayani Muheza, Musa
Rajabu, baada ya kumuwashia rasmi umeme katika nyumba yake, Machi 29, 2019
akiwa katika ziara ya kazi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi
Mwanaasha Tumbo na wa pili-kushoto ni Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na
wananchi wa kijiji cha Mamboleo-Lusanga, wilayani Muheza, kabla ya kuwasha
rasmi umeme katika kijiji hicho, Machi 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto)
akiwaonesha wananchi wa kijiji cha Mamboleo-Lusanga, wilayani Lushoto, kifaa
cha Umeme Tayari (UMETA) na kuwaeleza matumizi pamoja na faida zake, akiwa katika ziara ya kazi Machi 29, 2019. Naibu
Waziri aliwasha rasmi umeme katika kijiji hicho.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwa ameshika taa ya
Chemli na Kibatari, alizokabidhiwa na mkazi wa kijiji cha Misongeni wilayani
Muheza (kulia kwa Naibu Waziri); baada ya kumuwashia rasmi umeme katika nyumba
yake, Machi 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.
No comments:
Post a Comment