Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisisitiza jambo leo wakati akiongea na
Waandishi wa Habari katika siku ya Saratani Duniani, iliyofanyika katika Ukumbi
wa Idara ya Habari Bunge jijini Dodoma.
..................................
Na WAMJW – DOM
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amewatoa hofu Wananchi kwa kusisitiza
kuwa chanjo ya kuwakinga wasichana na Saratani ya Mlango wa kizazi haihusiani
na uzazi wa mpango wala kumzuia msichana kuja kupata uja uzito baadae.
Ameyasema hayo leo wakati akiongea na
Waandishi wa Habari katika siku ya Saratani Duniani, iliyofanyika katika Ukumbi
wa Idara ya Habari Bunge jijini Dodoma, huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni
“NITAFANYA JITIHADA ZOTE KUPUNGUZA JANGA LA SARATANI DUNIANI”.
Waziri Ummy amesema kuwa Chanjo ya
Mlango wa kizazi ni salama na imethibitishwa na Shirima la Afya Duniani
kwaajili yakuwakinga Wasichana dhidi ya maambulizi ya Saratani ya Mlango wa
kizazi.
” Chanjo ya kuwakinga wasichana na
saratani ya mlango wa kizazi haihusiani na uzazi wa mpango, ni chanjo ambayo
imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani kwaajili yakuwakinga wasichana dhidi
ya maambukizi ya Saratani ya mlango wa Kizazi” Alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa katika kila
wagonjwa wa Saratani 100, takribani wagonjwa 31 ni wanawake wa Saratani ya
Mlango wa kizazi, hivyo amewahasa wazazi na walezi nchini kuhakikisha wasichana
wanaostahili kupata chanjo hii, wanaipata bila vikwazo vyovyote ili kutokomeza
kabisa Saratani hii nchini.
“Katika kila wagonjwa wa Saratani
100, Wagonjwa takribani 31 ni wanawake wa Saratani hii ya Mlango wa kizazi,
kwahiyo hatuna haja ya kuiogopa chanjo hii kwasababu ndio itayowakinga watoto
wetu na maambukizi ya Saratani ya mlango wa kizazi” alisema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa kwa
mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC), zinaonyesha
kwamba kwa Tanzania kunatokea mgonjwa 1 wa Saratani kwa kila watu 1000, hivyo
Tanzania inakua na wagonjwa wapya wa Saratani 55,000 kwa mwaka na takribani
wagonjwa 28,610 hufariki kwa mwaka, ambapo ni vifo asilimia 52 ya wagonjwa
wapya.
Aliendelea kusema kuwa Taarifa kutoka
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonesha kwamba kumekuwa na ongezeko la
wagonjwa wa Saratani mwaka hadi mwaka, huku akisema kuwa Mwaka 2015 wagonjwa
wapya 5,764, huku mwaka 2016 wagonjwa wapya 6,338, na mwaka 2017 wagonjwa wapya
7,091, pia mwaka 2018 wagonjwa wapya 7,649.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy
amedai kuwa Serikali imeanzisha huduma kwenye vituo 624 vilivyopo katika
Halmashauri mbalimbali nchini ambapo jumla ya wanawake 375,522 walifanyiwa
uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti mnamo mwaka
2017, ukilinganisha na wanawake 416,841 waliofanyiwa uchunguzi huo mwaka 2018.
Kati ya hao, wanawake 16,147 waligundulika kuwa na mabadiliko ya awali mwaka
2017, na wanawake 18,341 mwaka 2018.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiteta jambo na Mkurugenzi wa Ubora kutoka
Wizara ya Afya Dkt. Mohammed Mohammed ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara
ya Afya.
Mkurugenzi wa Ubora ambaye alimwakilisha Katibu
Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mohammed Mohammed akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi wa
Tiba Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe leo katika tamko la siku ya Saratani
Duniani lililofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari Bunge jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Ubora kutoka Wizara ya Afya Dkt.
Mohammed Mohammed. ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya leo katika
tamko la siku ya Saratani Duniani lililofanyika katika ukumbi wa Idara ya
Habari Bunge jijini Dodoma.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza kwa makini
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu
wakati akitoa tamko la siku ya Saratani Duniani, leo jijini Dodoma
No comments:
Post a Comment