Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof.
Palamagamba Kabudi akihutubia Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la
Umoja wa Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi.
..................................
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof.
Palamagamba Kabudi amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekeleza
wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu na ustawi wa jamii kama
kipaumbele chake na itaendelea kushirikiana na Baraza hilo kuhakikisha
haki za binadamu nchini na duniani kote zinadumishwa.
Prof. Kabudi amesema hayo
alipolihutubia Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa
kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi.
Prof. Kabudi amesema Serikali ya
Tanzania imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha haki za binadamu, utawala
bora na utii wa sheria nchini na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu
wenye ulemavu.
“Serikali imelenga kuimarisha haki za
binadamu, utawala bora, utii wa sheria na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake,
watoto na watu wenye ulemavu, kwa sasa tunatekeleza mpango mkakati wa kitaifa
wa kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/18 – 2021/22,
lengo likiwa ni kulinda na kudumisha haki za wanawake, watoto na watu wenye
ulemavu,” alisema Prof. Kabudi.
Amesema Serikali pia inazingatia
suala la kuwapatia haki kwa haraka wananchi wasio na uwezo kwa kutolea maamuzi
kwa haraka mashauri yanayowahusu watu wasio na uwezo na kuwapatia msaada wa
kisheria kupitia utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 ili
wananchi hao waweze kupata haki zao kwa wakati.
Aidha, Prof. Kabudi amelihakikishia
Baraza hilo kuwa Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari
nchini na imeendelea kuhakikisha uhuru wa vyombo hivyo unalindwa huku jumla ya
vituo vya redio 152, televisheni 34, magazeti 172 nchini kote
yamesajiliwa na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira stahiki
yatakayowezesha vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru.
Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria
kuleta ustawi wa jamii kwa kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo
ikiongozwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 na kunadi kuwa Tanzania
imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu, afya na maji
zinawafikia wananchi wote.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika
kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu, afya na maji zinawafikia wananchi wote
na kuongeza kuwa Serikali inatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 23 kwa mwezi kutoa
elimu pasipo malipo na hivyo kuongeza udahili wa watoto wanaojiunga darasa la
kwanza kwa asilimia 35.2 na asilimia 20.1 kwa wanaojiunga na kidato cha
kwanza,” alisema.
Prof. Kabudi pia amesema Serikali
imedhamiria kufikisha huduma za afya karibu na watanzania wote ambapo imeongeza
bajeti ya afya kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi Shilingi bilioni
269 mwaka 2017/2018 na kuongeza kuwa Serikali inatekeleza mikakati ya kujenga
vituo vya afya ambapo hadi sasa imejenga vituo 304, na nyumba za watumishi wa
afya 578 zimejengwa nchini kote.
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja
wa Mataifa ni chombo cha Umoja wa Mataifa chenye jukumu la kukuza na kulinda
haki za binadamu duniani kote na kushughulikia uvunjwaji wa haki za binadamu
unaotokea katika nchi wanachama wa umoja huo na kushauri hatua za kuchukuliwa
ili kuboresha haki za binadamu duniani.
Baraza hilo pamoja na mambo mengine
linatarajia kupokea taarifa mbalimbali kuhusu haki za binadamu duniani na kutoa
nafasi kwa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutoa maelezo yao
kuhusu utekeelezaji wa wajibu wao wa kulinda na kukuza haki za biandamu katika
nchi zao.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof.
Palamagamba Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maofisa wa
Tanzania mara baada ya kuhutubia kikao hicho cha Baraza la Haki za Binadamu
jijini Geneva Uswissi.
No comments:
Post a Comment