Na
Omary Mngindo, Mlandizi - Machi 30
MOTO
mkubwa umezuka katika Kituo kidogo cha kupozea umeme cha Kanda ya Mlandizi
Kibaha Mkoa wa Pwani, ulioanza kuwaka saa moja asubuhi ya leo Machi 30, 2019.
Moto
huo ulioleta taharuki kubwa kwa wananchi waishio jirani kabisa na mtambo huo,
umezuka ghafla saa moja asubuhi, na kusababisha watu kukimbia kutoka kwenye
nyunba zao kwa kuhofia usalama wao.
Mitambo
hiyo iliyopo jirani na mashine za Maji Mlandizi, pia eneo hilo kuna uwanja wa
Mpira wa Miguu Maarufu uwanja wa DAWASA, ambapo kwa muda huo vijana walikuwa
wanafanya mazoezi hivyo kulazimika kukimbia kuhofia usalama wao.
Baadhi
ya vijana waliokuwa wanacheza mpira katika uwanja huo uliopo mita chache na
kituo hicho, walisema kwamba walisikia muungurumo mkubwa kutoka ndani ya uzio
kabla ya kuona moto mkubwa ukianza kuwaka.
"Tulifika
hapa saa 12 asubuhi kama kawaida yetu kwa ajili ya kufanya mazoezi, ghafla
tukasikia muungurumo mkubwa unaotokea kwenye uzio wa Tanesco kabla ya kuanza
kuripuka moto mkubwa," alisema Juma Ramadhani.
Aliongeza
kwamba ghafla hali ilibadilika kutokana na moto mkali ukiambatana na moshi
mzito uliotanda angani huku watu wakitaharuki wengine wakitoka katika nyumba zao
wakikimbia kwa kuhofia usalama wao.
"Leo
nimeona kwanini Tanesco imepiga marufuku watu kujenga jirani na miundombinu
yao, kwa moto huu kama kungekuwa na nyunba jirani sana na ulipo moto, mji wa
Mlandizi ungeteketea, ni moto mkali sana," alisema.
Nae
mkazi aliyejitambulisha kwa jina la Mariamu Hussein alisema kuwa yeye anaishi
mbali na kituo hicho cha kupozea umeme lakini aliona moshi mkubwa angani ndipo
alipokimbilia ili nae ajionee hali ilivyokuwa.
"Nikiwa
nyumbani nimeshuhudia moshi mwingi mzito angani, nikaona nije kujionea
kilichotokea nimekuta moto na moshi mzito, nimeamini miundombinu ya Tanesco
inapaswa kuachwa mita nyingi na makazi ya watu," alisema Mariamu.
Mkazi
mwingine dereva wa bodaboda ambaye hakupenda kutaja jina lake alisema kuwa,
katika eneo la Mlandizi kuna baadhi ya transfoma zimekuwa zimesababisha
miripuko ya mara kwa mara, lakini wahusika wanashindwa kuzibadilisha hivyo
miripuko hujirudiarudia.
"Katika
maeneo yetu kuna siku mbili tumekosa umeme lakini hakuna taarifa zilizotolewa
na viongozi wa Tanesco, tunawaomba wafanye juhudi za kuzibadilisha baadhi ya
Transfoma ambazo wanaona zimechoka, zinaweza kugharimu maisha ya watu,"
alisikika dereva huyo.
Juhudi za kuuzima moto huo zilifanyika ambapo Jeshi la zimamoto na uokoaji limefanikiwa kuuzima bila ya kuleta madhara makubwa.
Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika
Hata hivyo juhudi za mwandishi wetu kumpata msemaji wa Tanesco kuzungumzia ni hasara kiasi gani imepatikana hazikufanikiwa.
Kikosi cha Jeshi la zimamoto na uokoaji wakiendelea kuudhibiti moto huo uliotokea mapema hii leo Machi 30, 2019. katika Kituo kidogo cha kupozea umeme cha Kanda ya Mlandizi Kibaha Mkoa wa Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akishuhudia hali ilivyokuwa mara baada ya moto kuzimwa.
No comments:
Post a Comment