Kituo cha Afya Matimbwa Kata ya Yombo Wilayani
Bagamoyo Mkoani Pwani kimeigharimu Serikali milioni 400 kikiwa kimekalika
tayari kutoa huduma za upasuaji, maabara, mama, mtoto Kituo hicho kitaanza
kutoa huduma hivi karibuni na kuhudumia wananchi zaidi ya 8783.
..................................
Na: Lilian Lundo, MAELEZO, Pwani.
Waganga, Wakunga na Wananchi wa Mkoa
wa Pwani wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa hatua inazozichukua
kuboresha huduma za Afya kwa kutoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa vituo vya
afya na ujenzi wa hospitali za Wilaya mkoani humo.
Pongezi hizo zimetolewa na wadau hao
wa afya mapema wiki hii, huku wakimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa
anazozifanya.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha
Afya Lugoba, Halmashauri ya Chalinze, Dkt. Maganga Kazuri amesema wamepokea
shilingi mil. 400 kutoka Serikali kuu ambapo fedha hizo zimetumika kujenga
majengo matano mapya kituoni hapo ambayo ni jengo la maabara, upasuaji, mama na
mtoto, kuhifadhi maiti na nyumba ya mganga mfawidhi wa kituo hicho.
Amesema maboresho hayo yanawagusa
moja kwa moja wao kama watoa huduma pamoja na wananchi ambao kwa sasa wanapata
huduma nzuri na za kisasa.
“Tulikuwa tunalazimika kuwapa rufaa
wagonjwa kwenda hospitali ya Tumbi au Bagamoyo kutokana na kituo kutokuwa na
huduma ya upasuaji lakini kutokana na maboresho haya huduma hiyo
inatolewa hapa hapa kituoni,” amesema Dkt. Maganga.
Kwa upande wake, Mganga wa Kituo cha
Afya Kerege, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Dkt. Nyangasi Gideon
amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi anazozifanya katika kuboresha huduma za
Afya ambayo imewapa morali wa kufanya kazi na kutoa huduma bora kwa Wananchi.
“Tulianza rasmi ujenzi wa kituo cha
Kerege Octoba, 2017 ambapo kilikamilika Machi, 2018 na kuanza rasmi kutoa
huduma kwa wananchi wa kata ya Mapinga, Kerege na Kiromo, ambapo baada ya
maboresho wakina mama 360 wamejifungua,” amesema Dkt. Nyangasi.
Amesema, kabla ya kituo hicho
hakijafanyiwa maboresho kilikuwa kikipokea akinamama wawili hadi kumi kila
siku.
Aidha amesema, mil. 500 zilizotolewa
na Serikali zimejenga maabara, jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji na
nyumba ya mganga. Fedha hizo zilibaki na kujenga nyumba ya kuhifadhi maiti na
jengo la kufulia.
Nae, Muuguzi Mfawidhi wa Kituo cha
Afya Mkoani, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Immaculate Sangu amesema
maboresho yaliyofanyika kituoni hapo yataondoa msongamano wa wagonjwa ambapo
hupokea wagonjwa 350 hadi 400 kwa mwezi.
“Furaha yangu ni kuona kwamba hata
wagonjwa tuliokuwa tunawapa rufaa kwenda Tumbi sasa tutawahudumia hapa hapa
kutokana na uwepo wa chumba cha kisasa cha upasuaji na chumba cha mionzi”.
alisema Immaculate.
Vile vile mkazi wa Maneromango,
Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Omary Rajab amempongeza Rais Magufuli kwa
kukiwezesha Kituo cha Afya cha Maneromango kufanya maboresho makubwa ya kujenga
majengo matano kwa ajili ya maabara, upasuaji, kuhifadhi maiti, wodi ya wazazi
na nyumba ya mganga.
” Kabla ya maboresho haya
yaliyofanyika huduma zilikuwa duni. Lakini kwa sasa vifaa vipo na waganga pia
wapo, kwa hiyo hata watu wenye matatizo ya mabusha wanafanyiwa upasuaji hapa
hapa,” alisema Omary.
Pia, mwanafunzi wa Chuo cha Afya
Kibaha, anayefanya mafunzo kwa vitendo Kituo cha Afya Maneromango, Anety
Mwandiga amesema uwepo wa vifaa vya kisasa katika vituo vya Afya umemuongezea
ujuzi wa namna ya kutumia vifaa hivyo.
“Namshukuru Mhe.Rais, Dkt. John Pombe
Magufuli kwa maboresho haya ya vituo vya afya inawasaidia madaktari na wakunga
kupenda kazi zao na kufanya kazi zao vizuri, pia kuwahudumia vizuri Wananchi,”
amesema Anety.
Serikali ya Awamu ya Tano chini Mhe.
Rais, Dkt. John Pombe Magufuli katika kutimiza ahadi yake ya kuboresha utoaji
wa huduma za afya nchini. Ilipoingia madarakani ilianza uboreshaji huo
kwa kuanza na ujenzi wa vituo 44 vya afya na kufuatiwa na vituo 74 na sasa
vituo takribani 120 vinaendelea kujengwa maeneo mbalimbali ili kutimiza lengo
la kuwa na kituo cha afya kwa kila Kata.
Muonekano wa majengo mapya katika Kituo cha
Afya Mkoani kilichopo katika Halmashauri ya mji wa Kibaha mkoani Pwani
likiwemo jengo la wodi ya mama na mtoto, chumba cha upasuaji, maabara na eneo
la kufulia.
Jengo la zamani la Kituo cha Afya mkoani
kilichopo katika Halmashauri ya mji wa Kibaha mkoani Pwani kama
inavyoonekana kabla ya ujenzi wa majengo mapya ya wodi ya mama na mtoto, chumba
cha upasuaji, maabara na eneo la kufulia.
Jengo la Wazazi (mama na mtoto) katika Kituo
cha Afya Kerege Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kama inavyoonekana katika
picha ikiwa ni sehemu ya maboresho katika sekta ya Afya yanayowezesha huduma za
upasuaji na maabara kutolewa katika Kituo hicho ambapo upanuzi huo
umegharimu shilingi milioni 500 zilizotolewa na Serikali ukihusisha jengo la
wazazi, maabara, upasuaji na kufulia.
Muonekano wa Kituo cha Afya Kerege Wilayani
Bagamoyo mkoani Pwani katika picha baada ya ujenzi wa majengo mapya na
kuboreshwa kwa huduma katika kituo hicho, na kina uwezo wa kutoa huduma za mama
na mtoto, upasuaji, maabara na kimeanza kutoa huduma machi 2018 na
kimeshahudumia kinamama zaidi ya 360, awali kinamama walikuwa wakipata huduma
ya upasuaji Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Kituo hicho kitahudumia wananchi
zaidi ya 7114.
(Picha zote na Idara ya Habari- MAELEZO)
No comments:
Post a Comment