Na Omary Mngindo, Kibaha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa
Pwani, kimempongeza Mbunge wa Viti Maalumu Zaynabu Matitu Vulu, kwa kuuliza
swali kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Mafia Mbaraka Dau, kuhusiana na adha ya
usafiri visiwani humo.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama
hicho Taifa (MNEC) Haji Abuu Jumaa, akizungumza na Waandishi wa habari mjini
Kibaha, alisema hatua ya Vulu kusimama bungeni kuulizia mipango ya serikali juu
ya usafiri kwa wana-Mafia, inaonesha ni namna gani wabunge mkoani humo
walivyokuwa na ushirikiano.
"Mwishoni kwa wiki Pwani
tulisherehekea madhimisho ya miaka 42 tangu kuzaliwa kwa chama chetu, baadhi ya
wabunge na Mawaziri walihudhulia, wengine waliendelea na majukumu ya Bunge, katika
kikao hicho Vulu aliuliza swali kwa niaba ya Mbaraka Dau, lililohusu usafiri
wilayani Mafia" alisema Haji.
MNEC huyo alisema kuwa swali hilo
lililoulizwa bungeni, limehusiana na changamoto ya usafiri na usafirishaji,
linalowakabili wana-Mafia na Mkoa kwa ujumla wanaokwenda na kurudi kutoka
visiwani humo, ambao wamekuwa na adha hiyo kwa muda mrefu.
Nae Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi
Mkoa Jackson Josian alieleza kwamba, kama Jumuia imefurahishwa kwa hatua hiyo,
huku akieleza inatokana na mahusiano mazuri yaliyopo kwa wabunge mkoani humo.
"Hii inaonesha ni namna gani
wabunge wetu wanavyoshirikiana katika kuwakilisha matatizo ya wapigakura wetu,
niwaombe utaratibu huu uwe endelevu, kwani wote ni wawakilishi wa wananchi
kutokea katika chama kimoja cha CCM," alisema Josian.
Jumanne Feb 5 Vulu alimwakilisha Dau
wa Mafia, kuiuliza Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano,
juu ya mipango wa kupeleka ndege visiwani humo, sanjali kuongeza ukubwa wa
kiwanja cha ndege sanjali na kuimarisha usafiri wa majini.
Akizungumza kwa njia ya simu na
Mwandishi wa Habari hizi kutokea mjini Dodoma, Vulu alisema swali lake la
msingi kwa Wizara hiyo ni kutaka kufahamu hatua za serikali katika kuimarisha
sekta ya usafiri na usafirishaji visiwani humo, ambao kwa muda mrefu
wanakabilia na adha hiyo.
No comments:
Post a Comment