Wednesday, March 6, 2019

TAWA YASITISHA KIBALI CHA KUWINDA KAMPUNI YA GREEN MILES SAFARIS

Mwandishi wetu,Arusha

Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori nchini(TAWA),imejipanga kuendelea kuboresha sekta ya uwindaji wa kitalii na imesitisha kibali cha uwindaji wa kitalii cha kampuni ya Green Miles Safaris Ltd, kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya umiliki wa vitalu vya uwindaji.

Naibu Kamishna wa Utalii na Biashara wa TAWA, Imani Nkuwi alisema kampuni hiyo, imeshindwa kulipa ada za kutotumia zaidi ya asilimia 40 ya mgao wa kuwinda katika vitalu.

“kampuni hii tumeinyia huduma za kuwinda katika vitalu vyake vyote wakati suala lao likifanyiwa kazi”alisema.

Kampuni hiyo, inamiliki vitalu wilayani Longido na katika pori la akiba la Selous na katika siku za karibuni, imekuwa na migogoro na vijiji ilipowekeza wilayani Longido.

Hata hivyo, Nkuwi alisema bado wamiliki wengi wa vitalu wanazingatia sheria na taratibu zilizowekwa na serikali, ikiwepo kutunza vitalu vyao, kuzuia matukio ya ujangili na kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe ametoa agizo , kukamatwa mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Green Miles Salim Abdalah Awadhi, kutokana na kushindwa kulipa deni hilo la vijiji na halmashauri ya Longido mkoa wa Arusha.

Mwaisumbe alisema vijiji 23 vya wilaya hiyo, vinaidai kampuni hiyo, kiasi cha sh 329 milioni kutokana na makubaliano walioingia tangu mwaka 2017/18 na jitihada za malipo zimekwama kwa njia ya mazungumzo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Longido, Wakili Jumaa Mhina, alisema ofisini yake imekuwa ikiitaka kampuni hiyo kuwa na mahusiano na vijiji na kulipa fedha za vijiji na halmashauri bila ya mafanikio.

Hata hivyo,Mkurugenzi wa Green Miles Safari Ltd, Salim Abdalah Awadhi ambaye yupo nje ya nchi , amekuwa akikanusha tuhuma mbali mbali dhidi ya kampuni yake,ikiwepo kudaiwa na vijiji fedha .

No comments:

Post a Comment