Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
(kushoto) akiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Regina Chonjo,
wakati akikagua ujenzi wa Soko la Kisasa la Kimkakati la Manispaa ya
Morogoro, ambalo ndilo la mfano katika miradi ya kuziwezesha Mamlaka za
Serikali za Mitaa kujitegemea kimapato.
Muonekano wa Soko la Kisasa la Kimkakati la Manispaa ya
Morogoro, ambalo limekamilika kwa asilimia 30 na linatarajiwa
kukabidhiwa kwa Serikali Septemba mwaka huu na kuhudumia wafanyabiashara
zaidi ya 900.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa nne kushoto) akietendelea na ukaguzi wa
ujenzi wa Soko la Kisasa la Kimkakati la Manispaa ya Morogoro Mkoani
Morogoro .
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)
………………………..
Na Peter Haule, WFM, Morogoro
Halmashauri zote nchini zimetakiwa
kujifunza kutekeleza miradi ya Kimakakati inayopatiwa ruzuku na
Serikali, katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kuwa thamani
halisi ya mradi wa Soko la kisasa utakaogharimu Sh. bilioni 17 hadi
kukamilika kwake inaonekana.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, alipofanya ziara ya kikazi ya
kutembelea na kukagua mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Soko la Kisasa
katika Manispaa ya Morogoro Mkoani Morogoro wenye lengo la kuzifanya
Mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze kujitegemea kimapato.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Kama ipo
halmashauri iliyopewa fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati kwa
kuwekeana mkataba na Serikali na bado inashindwa kufuata makubaliano ya
mkataba ijifunze kutoka Manispaa ya Morogoro.
“Ukilinganisha na miradi mingine
ya kimkakati niliyoikagua katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, huu ni
wa mfano, zipo halmashauri ambazo zimepewa fedha halafu zinarudi tena
kuangalia upya mikataba ambayo waliwekeana saini na Serikali jambo
ambalo linatia mashaka, tuje tujifunze kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya
Morogoro kwa nini ameweza kwenda na wakati ulio katika mkataba”alisema
Dkt. Kijaji.
Alipongeza hatua iliyofikiwa
katika utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia asilimia 30 japo
walitakiwa kufikia asilimia 40 katika kipindi hiki kutokana na
changamoto ya kujaa maji na kuutaka uongozi wa Manispaa hiyo kukamilisha
ujenzi ndani ya kipindi cha miezi mitano ili wafanyabiashara waanze
kulitumia soko hilo.
“Mapato ya Soko hili yataongezeka
kutoka Shilingi bilioni moja, kwa mwaka hadi Sh. bilioni 4 kwa kuwa
idadi ya wafanyabiashara itaongezeka kutoka 400 kwa sasa hadi 900 na
huduma zingine zitatolewa kama Benki” alieleza Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji alisema kuwa dhamira
ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ya kuanzisha miradi ya
kimkakati kwa manufaa ya watanzania itatimia kupitia mradi wa Soko la
Kisasa la Manispaa ya Morogoro.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi.
Regina Chonjo, ameishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo Wilayani
kwake, kwa kuwa soko lililokuwepo lilijengwa mwaka 1953 hivyo kuwa na
miundombinu mibovu iliyosababisha wananchi kuwa na magonjwa ya mlipuko
kikiwemo kipindupindu, hivyo mradi huo si tu utaongeza mapato na kuweka
mandhari nzuri, lakini pia utaimarisha afya za wananchi.
Naye Meya ya Manispaa ya
Morogoro Bw. Pascal Kihanga, alisema kuwa waliwaahidi wananachi
kusimamia ujenzi wa Soko hilo jambo ambalo linatekelezwa kwa juhudi
kubwa, hivyo kufikia mwezi Septemba mwaka huu mradi utakabidhiwa kwa
Serikali na wafanyabiashara wote walioondolewa kupisha mradi na wengine
watarudi.
Mhandisi wa Mradi huo Antonio
Mkinga, amesema kuwa mradi huo utakamilika katika muda uliopangwa, kwa
kuwa mpaka sasa hakuna vikwazo ambavyo vinaweza kuzuia utekelezaji wake.
Halmashauri ya Manispaa ya
Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri 17 zilizokidhi vigezo vya
kutekeleza jumla ya miradi 22 ya kimkakati nchini kwa mwaka wa fedha
2018/2019 kwa gharama ya shilingi bilioni 147 ambapo Manispaa hiyo
ilipata mradi huo wa soko la kisasa litakalogharimu shilingi bilioni 17.
No comments:
Post a Comment