Kuongezeka wa idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa vipimo na uzibuaji wa
mishipa ya damu ya moyo ambayo imeziba kupitia mtambo wa Cathlab ni
ishara kuwa watu wengi wanahitaji kupata huduma hiyo.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akisoma ripoti ya utendaji
kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba
kwa bodi ya Wadhamini.
Prof. Janabi alisema tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2016 hadi
2018 katika mtambo wa Cathlab wameona zaidi ya wagonjwa 2389 ambao
waliwafanyiwa vipimo na kuwazibua mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa
imeziba.
“Kupitia mtambo huu tunafanya upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua
kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja. Kwa mwaka jana pekee
tulifanya upasuaji kwa wagonjwa 1056 na kuvunja rekodi katika nchi za
Afrika Mashariki na Kati”, alisema Prof. Janabi.
Alisema hivi sasa madaktari wa magonjwa ya moyo kwa watoto kupitia
mtambo huo wa Cathlab wameanza kuziba matundu na kuzibua mishipa ya
damu iliyoziba.
“Kipindi cha nyuma watoto walikuwa wanafanyiwa upasuaji huu na madaktari
wageni hii ilitokana na kutokuwa na daktari wa kutoa huduma hiyo katika
Taasisi yetu. Mwaka jana daktari wetu mmoja aliyekuwa anasoma Afrika ya
Kusini amerudi baada ya kumaliza masomo yake na anafanya upasuaji siku
ya Jumatano”,.
“Tumetenga siku moja kwa wiki ambayo ni jumatano watoto wanafanyiwa
upasuaji wa kuziba matundu na kuzibua mishipa ya damu iliyoziba, uhitaji
ni mkubwa na mtambo uliopo ni mmoja. Kuna haja ya kuwa na mtambo
mwingine wa Cathlab ili wagonjwa wengi wenye uhitaji wa huduma hii
waweze kuipata”, alisema Prof. Janabi.
Katika hatua nyingine Prof. Janabi alisema mwezi wa sita mwaka huu
Madaktari Afrika kutoka nchini Marekani watakuja nchini kupanda mlima
Kilimanjaro kwa ajili ya kuchangia fedha za matibabu ya magonjwa ya moyo
kwa watoto.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Prof. William Mahalu
aliipongeza menejimenti na wafanyakazi wote wa Taasisi hiyo kwa kazi
nzuri wanayoifanya ya kutoa huduma ya matibabu ya magonjwa ya moyo.
Prof. Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na
mishipa ya damu alisema kufanya vizuri kwa mtambo wa Cathlab kunaonesha
kuwa watu wengi wanahitaji huduma hiyo na wao kama bodi wameona
kunahaja ya kuongeza mtambo wa pili wa Cathlab ili wagonjwa wengi wapate
huduma hiyo.
“Mmetuambia hivi karibuni mmesaini mkataba wa makubaliano ya kuletwa
kwa wagonjwa kutoka nchi ya Malawi na Visiwa vya Zanzibar kwa ajili ya
matibabu, hongereni sana. Endeleeni kufanya kazi kwa bidii na kujituma
ili watu wengi zaidi wafaidike na huduma mnayoitoa”, alisema Prof.
Mahalu.
Alisema miaka minne au mitano ijayo wataalamu kutoka nje ya nchi
wanaokuja kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo watakuja nchini
kujifunza kutoka kwa watanzania baada ya wao kuja kutoa msaada.
Prof. Mahalu alimalizia kwa kuwataka wataalamu wa magonjwa ya moyo
kufuatilia maendeleo ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo pindi
wanaporuhusiwa kurudi nyumbani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Prof. William Mahalu akizungumza jambo na wafanyakazi wa maabara
alipotembelea maabara hiyo kwa ajili ya kuangalia mashine mpya za
uchunguzi wa vipimo vya magonjwa ya moyo zilizofungwa. Watatu kulia
kutoka kwa Prof. Mahalu ni mjumbe wa bodi Dkt. Donan Mbando.
Watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa
wanacheza gemu kama walivyokutwa na mpiga picha wetu. Watoto wawili
kati yao wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na wawili
wanasubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Prof. William Mahalu na mjumbe wa bodi hiyo Dkt. Donan Mbando wakitoka
kuangalia wodi mpya ya watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo imejengwa na
kufanyiwa ukarabati.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Prof. William Mahalu na mjumbe wa bodi hiyo Dkt. Donan Mbando
wakiangalia chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU)
kilichopo katika wodi mpya ya watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo
imejengwa na kufanyiwa ukarabati. Chumba hicho kikianza kufanya kazi
kitakuwa na vitanda nane na kuweza kurahisisha kutoa huduma kwa watoto
wanaohitaji matibabu ya dharula.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Prof. William Mahalu akiangalia (medical gas bed head panel) mahali pa
kuchomeka mashine ya kutolewa hewa ya matibabu kwenda kwa mgonjwa
katika wodi mpya ya kulipia ya watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo
imejengwa na kufanyiwa ukarabati.
Picha na JKCI
No comments:
Post a Comment