Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista
Mhagama akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wanakikundi cha Rasupashoma Group,
Bw. Ibrahim Malabela jinsi wanavyotengeneza viatu bora na vyenye kudumu kwa
muda mrefu. (Mwenye miwani ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali (Mst.),
Nicodemus Mwangela na (Kulia) ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Bw. James
Kajugusi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza
na vijana wanaopata mafunzo ya kilimo bora na ufugaji wa kisasa katika kituo
cha Maendeleo ya Vijana – Sasanda kilichopo Kata ya Nyimbili, Mkoani Songwe
alipofanya ziara kukagua maendeleo na miradi ya vijana katika kituo hicho.
...........................
Na; OWM
(KVAU) – SONGWE
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa
zilizopo kwenye maeneo yao kwa kuanzisha vijiwe vya kiuchumi.
Kauli hiyo
ameitoa na Waziri Mhagama wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo na
miradi ya vijana iliyopo katika Kituo cha Maendeleo ya Vijana, Sasanda
kilichopo Kata ya Nyimbili, Mkoani Songwe.
Akiwa
katika ziara hiyo Mhe. Mhagama alieleza kuwa, Serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeendelea kutimiza
azima yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, hivyo vijana watumie fursa hiyo
kujifunza mambo muhimu na kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawafanya
wabadilishe vijiwe wanavyokaa kuwa vya kiuchumi.
“Tunataka
kuona vijana watakapo jifunza kilimo bora, ufugaji wa ng’ombe au nyuki wataweza
kuboresha thamani mazao na bidhaa kwa kuanzisha viwanda vidogo ndani ya Mkoa wa
Songwe, mkakati wetu katika kituo hiki ni kutoa mafunzo yatakayowawezesha
vijana kuongeza thamani ya mazao na bidhaa watakazozalisha ambazo zitakuwa ni
kichocheo muhimu katika kufikia maendeleo yao” alisema Mhagama
Aliongeza
kuwa, Takribani vijana 500 kwenye kituo hicho wamejifunza stadi za maisha,
ufundi na elimu mbalimbali zinazotolewa kwenye kituo ambazo zitawawezesha
kujipatia kipato.
Sambamba na
hilo, Mhe. Mhagama aliwahimiza Viongozi wa Mkoa kushirikiana na Ofisi yake ili
waweze kuwasaidia vijana ambao wamekwisha anzisha viwanda vidogo vidogo ndani
ya mkoa huo kwa kuwawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuwatafutia soko la
uhakika ndani na nje ya nchi.
Aidha,
Waziri Mhagama alitoa rai kwa vijana kujiunga kwenye vikundi ambavyo ni
endelevu na vyenye muelekeo wa kuanzisha viwanda vidogo
vitakavyowawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao na pelekea kufikia uchumi
wa kati kama mpango wa maendeleo wa taifa unavyoelekeza.
Pia,
aliwaelezea juu ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo zitafanyika
katika Mkoa huo na kuwataka vijana na wanawake kutumia fursa hiyo kuutangaza
vyema mkoa wa Songwe.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi alieleza kuwa kituo
cha Maendeleo ya Vijana cha Sasanda kimewawezesha vijana kujitambua na
kujiwekea malengo ya maisha na kuyatekeleza kwa faida yao, jamii na taifa kwa
ujumla.
“Tunatarajia
kuanzisha mafunzo na programu zitakazowaelekeza vijana masuala ya kilimo
biashara ambacho kitasaidia upatikanaji wa malighafi zitakazokuwa zinahitajika
kwenye viwanda vilivyopo nchini,” alisema Kajugusi
Naye Bw.
Silia Kibona ambaye ni mnufaika kupitia kituo hicho, aliishukuru Serikali kwa
kuwajengea mazingira ya kujifunzia ambayo yamewasaidia kupata mafunzo muhimu na
aliwahamasisha vijana wenzie kuhudhuria mafunzo yanayotolewa kwenye kituo
hicho.
Kituo cha
Maendeleo ya Vijana – Sasanda kilianzishwa mwaka 1979 kwa ushirikiano wa
Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni wa Taifa, Vijana na Michezo iliyopo wakati
huo pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Uanzishaji wa Kituo hicho
ulifuatia kuanzishwa kwa mpango wa kuunda vikundi vya vijana vya uzalishaji
mali, uliolenga kuwawezesha vijana wasio na ajira kuweza kujiunga na kufanya
kazi za kujitegemea hasa katika sekta ya kilimo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza
na vijana walionufaika kupitia kituo cha maendelo ya vijana, Sasanda
alipotembelea kuona mradi walioanzisha katika Kata ya Nyimbili. (Wenye miwani)
ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali (Mst.), Nicodemus Mwangela.
No comments:
Post a Comment