Tuesday, March 12, 2019

KILIMO CHA MUHOGO KUKOMBOA WAKULIMA BAGAMOYO

 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Issa (kushoto) Makamo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Saidi Ngatipula (katikati) na kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Dar Canton Investment Company Limited,John Vedasto Rwehumbiza.
 
Mkurugenzi wa Kampuni ya Dar Canton Investment Company Limited,John Vedasto Rwehumbiza, akizungumza katika kikao cha Baraza la madiwani Halmashauri ya Bagamoyo.
.................................... 

 
Wakulima Wilayani Bagamoyo wamehimizwa kuongeza uzalishaji wa zao la Muhogo, kwani zao hilo kwa sasa, ni zao maalumu la kibiashara.





Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Ally Ally Issa katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.



Mwenyekiti Ally Ally Issa ambaye pia ni diwani wa Kata ya Fukayosi ameeleza kupitia mkutano huo wa baraza la madiwani kuwa, zao la Muhogo ndani ya Halmashauri ya Bagamoyo sasa ni zao la biashara na ukombozi kwa Wakulima wa Bagamoyo.



Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ameyasema hayo baada ya kuikaribisha kampuni ya Dar Canton Investment Limited ambayo ni kampuni ya Uwekezaji katika zao la muhogo inayotarajiwa kuanza kufanya kazi ndani ya Halmashauri ikijikita katika ununuzi na uchakataji wa muhogo.


“Waheshimiwa Madiwani wenzangu twende tukawahimize Wananchi kujikita katika uzalishaji wa zao la muhogo bora, Wataalamu mtusaidie kufika Vijijini kuwaelimisha Wananchi juu ya kutumia mbegu bora za muhogo na kulima kilimo kinachozingatia kanuni bora za kilimo.



Alisema kulima kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo kutapelekea wakulima wapate tija katika mazao yao, na kunufaika na ujio wa mwekezaji huyo aliye tayari kununua muhogo kwa Wananchi kuanzia sasa.



Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa kampuni ya Dar Canton Investment Limited, John Vedasto Rwehumbiza, alisema kampuni imepata eneo lililopo Kata ya Makurunge, katika Kitongoji cha Kifude ambapo imeshaanza kufanya upembuzi yakinifu ili kuanza ujenzi wa kiwanda cha uchakataji wa muhogo.



Alisema kwa sasa kampuni inaendelea kununua muhogo mkavu katika maeneo mbali mbali ndani ya Halmashauri na kiwanda kitakua na uwezo wa kununua tani 120 za muhogo kwa siku mara kitakapoanza uzalishaji wake, na kuongeza kuwa kwa sasa tayari wameanza ununuzi wa muhogo kwa wakulima mbalimbali ndani na nje ya Halmashauri hiyo.



Rwehumbiza, alisema wananchi wa wilaya ya Bagamoyo wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo ya kilimo cha muhogo kwani soko la uhakika lipo kupitia kampuni yao.


No comments:

Post a Comment