Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisema jambo na wadau wa
biashara ya kemikali (hawapo pichani) kwenye mkutano na wafanya biashara za
kemikali nchini.
..............................
Serikali itaendelea kusimamia na
kudhibiti matumizi ya kemikali ili kuhakikisha hazileti madhara kwa afya za
wananchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo alipokuwa
kwenye mkutano na wadau wa kemikali kujadili namna ya kuboresha mazingira ya
kufanya biashara ya kemikali nchini.
“Kemikali zisipodhibitiwa vizuri
zinaweza kuleta madhara katika afya, mazingira pamoja na kuhatarisha usalama wa
nchini, ipo haja ya kuweka mazingira mazuri ya kusimamia na kudhibiti uingizaji
na matumizi ya kemikali nchini ili zisilete madhara” amesema Waziri Ummy.
Hata hivyo takwimu za Shirika la Afya
Duniani (WHO) mwaka 2014 zinaonyesha vifo milioni 12.6 vilitokana na mazingira
duni ya kuishi, mojawapo ya kichocheo ni athari za kemikali ambazo zimekuwa
zikisababisha magonjwa na vifo.
Waziri Ummy amesema kuwa kemikali
zimekuwa na athari kubwa kwa binadamu kwa kusababisha magonjwa zaidi ya 100
huku akiyataja magonjwa ya moyo, saratani, ngozi, athari katika mifumo ya
fahamu, upumaji pamoja na chakula kuathiri zaidi wananchi wengi.
“Tukubali kuwa kemikali zina madhara
kwa wananchi lakini sasa tuwe na mazingira mazuri ya kuzidhibiti” amesema
Waziri Ummy na kuendelea kusema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira
mazuri kwa wafanya biashara ya kemikali nchini.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy
amezitaka Taasisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA)
pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kuangalia upya tozo
wanazotoza kwa wafanyabiashara za kemikali nchini pamoja na kupunguza urasimu
usiokuwa na ulazima ili kuwawekea mazingira rafiki wafanya biashara za
kemikali.
“Msiwe ni kikwazo kwa uwekezaji na
biashara, kikwazo cha kushamiri na kukua kwa uwekezaji nchini, nataka muwe
mawakala wa kukuza biashara na uchumi nchini” amesema Waziri Ummy.
Awali akisoma taarifa yake Mkemia
Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amesema Sheria ya Kemikali ya mwaka
2003 imekuwa na mchango mkubwa katika udhibiti wa matumizi ya kemikali nchini.
“Kabla ya kutungwa kwa sheria hii,
kemikali zilikuwa zikiingizwa nchini kiholela na kutumika bila ya kuwa na
ufatiliaji au udhibiti wowote” alisema Dkt. Mafumiko.
Dkt. Mafumiko amesema Sheria ya
kemikali imewawezesha kudhibiti usafirishaji, utumiaji pamoja uteketezaji wa
taka zinazotokana na kemikali.
“Ofisi ya Mkemia inasimamia kwa
ukaribu matumizi ya kemikali zote zinazoingizwa nchini kuanzia zinapoingia,
mahali zinapokwenda pamoja na matumizi yaliyokusudiwa” alisema Dkt. Mafumiko.
Naye Katibu Mkuu wa Mawakala wa
Forodha Tanzania Mhandisi Anthony Swai amesema tozo zimekuwa nyingi kiasi cha
kuwaumiza wafanyabiashara wa kemikali huku urasimu pia ukisababisha
wafanyabiashara kutumia muda mwingi kufuatilia vibali vya uingiza wa kemikali
nchini.
Aidha Mhandisi Swai ameiomba Serikali
kuainisha mipaka ya taasisi za umma pamoja na tozo wanatostahili kulipa kwani
kumekuwa na mwingiliano wa majumuku baina ya taasisi za Serikali ambazo
amezijata kuwa ni GCLA, TDFA na TBS (Shirika la Viwango Tanzania)
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Prof Esther Hellen Jason akisema jambo na
wadau wanaojihusiha na biashara ya kemikali (hawapo pichani) katika mkutano na
wadau wanaojihusisha na biashara ya kemikali.
Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt.
Fidelice Mafumiko akisema jambo kwa wadau wa biashara ya kemikali nchini
(hawapo pichani) katika mkutano na wadau wanaojihusisha na biashara ya kemikali
nchini.
Mdau wa bishara ya kemikalina
Katibu Mkuu wa Mawakala wa Forodha Tanzania Mhandisi Anthony Swai akiwa amebeba
sampuli ya kemikali mapema leo kwenye kikao cha wadau wanaojihusisha na bishara
ya kemikali nchini.
Wadau wanaojihusisha na
biashara ya kemikali wakiwa kwenye mkutano uliotishwa na Ofisi ya Mamlaka ya
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kujadili namna bora ya kuboresha biashara ya
kemikali nchini.
No comments:
Post a Comment