Friday, February 1, 2019

WAINGIZA MAGENDO PWANI KUKIONA.

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 

JESHI la polisi mkoani Pwani, limeweka bayana kuendelea kukaza uzi, katika kupambana na wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kwa njia za magendo kwa lengo la kukwepa ushuru na kuisababishia serikali kukosa mapato. 


Kutokana na kuchukua hatua hiyo jeshi hilo, limefanikiwa kukamata madumu 86 ya mafuta ya kula ambayo hayajalipiwa ushuru yakiwa yamehifadhiwa ndani ya stoo ya mfanyabiashara Mmas Athumani (35) mkazi wa Kongowe Kibaha mkoani hapo. 


Akieleza juu ya suala hilo, kamanda wa polisi mkoani Pwani, (ACP) Wankyo Nyigesa alisema, madumu hayo yamefikia jumla ya madumu 107  ya mafuta ya kula yaliyokamatwa katika kipindi cha wiki moja.


“Taarifa tumezipata kutoka kwa raia wema, ambapo walieleza mafuta hayo yameingizwa nchini kupitia Bagamoyo na kukwepa ushuru wa serikali kisha kusafirishwa kwa njia za panya hadi kwenye stoo hiyo eneo la Kongowe “alifafanua Wankyo. 


Alitaja mafuta ni dumu moja lita 20 aina ya jenau, madumu 26 ya lita 20 aina ya MTRA pamoja na madumu 59 ya lita 20 aina ya oki. 


Aidha Wankyo alisema, pia limekamata mifuko 18 ya sukari ambayo imeingizwa nchini kutoka nchi jirani kwa kukwepa ushuru. 


Wakati huo huo, wanamsaka mfanyabiashara mmoja ambae kwa sasa jina linahifadhiwa aliyetoroka baada ya kuona maafisa wa polisi wakimfatilia na kutelekeza madumu 21 ya mafuta ya kupikia aina ya Micogold yenye ujazo wa lita 20 kila moja ambayo hayajalipiwa ushuru eneo la Magomeni Bagamoyo. 


Kamanda huyo alitoa wito kwa wafanyabiashara, kuacha kujihusisha na biashara za magendo na ukwepaji wa ushuru katika biashara wanazofanya .


Wankyo aliwapa salamu kwamba, watambue hawapo salama kwani jeshi hilo limejipanga vilivyo kwenye KUTINDUA  mitandao yote ya wafanyabiashara wanaoingiza mali za magendo na ukwepaji ushuru kupitia bandari bubu. 

No comments:

Post a Comment