Saturday, February 23, 2019

MICHEZO NI MUHIMU KWA USTAWI WA AFYA-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Shule ya Sekondari ya  St. Pamachiwa  Inclusive wilayani Hai, Februari 22, 2019. Kulia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Isaac Amani na wa pili kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
...........................


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wanafunzi wanatakiwa washiriki katika michezo mbalimbali kwa sababu ina umuhimu mkubwa kwa ustawi wa afya ya binadamu pamoja na maendeleo ya nchi. 

Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Februari 22, 2019) wakati akizindua shule ya Sekondari Jumuishi ya Mtakatifu Amachius Inclusive katika wilaya ya Hai, Kilimanjaro. Amezindua shule hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.

“Lakini katika dunia ya leo michezo ni ajira na chanzo kikubwa cha mapato kwa vijana na Taifa kwa ujumla. Kwa kifupi michezo ni moja ya sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa, hivyo wazazi waruhusuni watoto washiriki.” 

Alisema kutokana na umuhimu wa michezo, Serikali imetenga vipindi kwa ajili ya elimu ya michezo katika ratiba za masomo na kuendesha mashindano ya michezo shuleni yaani UMITASHUMTA na UMISSETA. 

Waziri Mkuu alisema kuna wakati baadhi ya shule hususani za binafsi, dini na mashirika zimekuwa hazioni umuhimu wa kuwa na vipindi hivi au kushiriki katika mashindano. 

“Hivyo, taasisi zetu zizingatie kuwashirikisha wanafunzi katika programu za ufundishaji michezo na kushiriki mashindano ili waweze kujenga afya ya mwili na akili, kukuza amani, ushirikiano, upendo na mshikamano kati ya yao.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuutaka uongozi wa shule ya Sekondari Jumuishi ya Mtakatifu Amachius Inclusive kuwa na walimu watakaofundisha vipindi vya michezo pamoja na kuwawezesha wanafunzi wao kushiriki mashindano ya michezo.

No comments:

Post a Comment