Tuesday, February 12, 2019

HAKUNA VIBALI VYA KUAGIZA SUKARI KWA WAZALISHAJI WA NDANI- WAZIRI HASUNGWA.

 Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano na Wadau wa Sekta Binafsi uliofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House Jijini Dar es salaam, Leo Tarehe 12 Februari 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

 Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba (Mb) akizungumza wakati wa mkutano na Wadau wa Sekta Binafsi uliofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House Jijini Dar es salaam, Leo Tarehe 12 Februari 2019.
.........................................


Serikali imesema kuanzia sasa haitatoa vibali vya uagizaji sukari nje ya nchi kwa wazalishaji wa sukari badala yake serikali itatafuta utaratibu mwingine wa kuagiza.

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 12 februari 2019 wakati akifungua mkutano na Wadau wa Sekta Binafsi ambapo lengo lilikuwa ni kubadilishana uzoefu, kupata maoni yao namna bora ya kuongeza mahusiano pamoja na utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP II) ambayo inatekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali na Sekta Binafsi.

Waziri Hasunga imewataka wazalishaji hao wa sukari nchini kuja na mkakati wa namna gani wataongeza uzalishaji ili Tanzania iondoke na hitaji la kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi.

Waziri Hasunga amesema kwa kuwapa vibali vya kuagiza nje wazalishaji wa ndani hawataongeza uzalishaji ili waendelee kuagiza nje kwa kuwa sukari ya kutoka nje ni bei nafuu.

“Wazalishaji wa ndani ndio hao hao wanapewa vibali vya kuagiza, umewahi sikia wapi? Wataongeza ukweli kasi ya uzalishaji? Na Mimi niwaambie kabisa hilo hapa kwangu halipo kabisa kama ni kuagiza nitaagiza mimi,” alisema Waziri Hasunga.

Amesema mahitaji la sukari kwa mwaka ni Tani 670,000 wakati inayozalishwa na viwanda vya ndani Tani 320,000 na kuwaagiza Wazalishaji hao badala ya kutafuta vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi waje na mkakati wa kuboresha zaidi uhitaji uliopo kwani Tanzania ina ardhi nzuri pamoja na mashamba ya kutosha.

“Kama kuna Wafanyabiashara ambao walikuwa wanasubiri baada ya kikao hiki waje kuomba vibali wasahau kabisa, kwangu halipo badala yake nina mkakati wa kuboresha uzalishaji ili tusiagize tena nje,” alisema Waziri Hasunga.

Amesema kuwa anataka kuhakikisha ndani ya miaka mitatu Tanzania haitaagiza sukari nje tena kwa kujitosheleza kwa kilimo cha miwa na kukaribisha wawekezaji kujenga viwanda vya kutengeneza sukari, “kama tutakunywa kwa chumvi sawa, hapo ndio tutafanya bidii.”

Waziri Hasunga amesema hayuko tayari kuondoshwa kazini kwa utoaji wa vibali vya sukari kwa Wafanyabiashara wanaoagiza nje ya nchi kwani anaamini kuwa uwezo wa kuzalishwa hapa nchini upo. Waziri huyo alisema serikali inatoa fedha nyingi kuagiza bidhaa za chakula kutoka nje.

Alisema kwa mwaka zaidi ya Shilingi Bilioni 400 zinatumika kuagiza mafuta nje ya nchi wakati kuna uwezo wa kulima mazao mbalimbali yanayozalisha mafuta ikiwa ni pamoja na michikichi.

“Mimi naamini katika nchi zilizobarikiwa na kupendelewa ni pamoja na Tanzania, ardhi yenye rutuba, mito mingi na mbuga za wanyama lakini watu hawalimi kilimo cha umwagiliaji,” alisema.

Ameitaka Sekta Binafsi kuhakikisha kunakuwa na mashamba makubwa ambayo yatazalisha mazao yanayohitajika kwa viwanda na pia mazao ya chakula.

Waziri Hasunga amewataka Wadau wa Sekta Binafsi kutumia kikao hicho kutoa maoni, mapendekezo yenye muelekeo wa kutatua changamoto katika Sekta ya Kilimo ambapo anategemea maboresho hayo yataleta mabadiliko makubwa katika mfumo mzima wa

pembejeo za kilimo, masoko, uzalishaji wenye tija na utungwaji wa sheria ya kilimo.
 
 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akizungumza wakati wa mkutano na Wadau wa Sekta Binafsi uliofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House Jijini Dar es salaam, Leo Tarehe 12 Februari 2019.

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano na Wadau wa Sekta Binafsi uliofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House Jijini Dar es salaam, Leo Tarehe 12 Februari 2019.

 Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano na Wadau wa Sekta Binafsi mara baada ya kufungua mkutano huo  uliofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House Jijini Dar es salaam, Leo Tarehe 12 Februari 2019.

No comments:

Post a Comment