Waziri wa Maliasili na Utalii
Dkt. Hamisi Kigwangala akisisitiza jambo wakati akizungumza na Watumishi
wa Wizara hiyo kuhusu umuhimu wa kutekeleza maagizo kwa wakati yanayotolewa na
Viongozi wa Wizara hiyo katika kikao cha Baraza la 26 la Wafanyakazi wa
Wizara hiyo kilichofanyika leo Jijini Mwanza.
............................
Waziri wa
Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangala amewataka Watanzania
kuondokana na dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa watumishi wa Wizara hiyo
hususan wahifadhi wa wanyamapori na Misitu ni watu
katili wanaowatesa Wananchi.
Kauli hiyo
ameitoa leo wakati akifungua mkutano wa 26 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara
hiyo uliofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza.
Amesema
watumishi hao ni watu wenye utu na weledi wa hali ya juu na wanaozingatia
sheria katika kutimiza majukumu yao na hulazimika kutumia nguvu wakati
wakipambana na majangili wanaokutwa katika maeneo ya hifadhi wakifanya vitendo
vya ujangili.
‘’ Ulinzi
wa Rasilimali za nchi ni jukumu letu sote, wizara imepewa dhamana ya kusimamia
na kuongoza kwa niaba ya watanzania, kama kuna watumishi wa Wizara hii
wanaowanyanyasa wananchi naomba walete ushahidi kwetu ili tuwachukulie hatua’’
amesema Dkt. Kigwangala.
Waziri
Kigwangala amesikitishwa na idadi ya watumishi walipoteza maisha kwa ajali na
wengine kuuwawa na majangili wakati wakipambana nao katika maeneo yote ya
hifadhi nchini na kutoa wito kwa wananchi wote wenye taarifa au ushahidi
juu ya vitendo vyovyote vya kihalifu kuziwasilisha katika mamlaka zinazohusika.
Amesema
kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo
vya ujangili na uhalifu katika maeneo ya hifadhi na wale wote wanaoshirikiana
na makundi ya watu wenye nia ovu ya kukwamisha juhudi za uhifadhi wa rasilimali
za Taifa.
Ametoa wito
kwa wananchi kuheshimu sheria za uhifadhi na kuepuka kuvamia maeneo ya hifadhi
kwa shughuli za kijamii na ufugaji akitoa wito kwa viongozi mbalimbali wa Siasa
kuunga mkono juhudi za wizara za ulinzi wa maeneo ya hifadhi kwa kuwaelimisha
wananchi wanaowaongoza kujiepusha na vitendo vya uvamizi wa maeneo ya hifadhi
badala ya kuwatetea.
Kwa upande
wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof.Adolf Mkenda
akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho amesema kuwa jumla ya watumishi
23 walifariki dunia wakati wakitekeleza majukumu ya uhifadhi
na 5 walijeruhiwa na majangili wakiwa kazini.
Prof.
Mkenda amesema kuwa waliofanya vitendo hivyo hawaitakii mema Tanzania na
ni maadui wa shughuli za uhifadhi nchini akiongeza kuwa Serikali itaendelea
kusimama na kuwatetea watumishi na askari wa wanyamapori wanaotimiza majukumu
yao kwa kuzingatia sheria.
Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii Mhe,Constantine Kanyasu akizungumza na Watumishj wa
Wizara hiyo katika kikao cha Baraza la 26 la Wafanyakazi
kilichofanyika leo Jijini Mwanza.
Waziri wa Maliasili na
Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri wa Wizara, Mhe, Constantine
Kanyasu wakiwa wameshikana na watumishi wengine hukuwakiimba wimbo wa
mshikamano Daima katika Kikao cha Baraza la 26 la Wafanyakazi kilichofanyika
leo jijini Mwanza.
Waziri wa Maliasili na
Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Wizara
hiyo, Mhe. Constantine Kanyasu wakati akikagua gwaride la Jeshi Usu katika Chuo
cha Usimamizi wa Wanyamapori Pasiansi.
No comments:
Post a Comment