Friday, February 22, 2019

BARAZA LA MADIWANI KISARAWE LAPITISHA BAJETI YA BILIONI 30 KWA MWAKA WA FEDHA WA 2019/2020

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Hamisi Dikupatile akizungumza na wajumbe wa kikao cha baraza la madiwani mara baada ya kupitisha makadirio ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa 2019 /2020 kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na matumizi mengine.
...............................

VICTOR MASANGU, KISARAWE

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kisarawe iliyopo Mkoa wa Pwani  imeazimia kwa pamoja  kupitisha makadirio ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa  2019 /2020 kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi  mbali mbali ya maendeleo pamoja na matumizi mengine.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Hamisi Dikupatile akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani la kupitisha bajeti ya mwaka 2019 /2020 amewataka watendaji wote kuachana  kabisa na tabia ya  uzembe na badala yake wahakikishe wanajikita zaidi katika kusimamia miradi ya maendeleo pamoja na kuongeza kasi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato kwa maslahi ya wananchi.

“Kwanza kabisa nipende kuwashukuru madiwani na watendaji wote ambao kwa namna moja au nyingine mmeweza kushirikiana kwa pamoja hadi kuweza kufanikisha mpango huu wa bajeti kwa hiyo kikubwa mimi ninachowaomba tuongeze kasi zaidi katika kukusanya mapato ya ndani ili tuweze kufikia malengo ambayo tumejiwekea,”alisema Dikupatile.

Aidha alisema kwamba lengo kubwa la halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ni kuweka mikakati madhubuti katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya nadani pamoja na kuibua miradi mingine mbali mbali ambayo itaweza kusaidia kwa kiasi kukubwa katika suala zima la kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wake Diwani wa wa kata ya Kibuta Mhandisi  Mohamed Kilumbi akizungumza kwa niaba ya wenzake amebainisha kuwa bajeti ambayo wameipitisha itaweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo ikiwemo kumuunga Rais wa awamu ya tano  Dk. John Pombe Magufuli katika kutekeleza azma ya  ujenzi wa viwanda.

Naye Mkurugenzi mteandaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Mussa Gama amesema kwamba atahakikisha kwamba anaimarisha mifumo  yote kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato ya nadani sambamba na kuongeza uzalishaji katika kuwawezesha wananchi kiuchumi  kwa lengo la kuondokana na wimbi la umasikini.

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kisarawe Halfan Sika amempongeza Rais wa awamu ya tano Dk John Pombe Magufuli  katika suala zima la upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa wananchi na kuwaasa wakandarasi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kumaliza tenda wanazopatiwa kwa wakati na ziwe katika ubora unaotakiwa.
 Mbunge wa viti maalumu kupitia Mkoa wa Pwani Zainabu Vullu akichangia jambo katika kikao hicho cha baraza la madiwani halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kwa ajili ya kupitisha mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2019 /2020.

 

Baadhi ya viongozi wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani katika halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, kulia ni Mbunge wa viti maalumu Zainabu Vulu,kati kati ni  Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Mussa Gama na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Hamisi Dikupatile.

Baadhi ya madiwani wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani katika halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. (PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU)



No comments:

Post a Comment