Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Bagamoyo
limetoa maagizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kumaliza mgogoro wa
ardhi kata ya Kisutu pamoja na kutafuta eneo la kujenga shule kitongoji cha
Sanzale kata ya Magomeni.
Maagizo hayo yametolewa jana Machi 05, 2019 katika
kikao cha robo ya pili ambapo madiwani waliwasilisha taarifa za utekelezaji za
kata zao.
Diwani wa kata ya Kisutu, Aweso Mwidini amesema
kuna mgogoro wa muda mrefu kwenye kata yake ambapo idara ya ardhi imepima
viwanja kwenye eneo la barabara na kusababisha mgogoro baina ya wananchi
wengine na mmiliki wa viwanja hivyo.
Alisema amefanya juhudi za kukutana na mmiliki wa
viwanja hivyo ambapo mmiliki huyo wa viwanja ambae ni mtumishi wa Serikali aliyekuwa Bagamoyo na sasa amehamishiwa Halmashauri ya Mkuranga, alisema aliuziwa mpaka eneo la barabara na kwamba hawezi kuachia
barabara kwakuwa ni mali yake.
Diwani huyo alisema alifanya juhudi ya kumtafuta
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo ambapo Mkurugenzi alifika eneo la tukio lakini majibu
ya kuridhisha hayajapatikana.
Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Bagamoyo, Ally Ally Issa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Bagamoyo kushughulikia swala hilo haraka iwezekanavyo.
Alisema
barabara hiyo ndiyo inayotumika kufika shule ya Sekondari kingani pamoja na
wananchi wengine wakazi eneo hilo hivyo Mkurugenzi atafute namna ya kutatua
mgogoro huo ili barabara ibaki kama kawaida.
Katika hatua nyingine Diwani wa kata ya Magomeni Mwanaharusi Jarufu, amesema kitongoji
cha Sanzale kilichopo kata ya Magomeni kinakabiliwa na ukosefu wa shule ya
msingi hali inayopelekea watoto kutembea umbali mrefu kufuata shule.
Aidha, ametaka hatua za makusudi zichukuliwe ili
wananchi wa eneo la sanzale wapatiwe eneo la kujenga shule.
Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Bagamoyo Ally Ally Issa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo
kutafuta eneo katika kitongoji cha Sanzale kwaajili ya ujenzi wa shule.
Mwenyekiti huyo alisema yapo maeneo makubwa
katika kitongoji hicho ambayo mpaka sasa hayajaendelezwa hivyo ofisi ya
Mkurugenzi ifanye haraka kupitia maeneo hayo na kujua wamiliki wake ili yule
ambae hawezi kuendeleza eneo hilo lichukuliwe kwa maslahi ya wananchi.
Diwani wa kata ya Magomeni Mwanaharusi Jarufu, akiwasilisha taarifa za kata.
No comments:
Post a Comment