AFISA
Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Valintine Mbai ambaye ni
Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu wa Halmashauri hiyo
ametakiwa kuacha tabia ya
kutumia cheo chake kuomba rushwa ya ngono kwa Watendaji wa Vijiji
katika Halmashauri hiyo na kubadili mwenendo wake haraka iwezekanavyo.
Onyo hilo limetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa wakati wa kikao kazi na watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Akizungumza na watumishi hao, Mary amesema, ni aibu kwa afisa
huyo mwenye dhamana ya kusimamia maadili ya kiutumishi kutumia madaraka yake
vibaya kwa kuomba rushwa ya ngono toka kwa Watendaji wa Vijiji jambo ambalo ni
kinyume cha maadili ya kiutendaji katika utumishi wa umma.
Amemtaka afisa huyo kuacha tabia hiyo na kujirekebisha maramoja ili awe
mfano bora kwa watumishi anaowasimamia kimaadili.
Pia amemtaka, afisa huyo kuwa na heshima kwa wakuu wake wa kazi akiwemo
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ili kutengeneza mazingira mazuri ya
kiutendaji.
Aidha, Mary ametoa angalizo kwa Mwenyekiti wa Halmashauri
hiyo, Juma Abeid kutowatetea watumishi wasio waadilifu na badala yake awachukulie
hatua za kinidhamu hata kama ni marafiki zake.
Mary Mwanjelwa ameendelea kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi
wa umma nchini akiwa wilayani Mkuranga na kutoa wito kwa watumishi wote wa umma
kuhakikisha wazingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji Kazi katika Utumishi wa
Umma.
No comments:
Post a Comment