Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini
Bw.Biswalo Mganga akisoma moja ya nakala ya mashtaka wakati akizungumzia
malalamiko ya Musa Adam Sadiki ya kubambikiziwa kesi ya mauaji katika mahakama
ya Tabora. Kulia kwake ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw.Edson Makallo
na Kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari-MAELEZO Bi.Zamaradi
Kawawa.
.......................................
BARUA ya
wazi aliyoandikiwa Rais Dk. John Magufuli kupitia gazetini na mwananchi
aliyebambikiziwa kesi ya mauaji imewezesha kuachiwa huru kwa mwananchi huyo
huku Rais akiagiza hatua zaidi zichukuliwe kwa waliohusika kwenye tukio hilo
linaloichafua serikali.
Mwananchi
huyo Mussa Sadiki, aliandika barua ya wazi kwa rais Machi sita mwaka huu,
akilalamikia kubambikiziwa kesi ya mauaji namba 8/2018 katika Mahakama ya
Tabora baada ya kukamatwa na polisi ambapo baada ya rais kuisoma aliiagiza
Ofisi ya Mwendesha Mashataka Mkuu wa Serikali, kuchunguza swala hilo ili kubaini ukweli.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Mwendesha Mashataka Mkuu wa Serikali
(DPP), Biswalo Mganga, amesema kuwa baada ya mwananchi huyo kukamatwa,
polisi walimnyang’anya sh. 778,000, simu ya mkononi na mali alizokuwa amenunua
kwa ajili ya wakulima wakati akienda kwenye manunuzi.
“Kwa mujibu
ya malalamiko yake aliyoyaandika gazetini, baada ya kukamatwa aliwekwa kwenye
Kituo cha Polisi Tabora Mjini na kubambikizwa kesi ya kuvunja na kuiba ambapo
alikaa kituoni kwa muda wa juma moja na alipopelekwa mahakamani alisomewa
shtaka la mauaji,” alieleza.
DPP
amefafanua kuwa, baada ya Rais Dk. Magufuli kusoma barua hiyo, aliagiza
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ifuatilie malalamiko ya mwananchi huyo haraka ili
kujua ukweli.
Aidha
amesema kuwa Ofisi ya DPP ilifuatilia suala hilo kwa kufanya mahojiano na
mlalamikaji pamoja na kupitia nyaraka zilizopo katika kituo cha Polisi Tabora
Mjini zinazohusiana na sakata hilo.
“Katika
kufuatilia malalamiko hayo, ofisi ya DPP imebaini malalamiko hayo ni ya kweli.
Hii ni kwa sababu kitabu cha kuzuia wahalifu (detention register) kilichopo
katika kituo hicho cha polisi, kinaonyesha kuwa mwananchi huyo alikamatwa Juni
21 mwaka jana kwa kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba na aliingizwa mahabusu
ya polisi saa tisa alasiri.
Hata hivyo
amaesema kuwa kitabu hicho kinaonyesha kuwa Juni 29 mwaka jana,
mlalamikaji alitolewa mahabusu saa mbili asubuhi na kupelekwa mahakamani.
Mwendesha
Mashtaka Mkuu alieleza kuwa, tarehe hiyo hiyo mwananchi huyo
alifunguliwa kesi ya mauaji namba 8/2018 ikionyesha Mei sita mwaka jana katika
barabara ya Kazima Tabora Mjini, alimuua Jackson Thomas.
Ameeleza
kuwa wakati wa kufuatilia malalamiko hayo, ofisi ya DPP ilibaini Julai mosi
mwaka jana, alikamatwa Edward Matiku kwa makosa ya kuvunja nyumba usiku na
kuiba lakini Julai 16 mwaka jana, naye aliunganishwa katika shauri la mauaji
namba 8/2018 kuhusika na mauaji ya Jackson Thomas.
“Baada ya
kuyabaini hayo, Machi nane mwaka huu, niliwafutia washtakiwa wote wawili
mashtaka hayo na mahakama ikawaachia huru.
DPP
ameeleza kuwa baada ya Rais Dk. Magufuli kupokea ukweli wa malalamiko hayo na
hatua zilizochukuliwa, anampongeza Mussa Sadiki kwa ujasiri aliouonyesha kwa
kuweka wazi malalamiko yake.
Aidha
amesema kuwa Rais anavishauri vyombo vingine vya habari kuchunguza na
kuchapisha habari zenye ukweli kwa kuzingatia maslahi ya taifa.
“Mheshimiwa
Rais ameagiza hatua zaidi zichukuliwe kwa wote waliohusika na tukio hilo kwa
lengo la kukomesha tabia kama hizo zinazoichafua serikali kwa wananchi wake na
dunia nzima,” amesisitiza
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini
Bw.Biswalo Mganga akisikiliza maswali kutoka kwa waandishi wa habari (hawapo
pichani) wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari juu ya malalamiko ya
Musa Adam Sadiki ya kubambikiziwa kesi ya mauaji katika mahakama ya
Tabora. Kulia kwake ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw.Edson Makallo na
Kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari-MAELEZO Bi.Zamaradi
Kawawa.
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw.Biswalo Mganga
akizungumza na waandishi wa habari juu ya malalamiko ya Musa Adam Sadiki ya
kubambikiziwa kesi ya mauaji katika mahakama ya Tabora.Kulia kwake ni
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw.Edson Makallo na Kushoto kwake ni
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari-MAELEZO Bi.Zamaradi Kawawa.
No comments:
Post a Comment