Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
akizungumza wakati wa hafla ya uwashaji rasmi wa umeme katika kijiji cha
Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 27,
2019.
Mbunge wa Jimbo la Mtama,
Nape Nnauye akizungumza, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu (mwenye kilemba cha njano – meza kuu) kijijini Ntauna, Kata ya Rondo,
Lindi Vijijini, Februari 27, 2019. Naibu Waziri aliwasha rasmi umeme kijijini
hapo.
...................................
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka watanzania kuondoa shaka kuhusu
mipango ya serikali kufuatia gesi iliyogunduliwa mikoa ya kusini, kwani
haijabadilika na inaendelea kutekelezwa.
Aliyasema
hayo jana Februari 27, 2019 kijijini Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini,
alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku nne mkoani Lindi ambapo alikagua
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, kuwasha umeme katika vijiji
mbalimbali na kuzungumza na wananchi.
“Nataka
niwaaminishe wana-kusini, yale ambayo serikali iliahidi baada ya kugundua gesi,
mipango yake iko palepale na inafanyiwa kazi,” alisema.
Akifafanua
zaidi, Naibu Waziri Mgalu alisema moja ya mambo ambayo serikali iliahidi ni
umeme wa uhakika utakaowezesha uwekezaji.
Alisema
hadi sasa, taratibu za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa gesi
Mtwara wenye megawati 300 na Somanga Fungu wenye megawati 330 ziko katika hatua
za mwisho.
“Mradi
utaanza ndani ya mwaka huu wa fedha ambao utawezesha mikoa hii kuzalisha umeme
wa kutosha kuweza kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.”
Aidha,
aliongeza kuwa, jambo jingine kubwa ni kuviwezesha viwanda vya maeneo husika
kupata umeme wa gesi ambapo alisema tayari kiwanda cha saruji cha Dangote
kimeshaunganishiwa.
Pia,
alisema, serikali inaendelea kuzungumza na viwanda vya mbolea ili vizalishe
mbolea inayotokana na gesi ili pamoja na mambo mengine viongeze ajira kwa
wananchi.
Vilevile,
alisema kwa Mkoa wa Lindi, eneo la Likongo, serikali inatarajia kujenga kiwanda
cha kusindika gesi iwe katika hali ya kimiminika ambapo Rais John Magufuli
ametoa mwongozo wa kufanya mazungumzo na mbia mmoja mmoja. Alisema mazungumzo
yanaendelea vizuri.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri alizungumzia tathmini ya ziara yake mkoani Lindi,
ambapo alisema imekuwa yenye mafanikio.
Alisema,
kazi ya kuwaunganishia wananchi umeme vijijini inaendelea na ametoa wito kwa
mkandarasi husika kuboresha utendaji wake ili kuhakikisha anafikia malengo ya
kukamilisha kazi yote kwa mujibu wa mkataba ifikapo Juni 30, mwaka huu ambapo
ndipo mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza utakuwa
unahitimishwa.
Naibu
Waziri alisema yeyé pamoja na viongozi wengine wa Lindi akiwemo Mkuu wa Mkoa,
Wakuu wa Wilaya na Wabunge wamekubaliana kumsimamia mkandarasi husika katika
kuhakikisha anatimiza wajibu wake ipasavyo.
Kwa upande
wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, ambaye alifuatana na Waziri
wakati akihitimisha ziara yake, aliwahakikishia wananchi wa eneo husika kuwa yeyé
pamoja na viongozi wenzake watamsimamia mkandarasi husika ili kuhakikisha kazi
inatekelezwa kwa ufanisi.
“Tumekabidhiwa
hawa tuwasimamie, kwa hiyo nichukue nafasi hii kuwathibitishia kwamba
tutawasimamia kwelikweli ili kuhakikisha zoezi hili linakamilika vizuri sana,”
alisisitiza.
Naye Mbunge
wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa
upande wa nishati ambapo alisema imekuwa ikifanya kazi nzuri sana.
“Tunawashukuru
sana Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kama kuna Wizara inafanya
vizuri, basi Wizara hii inafanya vizuri.”
Hata hivyo,
Nnape alisema anatambua kiu kubwa ya umeme waliyonayo wananchi na kuwasihi kuwa
wastahimilivu maana zoezi la kuunganisha umeme ni hatua kwa hatua, awamu kwa
awamu. Alisema anayo imani kubwa kwamba vijiji vyote vitafikiwa na huduma hiyo
kabla ya mradi kuisha.
Mkurugenzi
wa kampuni ya State Grid, ambayo ndiyo inatekeleza uunganishaji wa umeme mkoani
Lindi, Charles Mlawa, akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo,
aliahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri katika
kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi.
Katika
ziara hiyo, viongozi wa ngazi mbalimbali walipongeza utendaji kazi wa Wizara
pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuomba jitihada zinazofanyika
ziendelee.
Katika
Miradi ya Umeme Vijijini, Mzunguko wa Kwanza (REA III – 1), jumla ya vijiji
takribani 133 vitaunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi bilioni 31.9.
Matarajio ni kuwaunganishia wananchi takribani 5,337.
Akiwa Lindi
vijijini, Naibu Waziri aliwasha umeme katika vijiji vya Ntauna, Mvuleni na
Tulieni.
No comments:
Post a Comment