Monday, February 25, 2019

DOKTA MPANGO AZIONYA TAASISI ZA SERIKALI ZISIZOTUMIA MFUMO WA KIELETRONIKI KUKUSANYA MAPATO


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akitoa ufafanunuzi wa kero zilizowasilishwa na Wafanyabiashara wa Sekta mbalimbali wakati wa kikao na Wafanyabiashara hao, kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC mkoani Arusha. 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mrisho Gambo akiwakaribisha Waheshimiwa Mawaziri, Wakuu wa Taasisi za Serikali na Wafanyabiashara wa Sekta mbalimbali (hawapo pichani), waliohudhuria kikao kilicholenga kutatua kero mbalimbali zinazokwamisha biashara mkoani humo kilichofanyika Jijini Arusha.


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akisalimiana na Wenyeviti wa Taasisi Binafsi waliohudhuria mkutano uliowakutanisha Mawaziri mbalimbali, Wakuu wa Taasisi za Serikali na Wafanyabiashara uliolenga kukuza biashara mkoani humo, kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC mkoani Arusha. 

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akiorodhesha baadhi ya hoja zilizowasilishwa na Wafanyabiashara wa Sekta mbalimbali wakati wa kikao na Wafanyabiashara hao, kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC mkoani Arusha, Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angela Kairuki. 

Viongozi mbalimbali wakijadili jambo kabla ya kuanza kwa kikao kilichowajumuisha viongozi hao, Wakuu wa Taasisi za Serikali, Wafanyabiashara wa Sekta mbalimbali kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC mkoani Arusha. 

………………………………………………………………………….. 

Na Josephine Majura na Ramadhani Kissimba, WFM, Arusha 

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango amezitaka Taasisi zote za Serikali kutumia kikamilifu mfumo wa malipo wa Serikali wa kielektroniki (GePG), ili kutimiza azma ya Serikali ya kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za Umma. 

Dkt. Mpango ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kikao cha wafanyabiashara wa sekta ya madini, utalii, mahotel na viwanda wa Mkoa wa Arusha kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC). 

Akijibu hoja na kutolea ufafanunuzi wa kero mbalimbali zilizowasilishwa na Wafanyabiashara hao, Dkt. Mpango alisema Serikali ilishatoa maagizo kwa Taasisi zote za Serikali kuwa malipo yote yafanyike kwa kutumia mfumo wa malipo ya Serikali, na endapo itatokea Taasisi yoyote itashindwa kufanya hivyo itachukuliwa hatua za kisheria. 

“Serikali iliziagiza Taasisi zote kuanza kutumia mfumo wa malipo ya Serikali ifikapo mwezi Juni, 2019, na nina agiza kuanzia leo mwananchi yeyote asikubali kulipa malipo yoyote yasiyotumia mfumo huu” alisisitiza Dkt. Mpango. 

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angela Kairuki alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Sekta Binafsi katika kukuza uchumi wa nchi, hivyo Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba inaboresha mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini. 

Mkutano huo uliandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mrisho Gambo, kwa lengo la kutatua kero mbalimbali za Wafanyabiashara wa Mkoa huo, na kuhudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Joseph Kakunda, Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe. Kangi Lugola, Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais Mazingira Mhe. Januari Makamba, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Isack Kamwele, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu, na Naibu Waziri wa Vijana, Kazi na Ajira, Mhe.Anthony Mavunde.

No comments:

Post a Comment