Tuesday, February 19, 2019

TAMPRO SACCOS YAKABIDHI MADARASA MAWILI KIBAHA VIJIJINI.

 Mbunge wa jimbo la Kibaha vijijini Hamood Abuu Jumaa (katikati) mara baada ya kukata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa madarasa mawili katika kijiji cha Mwembengozi ambayo yamejengwa kwa msaada wa TAMPRO SACCOS ya jijini Dar es Salaam, wanaoshuhudia, wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa TAMPRO SACCOS, Shabani Yasini na kushoto ni Meneja wa TAMPRO SACCOS, Saidi Ngolola.
..................................

Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo kilicho chini ya Jumuiya ya wataalamu wa kiislamu Tanzania, (TAMPRO SACCOS) kimekabidhi madarasa mawili yenye thamani ya shilingi milioni 26 katika kijiji cha Mwembengozi kilichopo kata ya Dutumi Halmashauri ya Kibaha vijijini wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa TAMPRO SACCOS, Shabani Yasini amesema ujenzi huo wa madarasa umefanikiwa kwa kushirikiana wanachama wa TAMPRO SACCOS pamoja na wadau wengine ili kuwapunguzia watoto wa kijiji hicho kutembea umbali mrefu kufuata shule.

Alisema wazo la kujenga madarasa hayo ni kutokana na kilio cha muda mrefu kutoka kwa wananchi wa kijiji hicho ambapo shule iliyopo ipo mbali na eneo hilo hali inayopelekea watoto kutembea umbali mrefu kufuata shule.

Aliongeza kwa kusem akuwa, kukamilika kwa ujenzi wa vyumba hivyo viwili kumetokana na ushirikiano kwa wanachama wa TAMPRO SACCOS na wadau wengine mbalimbali.

Alisema ujenzi huo ulianza tarehe 20/11/2018 na kukamilika tarehe 08/02/2019 ambapo mpaka kukamilika madarasa mawili zimetumika shilingi milioni 26.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya tukio la kukabidhi madarasa, Meneja wa TAMPRO SACCOS, Saidi Ngolola amesema hadi sasa TAMPRO SACCOS ina jumla ya wanachama 1800 ambao kati yao wanaume ni 1100 na wanawake ni 700.

Alisema chama kimetoa uhuru kwa wanachama kutoa mawazo yao ili kukiimarisha huku wanachama ndio wafanyaji wa maamuzi katika mambo mbalimbali yanayohitaji kutekelezwa.

Akielezea swala la mikopo kwa wanachama Ngolola alisema chama kina uwezo wa kutoa milioni 60 kila mwezi ambapo mwanachama anatakiwa kurejesha kidogo kidogo bila riba.

Aidha, alisisitiza kuwa, chama hicho Ushirika wa Akiba na Mikopo kinafuata sheria za uislamu katika miamala ya kifedha hivyo kuna mikopo ya aina mbili tu ambayo ni pesa taslimu (mkopo mwema) na pili kukopesha bidhaa (murabaha).

Mgeni rasmi katika makabidhiano hayo Mbunge wa jimbo la Kibaha vijijini Hamood Abuu Jumaa, aliwataka wananchi wa kijiji cha Mwembengozi kutoa ushirikiano kwa TAMPRO SACCOS ili wapate moyo wa kundelea kuisadia jamii ya kijiji hicho.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuishukuru TAMPRO SACCOS kwa msaada huo wa madarasa mawili ambao ni mkombozi kwa wananchi wa kijiji cha Mwembengozi.

Mbune huyo alimtaka Afisa elimu wa Halmashauri ya Kibaha vijijini kushughulikia swala la usajili wa shule hiyo ambayo mpaka sasa tayari ina madarasa mane ili watoto wapate elimu katika shule hiyo.
  Mwenyekiti wa TAMPRO SACCOS, Shabani Yasini  (kushoto) akimkabidhi Mbunge wa jimbo la Kibaha vijijini, Hamood Abuu Jumaa, funguo za madarasa mawili katika kijiji cha Mwembengozi, anaeshuhudia ni Diwani wa kata ya Dutumi, Mkali Saidi.
 
 Mbunge wa jimbo la Kibaha vijijini, Hamood Abuu Jumaa, akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya madarasa mawili yaliyojengwa kwa msaada wa TAMPRO SACCOS ya jijini Dar es Salaam katika kijiji cha Mwembengozi kata ya Dutumi Halmashauri ya Kibaha vijijini Wialaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

 
 Meneja wa TAMPRO SACCOS, Saidi Ngolola akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi madarasa mawili yaliyojengwa na
TAMPRO SACCOS ya jijini Dar es Salaam.
    Wananchi wa kijiji cha Mwembengozi kata ya Dutumi Halmashauri ya Kibaha vijijini Wialaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani, wakishuhudia makabidhiano ya madarasa mawili yaliyojengwa kijijini hapo na TAMPRO SACCOS ya jijini Dar es Salaam.
 
 Muonekano wa jengo la madarasa mawili yaliyojengwa kijijini hapo na TAMPRO SACCOS ya jijini Dar es Salaam.
  Baadhi ya wanachama wa TAMPRO SACCOS wakiwa katika hafla ya kukabidhi madarasa mawili katika kijiji cha Mwembengozi kata ya Dutumi Halmashauri ya Kibaha vijijini Wialaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani, wakishuhudia makabidhiano ya madarasa mawili yaliyojengwa kijijini hapo.

No comments:

Post a Comment