Wednesday, February 6, 2019

TAASISI YA IFAKARA YAPONGEZWA KWA UTAFITI.


Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa afya ifakara (ihi) Dkt. Honorati Masanja akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo.
 

Mkurugenzi wa huduma za afya ustawi wa jamii na lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe 
...................................................
 
Wataalamu wanaofanya tafiti za magonjwa mbalimbali hapa nchini wametakiwa kulenga mahitaji ya watekelezaji ili tafiti hizo zifanye kazi na kuleta mabadiliko yanayokusudiwa.


Akizungumza katika Mkutano  uliowajumuisha watafiti wa magonjwa mbalimbali uliofanyika mjini Bagamoyo leo February 06, 2019, Mkurugenzi wa huduma za afya ustawi wa jamii na lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe amesema changamoto iliyopo katika maswala ya utafiti ni kufanyika kwa tafiti bila ya kufanyiwa kazi.


Alisema, watafiti sasa wanapaswa kwenda sambamba na mahitaji ya watekelezaji ambao ni serikali.


Alisema changamoto iliyojitokeza kwa miaka kadhaa huko nyuma ni watafiti kufanya utafiti kisha tafiti hizo kutofanyiwa kazi kutokana na sababu mbalimbali.


Aidha, Dkt. Kapologwe ameipongeza Taasisi ya utafiti wa Afya ya Ifakara (ihi) kwani imekuwa ikihakikisha, tafiti inazofanya ni zile ambazo zenye uhitaji kwa mujibu wa mpango mkakati wa Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo ndiyo wizara inayohusika na utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya serikali.


Alisema uwepo wa Taasisi ya ifakara hapa ncini ni kiungo muhimu kati ya serikali na watafiti kutoka sehemu mbalimbali kwani maamuzi yanayofanywa na serikali hutegemea tafiti za kitaalamu kama zinazofanywa na Taasisi ya ifakara.


Aliongeza kuwa, kwa mwaka huu wa 2019 Ofisi Rais TAMISEMI itawasilisha maeneo ambayo yamekuwa na changamoto katika kutolea maamuzi mbalimbali kutokana na kukosekana na takwimu za kitafiti.


Alisema kwa sasa duniani huwezi kufanya maamuzi yoyote bila ya kuwa na matokeo ya kitafiti, hivyo jopo la watafiti ni sehemu muhimu sana katika kutekeleza mikakati mbalimbali ya serikali kwa kutokomeza magonjwa ndani ya jamii.


Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa afya ifakara (ihi) Dkt. Honorati Masanja amesema kituo cha utafiti cha ifakara (ihi) kimeweza kufanikiwa katika tafiti zake ambapo hivi karibuni imefanya utafiti wa chanjo ya Malaria na huenda ikawa ni chanjo ya kwanza kutolewa katika mfumo wa huduma za afya.


Alisema utafiti huo wa chanjo ya Malaria umefanyika kwenye kituo kilichopo Kingani Bagamoyo ambapo Taasisi ya ifakara ilikuwa ni miongoni mwa Taasisi 11 zilizofanya utafiti huo ambao umeonyesha mafanikio makubwa.


Aliongeza kwa kusema kuwa, kufuatia utafiti huo ulifanyika Bagamoyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limapanua wigo na kufanya utafiti huo kwenye  watu wengi zaidi ambapo nchi tatu zinashiriki kufanya utafit huo ambazo ni Ghana, Malawi na kenya.


Dkt. Masanja alisema utafiti huo umezaa matunda na baada ya kukamilika kwa utafiti unaosimamiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) huenda ikawa ni chanjo ya kwanza itakayotumika kwenye mfumo wa kawaida wa utoaji wa huduma za Afya.


Dkt. Masanja ameongeza kwa kusema kuwa, baadhi ya magonjwa yanajitokeza kutokana na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kazi ya watafiti ni kutoa taarifa mapema ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi katika magonjwa.


Alisema katika kufanya utafiti pia wataalamu hao wanafanya utafiti wa magonjwa yenye uhusiano wa binadamu na wanyama kutokana na baadhi ya watu kuishi karibu na mbuga za wanyama hivyo ipo hatari ya magonjwa ya wanyama kuingia kwa binadamu.


Mkutano wa kwanza wa mwaka ambao ambao umewakutanisha wanasayansi wa Taasisi ya utafiti wa Afya ya ifakara (ihi) umefanyika mjini Bagamoyo lengo likiwa ni kupitia mambo mbalimbali ya kiutafiti yaliyofanyika katika kipindi cha mwaka 2018.


Mkutano huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali katika sekta ya Afya wakiwemo wataalamu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Tume ya Sayansi na Teknolojia, Taasisi ya TPRA Arusha, Taasisi ya utafiti ya NIMRI, na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Muhimbili.

 Washiriki wa Mkutano huo wakiendelea na majadiliano. 

Washiriki wa Mkutano huo wakiendelea na majadiliano.

No comments:

Post a Comment