Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola (kulia)
akiangalia zoezi la upimaji wa kilevi kwa dereva wa basi la Kimbinyiko, Omary
Sauli (katikati). Dereva huyo hakuwa na kilevi chochote na aliruhusiwa aendelee
na safari yake
..........................................
Na Felix Mwagara, MOHA, Morogoro.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi
Lugola amefanya operesheni kubwa ya kukagua na kupima ulevi wa pombe kwa
madeveva wa mabasi na malori mjini Morogoro, leo.
Lugola pia alizungumza na abiria wa
mabasi hayo, pamoja na viongozi wa madereva waliopo stendi kuu ya mabasi
Msamvu, mjini humo, ambapo walimwelezea kero mbalimbali zinazowakabili.
Ukaguzi wa mabasi na malori hayo
ulifanyika barabara kuu itokayo Dodoma kuja Morogoro-Dar es Salaam ambapo Waziri
huyo akiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo (RPC), Mkuu wa Kikosi cha Usalama
Barabarani Mkoa huo (RTO), alisimamisha vyombo hivyo vya moto vilivyokuwa
vinaingia Mizani iliyopo eneo la Kihonda, nje kidogo ya Mji wa Morogoro.
Akizungumza na madereva, kondakta,
wapiga debe na abiria mara baada ya kufanya ukaguzi huo, Lugola alisema ni
wajibu wake kufanya hivyo katika hatua ya kupunguza kwa kasi ajali mbalimbali
zinatokana kwa uzembe wa madereva nchini.
“Mimi ni Waziri wa vitendo, nikiagiza
nataka nitekelezwe, na pia nikiahidi lazima nilifuatilie, niliwaambia nitakua
nakuja kufanya ukaguzi muda wowote ambao hamuujui, na ninafanya hivi kwa lengo
moja tu, kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa ikiwa ni hatua ya
kumaliza kupunguza au kumaliza kabisa ajali za barabarani hapa nchini,” alisema
Lugola.
Aliongeza kuwa, kwasasa ajali
zimepungua nchini, hasa Mkoa wa Morogoro, kwasababu ya askari wa usalama
barabarani kufanya kazi zao kiweledi, na pia madereva kufuata sheria za usalama
barabarani.
Lugola aliwataka madereva nchini,
kuacha uendeshaji wa mashindano, kuwa na leseni na pia kuhakikisha wanapokuwa
barabarani wanakua makini kwasababu ya kuwabeba abiria au mizigo mbalimbali
wanayoisafirisha sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi.
“Madereva wa mabasi na malori ambao
nimefanikiwa kuwapima kilevi leo, ambao wasiopungua sita, sijawakuta na kilevi,
wapo makini na hii inaleta nguvu na imani kuwa madereva wanaelewa na kuzingatia
sheria za usalama barabarani, na pia ndani ya mabasi niliyokuwa nayakagua nimezungumza
na abiria wakaniambia madereva wanaendesha vizuri na pia niliwakuta wamevaa
mikanda, naamini safari yetu ya kuondoa ajali za barabarani tunazidi
kufanikiwa,” alisema Lugola.
Wakizungumza kwa wakati tofauti
katika stendi kuu ya mabasi, madereva walilipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa
Morogoro, kwa usimamizi mzuri ambao umewaunganisha na kuwafanya waifurahie kazi
wanayoifanya.
Dereva Juma Rashidi wa basi
linalosafiri kutoka Ifakara kuja Morogoro, alisema wanajisikia furaha kubwa kwa
uongozi mpya wa Jeshi la Polisi ulioletwa Mkoani Morogoro hivi karibuni.
“Naomba niseme ukweli, RPC na RTO
hakika wanatuongoza vizuri, hakuna kero za ajabu kama zamani, tupo huru kufanya
kazi zetu, hii inaonyesha viongozi hawa wanataka tufanye kazi ili tuweze kupata
riziki zetu kwa njia halali bila usumbufu wa kusumbuana kama ulivyokuwa siku za
nyuma,” alisema Rashidi.
Lugola alifanya ziara katika kituo
hicho, na baadaye kutoka nje ya kituo hicho kuyakagua mabasi na malori, mara
baada ya kumaliza ziara yake aliyoifanya Wilayani Kilosa ya kutatua migogoro ya
ardhi ya wananchi wa Tarafa ya Kimamba wilayani humo, juzi.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola
akiwauliza maswali abiria wa basi la Kimbinyiko kuhusiana na mwendokasi wa
dereva wa basi hilo, na pia kuwapa elimu kuhusiana na kujua haki zao wanapokuwa
safarini. Abiria hao walimweleza Waziri huyo dereva huyo yupo makini na pia
walimshukuru kwa kufanya ukaguzi kwa mabasi mbalimbali nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akitoka
ndani ya basi la Kimbinyiko kufanya ukaguzi na kuzungumza na abiria wa basi
hilo, mjini Morogoro, leo. Abiria hao walimweleza Waziri huyo dereva huyo wa
basi hilo yupo makini na pia walimshukuru kwa kufanya ukaguzi kwa mabasi
mbalimbali nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola (wapili kulia)
akiwa ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu, mjini Morogoro, wakati
alipokuwa anafanya ukaguzi na kupima kilevi kwa madereva wa mabasi kituoni hapo
pamoja na wa malori katika barabara ya Morogoro-Dodoma. Kulia ni Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola
(kushoto) akizungumza na madereva wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu, Mjini
Morogoro, leo, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kituo hapo kwa ajili ya
kukagua na kupima kilevi kwa madereva wa mabasi kituoni hapo. Pia Lugola
aliwapima madereva wa malori barabara kuu ya Morogoro Dodoma. Wapili kushoto ni
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa. Picha na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
No comments:
Post a Comment