Watu 29 wamekamatwa na Jeshi la
Polisi kwa tuhuma za kufanya utekaji na mauaji ya watoto Mkoani Njombe.
Akiwasilisha bungeni leo Jijini
Dodoma taarifa ya Serikali kuhusu mauaji hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mhe. Kangi Lugola amesema Serikali imeshachukua hatua mbalimbali katika
kutatua na kuzuia matukio hayo sanjari na kutoa maelekezo ya hatua za kupambana
na uhalifu huo ikiwemo kuwatia mbaroni watuhumiwa.
“Mpaka sasa hatua zilizochukuliwa na
Serikali zimefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 29 kwa ajili ya uchunguzi na
mahojiano zaidi na kazi bado inaendelea” ameongeza Waziri Lugola.
Mhe. Lugola amebainisha kuwa, hivi karibuni kumejitokeza matukio
yasiyo ya kawaida ya utekaji na mauaji ya
watoto yaliyokuwa yakihusishwa na imani potofu za kishirikina katika Mkoa wa
Njombe.
“Kufuatia matukio hayo hadi sasa
watoto saba wa umri chini ha miaka 16 wameripotiwa kuuawa, mmoja kujeruhiwa na
wawili kupotea na badae kuonekana, matukio haya yametokea katika
maeneo ya Ikando, Matembwe, Mjimwema, Msitu wa Sekondari ya Njombe, Lukosa,
Sido na Mfekere,” ameeleza Waziri Lugola.
Akifafanua zaidi, Lugola amesema
kuwa, mbali na juhudi za Serikali, Jeshi la Polisi kushirikiana na Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Njombe imechukua hatua mbalimbali kuzuia aina hiyo
ya uhalifu kwa kutumia timu ya wataalamu wa upelelezi kuvisaidia vyombo vya
dola kuchunguza matukio hayo.
Pia kutumia falsafa ya ulinzi shirikishi
wa jamii kwa kutoa elimu mashuleni kwa walimu ili kuweza kuwaelimisha wanafunzi
kuongeza umakini katika mienendo yao, kutumia vyombo vya habari kutoa elimu kwa
wazazi na wananchi kwa ujumla juu ya elimu ya ulinzi na usalama, vikao na
waganga wa kienyeji, viongozi wa dini, Wazee wa Mila, Viongozi wa Kata pamoja
na kufanga doria na misako kwenye maeneo mbalimbali ya misitu na nyumba za
kulala wageni zilizopo pembezoni, ni mbinu zilizotumika kuzuia vitendo hivyo.
Hata hivyo, Mhe. Lugola ametoa wito
kwa wananchi kutojihusisha na matukio hayo na itikadi za kisiasa, imani za
kidini au shughuli za kibiashara.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali
itachukua hatua kwa wale watakaojihusisha na vitendo vya usambazaji wa taarifa
za kichochezi mitandaoni hivyo amewaasa Watanzania kuacha kusambaza taarifa za
uzushi mitandaoni kwa nia yoyote ile kwani ni takwa la Sheria ya
Mtandao.
Mbali na hayo amesema kuwa, Serikali
itahakikisha wote waliohusika na mauaji wanaendelea kusakwa, kuhojiwa na
kufikishwa kwenye mikono ya sheria bila kujali nafasi zao katika jamii.
Hivi karibuni yamajitokeza matukio ya
utekaji na mauaji ya watoto wadogo Mkoani Njombe, jambo ambalo limezua taharuki
mkoani humo na nchini kote kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment