Monday, February 4, 2019

MIL. 800 ZABORESHA ZAHANATI MKAMBA NA KISIJU WILAYA YA MKURANGA.




Na Omary Mngindo, Mkuranga

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, imeishukuru Serikali kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa kuipatia shilingi milioni 800, zinazokarabati Zahanati za Mkamba na Kisiju wilayani hapa.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mhandisi Mshamu Munde, ameyaeleza hayo Jumapili ya Feb 3 alipokuwa anazungumza mbele ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, kwenye sherehe za miaka 42 ya kuzaliwa kwa chama hicho.

Mbele ya Mwenyekiti wa chama hicho Ramadhani Maneno, Katibu Anastasia Amas, Mkuu wa Mkoa Mhandis Evatist Ndikilo, Waziri wa TAMISEMI Suleiman Jafo na Manaibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu na wa Mifugo Alhaj Abdallah Ulega, Munde alisema kuwa ujenzi unaendelea vizuri.

"Pamoja na juhudi hizo za Serikali Kuu, hospitali yetu inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo kuelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaokuja kutoka maeneo mbalimbali, huku bajeti yetu ikiwa tofauti na ongezeko hilo, hatua inayolalamikiwa na wananchi" alisema Mhandisi Munde.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo wananchi wamekuwa wakitoa malalamiko ya upungufu wa dawa, hatua ambayo halmashauri haina namna juu ya malalamiko hayo, huku akipongeza wana-CCM hao kwenda kutembelea hospitalini halo na kifanya usafi.

Mganga Mkuu halmashauri ya Mkuranga Stephano Mwandambo alisema kuwa wanakabiliwa na upungufu wa damu, huku akiomba wananchi wajitokeze kuchangia ili kuokoa wagonjwa wanaohitajo huduma hiyo.

"Tuna mahitaji makubwa ya damu, hospitali yetu inahitaji damu lakini iliyopo haikidhi kuwahudumia wanaohitaji, tunawaomba wananchi kutoka maeneo mbalimbali wafike kusaidia kuchangia damu," alimalizia Dkt. Mwandambo.



No comments:

Post a Comment