Monday, February 4, 2019

WAKULIMA WA PAMBA WATARAJIE MABADILIKO MAKUBWA- WAZIRI HASUNGA.

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Katikati) akiongoza kikao kazi cha Wabunge wa maeneo yanayolima pamba nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo Jijini, Dodoma leo Jumatatu tarehe 4 Februari, 2019. Wengine pichani ni Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Kulia) na Naibu waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumbwa. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
.................................... 


Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga amewaambia Waheshimiwa Wabunge wa maeneo yanayolima pamba kuwa Wizara ya Kilimo imedhamiria kumkomboa Mkulima wa pamba na kwa kuanza imeanzisha zoezi la kuwasajili Wakulima wote nchini wakiwemo Wakulima wa pamba ambapo Serikali imetengeneza mfumo maalumu wa kuwatambua kwanza Wakulima, maeneo wanayotoka, mashamba yao yapo wapi na yana ukubwa gani.


Mhe. Hasunga ameyasema hayo wakati wa kikao maalumu na Waheshimiwa Wabunge hao katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo Jijini, Dodoma leo Jumatatu tarehe 4 Februari, 2019.


Kikao hicho kilikuwa na lengo la kufanya maboresho kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa mauzo ya pamba ambao unatarajia kuanza Mwezi Aprili mwaka huu.


Mhe. Hasunga amesema moja ya mambo ambayo Wizara ya Kilimo itahakikisha inayashughulikia ipasavyo, sambamba na kuwatambua Wakulima wa pamba ni pamoja na kuupitia upya mfumo wa Ushirika katika ununuzi wa pamba, mfumo wa uagizaji na uingizaji wa viuatilifu vya pamba pamoja na masoko ya zao hilo.


Waziri Hasunga amesema katika kipindi hiki kifupi amekuwa akipata malalamiko mengi kutoka kwa Wakulima wa mazao mbalimbali kuhusu udhaifu wa mfumo wa uagizaji wa uingizaji wa pembejeo za kilimo yakiwemo madawa na mbegu hafifu.


“Napenda nikiri kuwa tuna tatizo katika mfumo wa uagizaji na uingizaji wa pembejeo za kilimo, bado haujakaa vizuri lakini baya zaidi ni viuatilifu hafifu. Serikali kamwe haiwezi kutazama Wakulima wakionewa na Wajanja wachache na huu ni uhujumu uchumi lazima wanaofanya mambo haya wachukuliwe hatua kali za kisheria”. Amekaririwa Waziri Hasunga.


Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya Wabunge wameshauri kuwa muda wa kupeleka pembejeo za kilimo kama mbegu bora na madawa uwe mapema zaidi kuliko ilivyo sasa. Mhe. Kiswaga Boniventura. 


Mbunge wa Magu ameishauri Serikali kuwa wakati wa zoezi la ununuzi wa pamba ghafi zoezi hilo liendane na zoezi la kuwapelekea Wakulima mbegu bora za pamba na kuongeza kuwa litaokoa fedha za Umma kwa kuwa fedha za usafirishaji itatumika mara moja tu.


Naye Mbunge wa Itilima Mhe. Njalu Silanga amesema kuna haja kubwa ya kupitia mfumo mzima wa Vyama vya Ushirika vinavyonunua pamba, akitoa mfano katika msimu wa pamba uliopita wa mwaka 2018/2019 Wakulima wa pamba walikuwa wakikatwa shilingi 100 katika kila kilo moja kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa viuatilifu (Madawa ya pamba) katika msimu ujao wa kilimo.


Mhe. Njalu amesema kuna maeneo mengi ambayo Wakulima wengi wanafikisha zaidi ya kilo mia tano (500) na anapokatwa kiasi hicho cha fedha makusanyo yanakuwa makubwa hadi kufikia shilingi elfu hamsini (50,000/=) wakati thamani halisi ya pembejeo ambazo atapewa na Chama chake cha Ushirika hakizidi shilingi elfu kumi (10,000/=).


Mhe. Waziri Hasunga amekiri kuwa jambo hilo linaweza kuwepo na kuna haja ya kuufanya maboresho makubwa mfumo mzima ununuzi wa pamba kabla ya kuanza msimu mpya wa ununuzi wa pamba ambao unataraji kuanza mapema Mwezi Aprili, 2019

No comments:

Post a Comment