WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka
vijana mkoani Kigoma waanzishe mashamba ya michikichi kwa kuwa zao hilo
litawapatia kipato cha uhakika.
Amesema Serikari imedhamiria
kufufua zao la michikichi ili kuliwezesha Taifa kujitosheleza kwenye mafuta ya
kula na kuokoa fedha za kigeni.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu,
Februari 18, 2019) alipowasalimia wananchi wa kijiji cha Nyakitondo wilayani
Kasulu akiwa njiani kwenda Kibondo.
Waziri Mkuu ambaye yupo mkoani
Kigoma kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kufufua kilimo cha michikichi amesema
ni vema wananchi wakachangamkia fursa hiyo.
“Vijana limeni michikichi kwani
ukipanda ukiwa darasa la tano baada ya miaka mitatu utaanza kuvuna na kujipatia
kipato ambacho kitakuwezesha kujikimu.”
Amesema kilimo cha zao la
michikichi kitawawezesha wananchi hususani vijana kupata mitaji ya uhakika kwa
ajili ya shughuli zingine za kiuchumi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema
Serikali imejipanga kuhakikisha Tanzania inaongoza kwa kilimo cha zao la
michikichi katika nchi za Afrika Mashariki.
Kadhalika, Waziri Mkuu
amewahamasisha wananchi hao wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili wawe
na uhakika wa matibabu kwa yao na familia zao.
Wakati huohuo Waziri Mkuu
ametembelea kambi ya Wakimbizi ya Nduta wilayani Kibondo na kukagua shule ya
msingi Kassim Majaliwa na baadae wodi ya wazazi katika Hospitali Nduta.
No comments:
Post a Comment