Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha na Halmashauri ya Wilaya
ya Kibaha, wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao chenye
lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao, kabla kukagua
utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hizo mkoani Pwani.
............................
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amempa onyo kali Afisa Utumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kibaha, Bi. Ruth Mwelo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utawala na
Rasilimaliwatu wa Halmashauri hiyo kwa kumtolea lugha chafu mstaafu
aliyekuwa akidai haki yake na kumtaka afisa huyo ajirekebishe haraka
iwezekanavyo.
Onyo hilo
amelitoa wilayani Kibaha, wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya
Mji wa Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha chenye lengo la kuhimiza
uwajibikaji, kabla ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
katika wilaya hizo ili kujiridhisha na utekelezaji wake.
Mhe. Dkt.
Mwanjelwa amesema, haiwezekani afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia Sheria,
Kanuni na Taratibu za kiutumishi ndio awe kikwazo cha utendaji kazi katika
Halmashauri hiyo kwa kutoa lugha chafu dhidi ya wanaofuta huduma ofisini kwake,
na kuongeza kuwa, afisa huyo ndiye anayestahili kuwa kwenye Kamati ya Maadili
ili kutoa miongozo ya uadilifu na kusimamia maadili ya watumishi kwa ujumla
katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Mhe. Dkt.
Mwanjelwa amemtaka afisa huyo kutotumia cheo chake vibaya na badala yake
asimamie vema nidhamu na masilahi ya watumishi wa umma.
Sanjari na
hilo, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amemtaka afisa huyo kuacha tabia ya kutoa siri za
ofisi na kutokuwa mchonganishi miongoni mwa watumishi wenzie kwani matendo hayo
hayapaswi kufanywa na mtumishi yeyote nchini.
Aidha, Mhe.
Dkt. Mwanjelwa amesema ameamua kuweka bayana mapungufu ya afisa huyo
mbele ya watumishi wenzie ili ajifunze kutokana na matendo yake yasiyoridhisha
na aweze kubadili mwenendo wake mbaya wa kimaadili.
Mhe. Dkt.
Mary Mwanjelwa (Mb) ameendelea kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma
nchini, kwa kutoa onyo kwa watumishi wote wanaobainika kukiuka Kanuni za
Maadili ya Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma.
Katibu Tawala Mkoa wa Pwani,
Bi. Theresia Mbando akitoa neno la utangulizi kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha na
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na
watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao,
kabla kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hizo mkoani
Pwani.
Baadhi ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Mji Kibaha na
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani), wakati wa kikao kazi cha watumishi hao
na Naibu Waziri huyo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi
hao, kabla ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri
hizo mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment